SERIKALI KUU NA SERIKALI ZA MITAA ZIIMBE WIMBO MMOJA

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Mwanakwetu alikuwa Kijijini Chamwino Ikulu, mkoani Dodoma huku akiimwagilia miwa yake , kwa kuwa zoezi la kuimwagilia mimea hiyo ni nzito kama hauna zana bora hivyo baadhi ya vitu vilivyokuwa mfukoni mwake aliviweka katika benchi ili visiloane ikiwamo simu yake ya mkononi maana Mwanakwetu ni kabwela simu ikiharibika kuinunua nyingine ni kazi, siye akina pangu pakavu tia mchuzi.

Akiwa anaendelea kuimwagilia mimea hiyo gafla smu ikaita na kuacha zoezi la kumwagilia na kwenda kuipokea.

“Samahani baba , mimi ninaitwa… ni mjumbe wa Kamati ya Chakula ya shule ya sekondari ya Ilomba Mkoani Mbeya. Hapa kuna kijana wako anaitwa Francis Makwega wa kidato cha nne anadaiwa pesa ya chakula cha mchana na pesa ya kambi maana kidato cha nne Bodi ya Shule imeamua wakae kambini hadi watakapomaliza mitihani yao ya kidato cha nne. 

Kwa simu hii baba yangu tunakuomba ulipe pesa hiyo, wakija kambini waje na magodoro, shuka na blangeti. Jambo la mwisho la muhimu katika ujumbe huu kila vinapoitishwa vikao vya wazazi/walezi tunawaomba wazazi/walezi muwe mnashiriki.”

Simu inapigwa kutoka Mbeya, nadhani shule hii ipo katika jimbo la Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Msomaji wangu tambua kuwa shule hii ni ya umma ipo Mbeya na anayepigiwa simu yupo Dodoma ambapo ni umbali wa KM kama 600.

Msomaji wangu kumbuka pia Mwanakwetu yupo shambani kwake na anamwagilia mimea yake na hapo ametoka kupokea simu ya mkononi kutoka kwa Mjumbe wa Kamati ya Chakula ya Shule ya Sekondari Ilomba ambapo kijana wa Mwanakwetu mwenye jina la Francis Makwega alikuwa anasoma wakati huo.


 

Kwa kuwa Mwanakwetu anamwagilia mimea yake milio wa simu yake siyo mkali sana na anapoimwagilia maji yana presha kubwa, kwa hiyo inapopigwa hawezi kuisikia kwa haraka hivyo basi akaamua afungue redio katika simu yake kisha awe anaisikiliza redio hiyo ikiwa inarusha matangazo na kama simu itapigwa redio itakata hivyo atatambua simu imepigwa, hapo hapo akaiwasha redio mojawapo ya hapo Dodoma na kuisikiliza huku akimwagilia mimea yake.

Redio hii ikawa inaimba wimbo wenye maneno haya;

“…All of those things that we've been through
Used to make me happy, now make me blue
I didn't believe the things that I've heard, no
But now I've seen it with my own eyes
I know action speak louder than word

But Lord know that I don't wanna be lonely tonight
Granny know that I don't wanna be lonely tonight
I mean it, yes I mean it I don't wanna be lonely tonight
But I would rather to be lonely than to live a dirty lie

I'm so sorry we been through
I'm so fed up I don't know what to do…”

 

Sauti ya muimbaji ilimjia Mwanakwetu akilini mwake kuwa ni Gregory Isaack na wimbo aliukumbuka kuwa ni Front Door ambao ulitolewa hadharani mwaka 1981 katika mtindo wa Strong Reggae.

 

Mwanakwetu huku akimwagilia mimea yake alikumbuka kuwa wimbo huo ni wa mapenzi huku mkongwe Gregory Isaack akihusianisha mapenzi na mpenzi kama mlango wa mbele ambapo nyimbo nyingi za ndugu huyu zimekuwa za hisia za mapenzi. 

 

Redio inaendelea kuimba nyimbo zingine zingine akili ya Mwanakwetu ikamjia juu ya Milango Miwili; Mlango wa Mbele na Mlango wa Nyuma.

 


 

 

Msomaji wangu pia kumbuka kabla ya Mwanakwetu kuiwasha redio katika simu yake na kabla ya kuusikiliza wimbo wa Gregory Isaack Mwanakwetu alipigiwa simu juu ya Chakula cha Mchana na Pesa ya Bweni ya Kijana wake.

