Adeladius Makwega-Musoma MARA
Leo hii nimeikumbuka haiba ya mama mmoja ambaye aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne. Msomaji wangu usione gere, leo Mwanakwetu na haiba ya mama waziri wa zamani? Nasema Naaam HAIBA WAZIRI WA ZAMANI? Tambua kuwa kila mmoja wetu anavyo vitu anavyovipenda.
“Waziri huyu alikuwa mama mmoja mrefu, mwembamba, maji ya kunde, akibadilisha nguo za rangi tafauti, hayo yote tisa kumi ni ule mtindo wa nywele zake. Ehee alikuwa anavaa wigi? Alikuwa akiweka dawa nywele zake na kuchana mitindo mbalimbali kama vile Bob, Bati, Moja kwa moja, Mkeka ,yeboyebo au mingine mingi? ”
Huko kote Mwanakwetu sipo.
“Siye Waswahili tuna mitindo mingi ya nywele, mathalani Mwali Anatoka Mkoleni, Mwali Anakwenda Mkoleni, Kilimanjaro, Kukata nywele, Mabutu na Upara.”
Mabutu husukwa kulingana na upenzi wa msukwaji kama yanasukwa mawili au zaidi ya hapo. Mabutu hayo yanaweza kuwekewa nyuzi au bila nyuzi. Upara nao ni mtindo mwingine huo hupakwa mafuta mengi huku ukimiminiwa na ufuta hasahasa bibi harusi akiwa anaolewa au akiwa anatolewa nje baada ya kukaa ndani. Je Mwanakwetu nimeangukia wapi?
“Wakati wote niliyojaliwa kumuona waziri huyu wa zamani, macho yangu yalialikiwa na tabasamu zito lililopambwa na nywele za mtindo wa twende kilioni, nywele zake zilikuwa mithili ya maua yaliyoota mlimani katika bustani nzuri ya mfalme. Macho yangu yalipoutazama mtindo huo, yalinipa hamu ya kutamani sana kukishika kichwa hicho cha mheshimwa waziri wetu wa zamani, ningekuwa mtoto ningedanganya kwa kumsalimia kwa kumshika kichwa ili ile kiu yangu ikatike lakini sifa ya utoto Mwanakwetu sina. Mie ni mkubwa, baba na midevu yake kibali cha kufanya hivyo sina. Nina hakika mwenye kibali cha kufanya hivyo kwa mheshimiwa huyo yupo na Mwanakwetu akimuone gere huyo mwenye kibali hicho “
Swali lililobaki moyoni mwangu tangu wakati huo hadi sasa, je kama kuzishika bila kibali ni kosa kama sheria ya SOSPER inavyonadi, je kuusifia mtindo wa nywele hizo za mheshimiwa wetu ni kosa?
Ebu nikague simu yangu kama bado ninayo namba simu ya Mh Jaji Mstaafu Bi Agusta Bubeshi nimuulize ili nibaki kuwa salama lakini naona hakuna kosa labda kuna haja ya kufunga safari hadi parokiani kwangu kumuuliza Baba Padri/Baba Mchungaji juu ya hili la kusifia mtindo huu wa nywele wa mheshimiwa wetu wa zamani.
“Je kweli kusifia itakuwa dhambi, hilo siamini.”
Yote hayo ni ya waziri wa zamani, Fenera Mukangara Dkt aliyechagua mtindo wa Twende Kilioni ambapo huko ndipo moyo wangu ulipo, kwa hesabu zangu Mheshimiwa Fenera Mukangara hupenda kusuka nywele 16, yaani 16 kichwa, moja ,mbili tatu…hadi ya kumi na sita. Kwa hakika mtindo wa Twende Kilioni umemtambulisha mno mheshimiwa Fenera Mukangara lakini pia ametuwakilisha vizuri katika utamaduni wetu siye makabwela kwa kuusuka mtindo huo kila mara.
“Yule Waziri aliyekuwa akisuka twende Kilioni, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi!”
Hapo makabwela wanamkumbuka Fenera Mukangara huku wakiusifia mtindo wake wa nywele. Nyumbani kwetu Mbagala Sabasaba Dar es Salaam kuna mama mmoja maarufu mno anaitwa Mama Amina Ngwele aka Mama Mchafu, mama huyu na binti zake ni wasusi wazuri sana wa aina mbalimbali za nywele, nilipowauliza juu ya gharama za kusuka twende kilioni walicheka sana.
“Kaka unaulizia kusuka twende kilioni unataka kumleta shemeji yetu kusuka? Kaka acha ubahiri ”
Niliambiwa, Nikajibu hapana, wakacheka sana wakasema kaka huo mtindo tunasuka bure, huo ni kama kachumbari katika pilau, lakini mitindo mingine ni pesa yako tu kati ya Tsh 5,000-70,000/-
“Lakini kaka, mwanamke akisuka twende kilioni anajiamini sana, hakuna kusema nywele zimetimka wala zitaanguka chini, hapo unahitaji tu kuziosha vizuri, kuziweka mafuta ya maji na unazisuka vizuri.”
Aliniambia Mama Mchafu. Mwanakwetu binafsi ninaupenda sana usukaji wa mheshimiwa Fenera Mukangara wa Twende Kilioni, wanaume wengine wataanza kuleta nongwa ohh Mwanakwetu anamsifia sana Dkt Fenera , ehee namsia maana anapendeza, nawaomba wengine pendeni mitindo mingine hata ya magauni, madela vitenge , mitindo viatu, namna wnavyotembea , maumbile yao hata macho kumchuzi wewe chaguo kimoja lakini huu mtindo wa twende kilioni ni wangu mie Mwanakwetu Mwana wa Mbagala.
.
Kwa sasa sifahamu mheshimiwa Fenera Mukangara alipo, lakini popote ulipo mh Dkt,
“Nakualika kwa heshima na taadhima uje kusuka mtindo huu kwetu Mbagala Sabasaba na nina hakika Mama Mchafu ataweza kutoa 32 kichwa ya twende kilioni yaani moja mbili , tatu …hadi ya thelathini na mbili kwa heshima yako Dkt Mukangara.
Usiniangushe Dkt Fenera upatapo ujumbe huu nijulishe ili ndugu zangu wa Mbagala wajiandae kukusuka kabla ya Pasaka ya mwaka huu wa 2025. Nilitamani makala yangu yakufikie kwa siri lakini nimeweka hadharani ili ndugu zangu watambue husuda yangu hii ya tangu mwaka 2014 kwa mtundo huu wa twende kilioni unaopamba wajihi wako.”
Mwanakwetu upo?
Kumbuka.
Mwanakwetu na Husuda ya Twende Kilioni cha Dkt Fenera Mukangara.
makwadeladius@gmail.com
0717649257











Post a Comment