ASKOFU GWAJIMA AJITENGA NA MAJIBU YA KAINI BAADA YA KUMUUWA NDUGUYE ABELI



Adeladius Makwega-MBAGALA


Hivi Karibu Askofu Dkt. Josephart Gwajima, Mbunge wa Kawe na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ametoka hadharani na kufanya mkutano na vyombo vya habari huku akizungumza vizuri na kueleza umma wa Tanzania kile anachokifahamu juu ya hali ya siasa ya Tanzania ya mwaka huu wa 2025, huku kiongozi huyu akilaani wazi wazi juu ya kupinga matukio ya utekaji, uonevu, ukandamizaji na mauwaji yanayoendelea nchini Tanzania.

Ndugu yetu Baba Askofu Dkt. Gwajima amekwenda mbali na kutoa ushauri wa wazi kuwa Tanzania kama nchi inatakiwa kutazama namna viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wanavyoondolewa katika nafasi zao, akishauri hilo linahitaji Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge kuhusishwa ili wawe na nguvu na kwa hali ya sasa viongozi wa vyombo vya ulinzi wanaweza kuondolewa katika nafasi hizo huku pengine wakilinda rasilimali za taifa, akisema kwa sasa tuna wajibu wa kuweka utaratibu huo ndiyo kusema kama sheria/ Katiba ibadilishwe.

Mwanakwetu wa Mbagala kwa nafasi yake binafsi kabisa anampongeza Baba Askofu Dkt.Gwajima kwa maoni haya na anapaswa kupongezwa kwa kutoka hadharani na kutoa maoni yake juu ya namna ya kuendesha taifa hili, maana kinyume chake tunapokaa kimya hakuna aijuaye kesho na lipi linakuja?


 

 

Pongezi za Mwanakwetu kwa Baba Askofu Dkt.Gwajima naomba zikufikie hapo ulipo,

“Baba Askofu Gwajima utapokuwa unayasoma makala haya nakuomba ukimaliza sali sala ile aliyotufundisha Bwana Wetu Yesu Kristo na sala hii Baba Askofu nakuomba kwa hisani yako uisali mara tatu, nakuomba uisali mara tatu huku Mama Askofu akiwepo na kama Mama Askofu yu mbali basi sali nae huku ukiwasiliana naye kwa njia ya simu, kisha endelea na shughuli zako.”

Kwa kuwa mimi ni mwana CCM na Baba Askofu Dkt.Gwajima ni mwana CCM mwezangu, nakuomba ufahamu hili, ulichokifanya ni kitu cha kizalendo ambapo ndivyo inavyotakiwa Mwana CCM wa Kweli, narudia kusema Mwana CCM wa Kweli anavyotakiwa awe maana sasa wapo Wana CCM aina mbili wa Kweli na wa Uwongo.

“Kwa hakika Baba Askofu Gwajima ni MwanaCCM wa Kweli.”

Naomba Baba Askofu Gwajima urejee Azimio la Mkutano Mkuu wa Pamoja wa TANU na ASP lililofanyika Januari 21, 1977 yapo mambo matatu yaliyozungumzwa kwa Pamoja baina ya TANU na ASP mojawapo ni kuvunjwa kwa TANU na ASP na jambo la pili lilikuwa vyama hivyo vinavyovunjwa siyo kwamba vimeshindwa kazi, bali wanaongeza nguvu ya pamoja na jambo la mwisho walilokubaliana ni hili;

“Tumeamua Kwa pamoja kuunda chama kipya, kuendeleza Mapinduzi ya Kijamaa nchini Tanzania na Mapambano ya Ukombozi ya Bara zima la Afrika juu ya msingi iliyowekwa na TANU na ASP. Chama tunachounda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini na kupambana na jaribio lolote la mtu kumuonea mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au kuzorotesha maendeleo ya taifa.

Chama tunachounda tunataka kishike Barabara hatamu za uongozi wa shughuli zote za umma kwa maslahi ya Wakulima na Wafanyakazi wa taifa letu. Chama tunachokiunda tunataka kiwe kiungo kati ya Wanamapinduzi wa Tanzania na Wanamapinduzi wenzetu popote walipo.”

Baba Askofu Gwajima kwa heshima zote nakuomba urejee vizuri hili Azimio la Pamoja la wazee wetu wa TANU na ASP hasa maneno haya;

“Chama tunachokiunda kifutilie mbali aina zote za unyonyaji nchini na kupambana na jaribio lolote la mtu kumuonea mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi…”

Haya ninayoandika Baba Askofu Dkt. Gwajima yapo katika kurasa za mwanzo mwanzo za Katiba ya CCM ambayo kila Mwana CCM anayo lakini je yanayofanyika hayakiuki azimio hili? Kwa hakikakinachofanyika sasa ni kukiukwa kwa Azimio hili.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika huu utekaji uliofanywa dhidi ya Mdude Nyagali, dhidi ya Kijana Shedraki Chaula dhidi ya shambulio la Padri Charles Kitima, hata mauwaji ya Ali Mohammed Kibao na matukio yote yaliyofanyika dhidi ya uzalilishaji wa utu wa binadamu tangu mwaka wa 2015 hadi sasa 2025 hayakubaliki kufanyika katika ardhi ya Tanzania, kwa hakika haya yote ni majaribio ya uonevu na udhalilishaji wa wananchi lazima tuyalaani kwa kauli moja.


 

Baba Askofu Dkt.Gwajima kwa hakika wewe binafsi umejitenga ni majibu ya Kaini mara baada kumuuwa nduguye Abeli kama kinavyodokeza kitabu cha Mwanzo sura ya 4,9-10.

“BWANA akamwambia Kaini yupo wapi Abeli ndugu yako ? Kaini akajibu sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? BWANA akasema umefanya nini maana sauti ya damu ya ndugu yako inanililia, kutoka katika ardhi.”

Kwa hakika Mwanakwetu anatoa heko na hongera tele kwa Baba Askofu Gwajima kwa kujitenga na majibu haya ya Kaini ya mimi si mlinzi wa ndugu yangu.Viongozi wengine ndani ya CCM wajitathimini kama kuendelea kupingana na alichokisema Baba Askofu Gwajima au kukubaliana nacho kama wanapingana nacho huko ni kuendelea kutoa majibu ya Kaini baada ya kumuu nduguye Abeli na pia kupingana na Azimio la TANU na ASP Januari 21, 1977.


 

Mwanakwetu upo?

Je makala haya niyaitaje? Askofu Gwajima Ajitenga na Majibu ya Kaini Baada ya Kumuuwa Nduguye Abeli, Wanapingana na Azimio la TANU na ASP au Askofu Gwajima ni MwanaCCM wa Kweli? Mwanakwetu anachagua Askofu Gwajima Ajitenga na Majibu ya Kaini Baada ya Kumuuwa Nduguye Abeli

Mungu ambariki Baba Askofu Dkt.Gwajima.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 




















 





0/Post a Comment/Comments