 

Mwanakwetu akasema moyoni maneno haya,

 

“Suala la Chakula cha Mchana Shuleni na suala la Wanafunzi kukaa bweni kwa shule za kutwa ni jambo la muhimu sana lakini kwanini jambo hili linaachiwa Kamati ya Shule? Hili jambo jamii ingeambiwa mapema tu na linapaswa kuwepo katika fomu ya kujiunga za mwanafunzi ili mzazi ajiandea mapema na mwanafunzi aweze kupatiwa mahitaji yake muhimu mapema.

 

Serikali Kuu ingesema wazi kuwa yenyewe inalipa mishahara ya walimu na mambo mengine wazazi/ walezi wawajibike kwa chakula cha mchana na hii hoja ya Elimu Bure kupigiwa chapuo iondoke.

 

Kwa Hiyo Serikali Kuu inasema Elimu Bure huku Serikali za Mitaa jamii inahangaika kukusanya michango ya chakula cha mchana.”

 

Mwanakwetu anaendelea kumwagilia mimea yake huku akitafakari juu ya suala hili la elimu bure na michango mashuleni.Mwanakwetu akasema hapa tunatumia Mlango wa Nyuma katika kufanikisha Elimu huku katika Mlango wa Mbele tunasema elimu bure.

Kwa hiyo Mwanakwetu huu wimbo wa Front Door wa Reggae ukampa tafakari kubwa juu ya Serikali ya Tanzania inawajibu wa kuacha kutumia uchangishaji wa elimu kwa kupitia mlango wa nyuma yaani Serikali za Mitaa bali itumie mlango wa mbele yaani Serikalia Kuu na kila mmoja ajue hilo na kuacha kulipiga chapuo la elimu bure na ndiyo maana suala la kufanikisha wanafunzi kula chakula cha mchana katika shule za nyingi za umma bado halijafanikiwa kabisa isipokuwa Mkoa wa Kilimanjaro peke yake.

Mwanakwetu alipomaliza kumwagilia mimea yake alibeba simu yake na kuiweka mfukoni na kurudi nyumbani kwake na kuamua kuyatarisha makala haya.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Suala la uchangiaji katika shule za umma alikwepeki ni jambo la lazima kwa kila mmoja wetu awe mzazi/mlezi, lakini mafanikio ya uchangiaji mashuleni nchini Tanzania yanaweza kuleta tija kama Serikali Kuu itaacha kutumia mbinu ya uchangia kwa kutumia mlango wa nyuma yaani Serikali za Mitaa.

Maana Serikali Kuu inapiga chapuo la elimu bure , huku kamati za shule zinahangaika kukusanya michango ya chakula cha mchana, kama Serikali Kuu ingepigia chapuo wananchi kuchangia chakula cha mchana jambo hili lingekuwa jepesi, Mwanakwetu anaamini Serikali za Mitaa  kuifanya kazi hii peke yake , peke yao ni kuwatwisha mzigo mzito, mzigo mzito tuubebe sote.

Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Bunge wanaimba wimbo wa elimu bure lakini Halmashauri zinaimba wimbo wa michango michango michango ya chakula cha mchana. Lazima Rais, Waziri Mkuu,Mawaziri wote na Bunge wangesema hadharani na kurudia rudia  hilo kila mara kama inavyotamkwa sasa MITANO tena  jamii ingetambua umuhimu wa CHAKULA CHA MCHANA SHULENI.

Chakula cha Mchana shule za kutwa iwe ajenda ya kudumu katika vikao vyua hadharani na siyo vikao vya ndani tu, vikao vya  ndani  hawapo wachangiaji, hawapo wenye watoto shule za kata. Chakula cha Mchana iwe ajenda ya kila waziri, iwe ajenda ya Serikali Kuu na Iwe Ajenda ya Bunge.

Dunia hakuna cha bure, Mwanakwetu anatambua shida wanasiasa wanataka kutumia Elimu Bure kama karata ya uchaguzi, hilo siyo sahihi hilo halikubaliki, sote tuimbe wimbo mmoja.

 

 


 

Serikali Kuu na Serikali za Mtaa Ziimbe Wimbo Mmoja

Mwanakwetu Upo?

Je makala haya niyaitaje? Elimu bure ni Karata ya uchaguzi Mkuu? Michango Shule Za Umma Isitumie Mlango wa Uani? Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Ziimbe Wimbo Mmoja? 

Mwanakwetu anachagua Serikali Kuu na Serikali Za Mitaa Ziimbe Wimbo Mmoja.


Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

NB Makala haya yametayarishwa na Mwanakwetu kwa heshima zote kwa Binamu Yake  Mpendwa  Msekwa Njama ambaye ni Mwalimu wa sekondari katika Jiji la Dodoma nchini Tanzania.

 












 

0/Post a Comment/Comments