Msomaji wangu! Nakualika tena katika makala ya Katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi wa katuni ambapo mtayarishaji wa makala haya uchagua katuni nne na kuzielezea kama zilivyochora na kisha kufanya uchambuzi wa katuni hizo moja baada ya nyingine.
Kuianza safari ya makala haya Mwanakwetu akiwa kandokando ya kuta za Mahakama Kuu ya Tanzania, inayoongozwa na Profesa Ibrahimu Juma , Mwanakwetu ameikamata katuni nambali moja ambayo inamuonesha kipanya na kijana wake , kijana huyu wa anasema Eti Baba mtu mzima akiwa hana pesa huwa anakuwa na hasira? Kipanya anajibu swali hilo kwa kusema kuwa Ntakunasa makofi asa hivi.
Mtoto wa kipanya anakuwa mpole na kutokomea mbali, huku akiguna, Duuu! Kijana wa Kipanya hapo akiwa amehakikisha mambo mawili; moja kumbe ni kweli mtu asiye na pesa huwa na hasira na jambo la pili kumbe hata baba yake siku hii hana pesa, msomaji wangu kumbuka tu Katuni hii imechorwa na alwatan Masoud bini Kipanya.
Mwanakwetu anaingia katika geti la Mahakama Kuu ya Tanzania akienda kumsalimu Jaji Mkuu wa Tanzania huku akiikamata katuni yake ya pili ambayo imechorwa na King Kinya hapa akionekana jamaa mmoja amelala kitandani, jamaa huyu sura yake inafanana na mwanasiasa wa Tanzania Tundu Lissu akiwa amelala fofofo huku akionekana kana kwamba kama yupo ndotoni.
Huyu Tundu Lissu anaonekana anamuota kijana aliyeva skafu ya kijani akimkodolea macho, nayo sura yake kajificha akiwa ameshika kamba nadhani ni kitanzi.
Kwa kuitazama katuni hii inaonesha ilichorwa Februari 17, 2025 lakini maudhui yake yanaonesha kana kwamba imechorwa baada ya Tundu Lissu kupelekwa Kolokoroni kwa Makosa ya Uhaini ambapo kwa sasa sarakasi zipo katika mahakamani ya Tanzania inayoongozwa na Jaji Profesa Ibrahimu Juma. Kwa hakika bado Mwanakwetu anaendelea kupinga Profesa Jumaa kuongezewa muda wa kuiongoza Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa katuni hii inaonesha japokuwa Tundu Lissu yupo Kolokoroni lakini kauchapa usingizi wa amani huku akiota hukumu yake. Jambo linalompa matumaini mtayarishaji wa makala haya ni Tundu Lissu kuweza kuuchapa usingizi wa amani na kuweza kuota, hili ni jambo la matumaini lakini hatima ya shauri hili mbele ya Mahakama ya Tanzania inayoongozwa na Profesa Ibrahimu Juma ajuaye ni Mwenyeezi Mungu.
Huku wanaolitazama shauri hili wakiwa na maswali mengi kwa Polisi ya Tanzania, sawa Tundu Lissu pengine amefanya kosa vipi waliomshambulia mwanasiasa huyu mbona polisi hawajatimiza wajibu wao?
Mwanakwetu akiwa katika ngazi za Mahakama Kuu ya Tanzania sasa anakutana na katuni ya tatu iliyochorwa na King Kinya ambapo kuna maneno manne; NO mara mbili na Election na Reform haya maneno hayya yamepigwa pingu na jamaa ambaye anaonekana kama amevaa sare za Polisi ya Tanzania huku kukiwa na V mbili zilizocheza tiki taka.
Kwa uhakika katuni hii inatoa taswira za siasa za Tanzania tangu mapema ya Februari, 2025 hadi Aprili, 2025 ambapo CHADEMA walikuwa na harakati zao kwa hakika harakati zao zimepunguzwa kasi kwa ukamatwa kwa Tundu Lissu na na sasa Tundu Lissu Mzaliwa wa Singida Tanzania , mwanasheria nguli amelala katika kuta za Magereza ya Tanzania kama mahabusu kwa tuhuma za uhaini ambapo hukumu yake ni kunyongwa.
Mwanakwetu sasa anaingia katika kuta za Mahakama ya Tanzania na kuangalia maboresho makubwa ya Mahakama ya Tanzania hususani majengo makubwa makubwa, akiwa hapa Mwanakwetu anakutana na katuni inayomuonesha jamaa mmoja aliyeva mavazi kama ya kijaji huku sura yake ikilingana na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma, katuni hii imechorwa na King Kinya, huku jajia huyu akiwa ameketi katika kiti chake na akishangaa jambo, Mwanakwetu hafahamu Jaji Mkuu wa Tanzania alikuwa anashanga nini. Swali hilo Mwanakwetu anaona ni vigumu kumuuliza Profesa Ibrahimu Juma mwenyewe lakini Mwanakwetu anaweka miaadi na wewe msomaji wake kuwa atamuuliza King Kinya akikutana naye.
