AHF YAPIGA JEKI HIV NA UKIMWI

 


Adeladius Makwega–Musoma MARA

Ni majira ya mchana ya Mei 6, 2025 Katibu Tawala Mkoa wa Mara, ndugu Gerald Msabila Kusaya amepokea vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 43.5 za Kitanzania kutoka AHF Shirika la Kimataifa Lisilo la Kiserikali ambalo linajihusisha na mkakati wa kufanikisha udhibiti wa HIV na UKIMWI duniani.

“AHF ni wadau wetu wakubwa katika mapambano dhidi ya HIV na UKIMWI, ninawashukuru sana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mara, Mhe Kanali Evans Mtambi, ninaungama mbele yenu kuwa vifaa hivi tutavitunza vizuri, vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa lakini BI Aika Mtui, mama yangu ninapokushukuru hapa leo hii hadharani maana yake tunaendelea kuomba tena, kama mkipata tena uwezo huo jamani msisite kutoa msaada zaidi kwa mkoa wetu wa Mara, maana leo hii umegusa wilaya mbili na vituo vitatu tu vya afya. Mbele yako ninawaagiza Wakurugenzi wa Wilaya za Tarime na Rorya vifaa hivi vitunzwe na vifanye kazi iliyokusudiwa ili mabadiliko yaonekane kwa yale malengo ambayo tulikuwa hatujayafanikisha na tuyafanikishe.”

Akizungumza mbele ya jua kali linalowaka kandoni kwa Hafla hii fupi Dkt. Khalifan Lekizenda, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya aliungama hadharani kuwa .

“Hivi vifaa vilivyopokelewa hapa kwa niaba ya vituo vyetu vya Afya vya Utegi na Changuge ni vitu muhimu ili kuboresha huduma zetu ziweze kuimarika mathalani pikipiki zitawatafuta na kuwafikia wagonjwa waliotoroka dawa ili waendelee na matibabu , bado hawa wateja wanapokuja katika vituo vyetu taarifa zao zinatakiwa kuhifadhiwa, tumepewa kompyuta na runinga kwa ajili ya kutoa elimu kwa wagonjwa.”

Kwa upande wao Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mganga Mkuu wa Wilaya hii Dkt. Amini Wasomana alisema kuwa Kituo cha Afya cha Nyangoto ndiyo kinachopokea vifaa hivyo kutoka AHF huku akikumbuka na hili,

“Ninawashukuru sana AHF kwa kutupatia vitendea kazi hivi japokuwa changamoto ni nyingi kwa dhati kabisa vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kuwafikia wenzetu wenye HIV na UKIMWI.”

Kwa upande wake Dkt .Omari Jamuya ambaye ni Mratibu wa Huduma za Kudhibiti UKIMWI na Magonjwa ya Ngono na Homa ya ini Mkoa wa MARA aliwashukuru wadau kwa vifaa walivyotoa,

“Hivi ni vifaa muhimu kwa VVU na UKIMWI na bado mpaka sasa kwa utafiti wa mwaka wa 2022/2023 Mkoa wa Mara una maambukizi asilimia 5 ambayo ni juu ya hali ya wastani wa maambukizi ya kitaifa.”

Awali akizungumza katika hafla hii Meneja Mkazi wa AHF kwa Tanzania Bi Aika Mtui alisema kuwa shirika lao linafanya kazi kwa miaka karibu 40 sasa dunia nzima.

“Kwa sasa tupo katika nchi 52, tunashirikiana na Wizara ya Afya ya Tanzania kwa magonjwa ya Kifua Kikuu na Magonjwa yote ya Ngono kwa mikoa miwili tu ya Mara na Simiyu baada ya kufanya uchambuzi yakinifu ili kuboresha huduma hizo.Ninatoa ahadi kuwa AHF itaendelea kutoa msaada kwa Mkoa wa Mara kulingana na bajeti yetu ya mwaka husika”

Vifaa vilivyopokelewa ni Kompyuta za mezani zenye thamani ya shilingi milioni 15,222,000/=, Simu za mkononi za kisasa zenye thamani ya shilingi milioni 2,690,000/=, Printa zenye thamani ya shilingi 6,018,000/=, runinga zenye thamani ya shilingi 5,133,000/=, vihifadhia kumbukumbu venye thamani ya shilingi 672,000/=, Pikipiki zenye thamani ya shilingi milioni 13,500,000/=.


 

Mara baada ya zoezi hilo halmAshauri ya Rorya na Tarime zilibeba vifaa vyao na kuvipeleka vifaa hivyo kuanza kutumika dhidi ya mapambano ya HIV naUKIMWI mara moja.

Wakati haya yakifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, hali ya Hewa ya Mji wa Musoma ilibahatisha kupata mvua kwa siku mbili mfululizo yaani Jumamosi na Jumapili.

makwadeladius@gmail.com

0717649257







 





 

0/Post a Comment/Comments