Mwanakwetu kwa katuni hii kwa kuwa yupo katika kuta za Mahakama Kuu ya Tanzania anabebwa mzega mzega hadi Februari 3, 2025 Katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma, kukiwa na shughuli ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Jumaa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia suluhu Hassan, Profesa Jumaa alizungumza kwa dakika 33 na miongoni mwa maelezo yake ya mwishoni mwishoni yalikuwa haya,
“Katika historia ya Tanzania (Tanganyika) Jengo lililokuwa linatumika ni lile la pale muembeni. Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete aliwahi kututania kuwa jengo la Mahakama Kuu lilikuwa Bar… Mhe Rais itakuwa heshima kubwa pale utakapotupa funguo…mwaka 1958 ulikuwa ufunguo wa fedha…kwa sasa kwa sababu nchi yetu ina utajiri mkubwa wa dhahabu ikukupendeza kama utatupatia ufunguo wa dhahabu na tutautunza…”
Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma Katikati ya mazungumzo yake siku hiyo pia aliyasema maneno haya,
“Mhe. Rais kipekee ninapenda kukushukuru wewe na Serikali unayoiongoza…katika dira ya 2050 kutakuwa na uwezeshaji wa kutosha ili rasilimali pesa isiwe kizingizio … nakushukuru kwa kutupatia dola milioni 61 na dola milioni 91 kutoka Benki ya Dunia, tunakushukuru sana sana kwa hilo...”
Mwanakwetu alitafakari hizo dola milioni 152 kutoka benki ya dunia kwa awamu mbili, kwa hakika maana yake fedha hizi ni mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo umeifikia Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kulingana na taarifa za nambali za kubadilisha fedha Aprili 29, 2025 Dola Moja ya Marekani ni sawa na shilingi 2693.43 za Kitanzania. Dola hizo Milioni 152 ni sawa na shilingi 409,402,360,000 ambapo ni Shilingi za Kitanzania Bilioni 409.4 kwa hesabu za Mwanakwetu, lakini yaweza kupungua au kuongezeka kutokana na muda na siku fedha hizo zilivyopokelewa na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mwanakwetu anaona kuwa kwa sasa Watanzani tuna wajibu wa kufuatilia matumizi ya fedha hizo, je zinatumika sahihi katika mahakama zetu? Au fedha hizo zilipaswa kutumika katika Nyanja zingine kama za Tiba, Elimu na Kilimo? Maana mahakama haizalishi chochote, yenyewe inatoa huduma tu kwa jamii ya Watanzania ya kuyatatua mashauri yanayokwenda hapo. Je ilikuwa sahihi kwa Serikali kuipa mahakama ya Tanzania Dola Milioni 152 za mkopo?
Jambo la mwisho ni Mahakama Kuu ya Tanzania kuomba ufunguo wa dhahabu, hili Mwanakwetu anapinga kabisa Mahakama ya Tanzania kupewa ufunguo wa dhahabu, kama mkoloni hakuipa mahakama ufunguo wa dhahabu, kwanini leo hii Mahakama Kuu ya Tanzania ipewe ufunguo wa dhahabu na tena kwa kuomba? Hayo ni matumizi mabaya ya rasilimali za taifa hili, Jaji Mkuu anapaswa kuomba maboresho ya mishahara ya watumishi wa mahakama na siyo mahakama iombe ufunguo wa dhahabu. Mahakama ya Tanzania lazima iwe mfano wa kukwepa matumizi yasiyo ya lazima ili Serikali na Bunge vijifunze katika hili. Tanzania ni taifa la watu masikini, watu chakula kupata ni tabu , maji safi na salama ni tabu leo hii mahakama inaomba ufunguo wa dhahabu? Hili halikubaliki. Mwanakwetu anamshauri Rais wa Jamhuri ya Tanzania wa Tanzania asiipe Mahakama ya Tanzania Ufunguo wa Dhahabu.
Mwanakwetu upo?
Basi hadi hapo ndiyo mimi natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka nilikuwa na katuni nne zilizokusanywa na mtayarishaji wetu; ya kwanza ni kipanya na swali la mtoto wake kuwa watu wazima wakiwa hawana pesa huwa wanakuwa na hasira, ya pili ni ile ya ndoto ya Tundu Lissu Kolokoroni , ya tatu ni ile ya pingu za No reform no election na ya nne ni hii mshangao wa jamaa anayefanana na jaji Mkuu wa Tanzania.
Kumbuka,
“Mahakama ya Tanzania Isipewe Ufunguo wa Dhahabu.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
NB -Makala haya ya katuni yametayarishwa kwa heshima zote kwa binamu wa Mwanakwetu Bi Msekwa Njama ambaye ni mwalimu wa Sekondari Jijini Dodoma.
Post a Comment