Adeladius Makwega-Musoma MARA.
“Kuna mito miwili mikubwa lakini upo mto mmoja mkubwa na una mamba wengi wakali, ebu fikiri mtu ameuwawa kikatili anabebwa hadi kando ya mamba anakuwa chambo, anatupwa katika mto wenye mamba wengi na jamaa walivyo mafirauni wanakaa kando hadi mamba waje kula wakihakikisha mwili umeliwa ndiyo wanaondoka.
Unajua hata mamba wa mto kama huu wanaweza kuzoea kula nyama za binadamu tu na baadaye inakuwa shida hata watu wanaokaa jirani na mto wa aina hii maisha yao yako hatarini.”
Simulizi kama hizi zilisikika mno katika kipindi cha Nduli Iddi Amini, hilo liliitisha sana jamii ya Watanzania, Iddi Amini alionekana kuwa bedui, haramia na mwanaharamu akilini, moyoni na machoni mwa Mtanzania, hivyo kwenda kupambana naye ilikuwa lazima, lakini ifahamike hata Nduli Iddi Amini Dada alizaliwa na wazazi, baba na mama na ndugu zake kadhaa, kama ilivyo mimi na wewe na alikuwa na nyama na damu kama ilivyo binadamu wengine tu.
Tabia kubwa za binadamu ziko mbili nazo ni wema (utu) wako ubaya(mafirauni). Kwa hakika wanatembea wakiwa wamevaa nguo, kuficha tupu zao lakini mioyo yao ni sawa na MAGENDAEKA.
Tabia za binadamu zinatafautiana, mathalani mnaishi kijijini, mtu mmoja anaweza kuwa mchafu sana, hafui, haogi na hasafishi mazingira ya nyumba yake, lakini huyu ndugu ni mkulima mzuri, nyumbani kwake hakikosekani chakula, sasa kama mnatafuta Mwenyekiti wa Kitongoji ni kweli Kitongoji kinahitaji mchapa kazi ili kiweze kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine, je huyu jamaa mchafu tunaweza kumpa Uenyekiti wa Kitongoji?
Jibu lake ni hili,
“Huyu ndugu ni sawa mchapakazi lakini ule uchafu wake unaweza kusababisha Kitongoji kikapotea kabisa katika ramani ya dunia kwa magonjwa ya tumbo, iwe la kuhara au Kipindupindu, kikapindua Kijiji chote na kijiji kikapachikwa jina Kijiji Kilichopotea Kwa Kipindupindu. Mwanakwetu tambua kuwa kijiji siyo majengo kijiji ni binadamu.”
Natambua msomaji wangu tupo pamoja, twende taratibu na nina hakika msomaji wangu tutaelewana tu, twende kwenye kisa mkasa cha leo. Kuna wakati Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilikuwa na vikao vyake vikubwa vitatu; Kwanza Kikao cha Wakuu Idara(KCWWI) chini ya Uenyekiti wa Mkurugenzi Mtendaji, baadaye ajenda kujadiliwa kwenda Kamati Mipango na Fedha(KMF) na ajenda zote kupelekwa Kwa Baraza la Madiwani kwa uamuzi (BLM).
Ajenda mojawapo ilikuwa ni kuwafukuza kazi kundi la watumishi, kama unavyofahamu wakati huo Manispaa ya Kinondoni ilikuwa pia na hii Ubungo ya leo ambalo lilikuwa dude kubwa. Hapa mashitaka yalikuwa mengi mojawapo aliyekuwa kikaangoni ni jamaa wa Mwanakwetu, jamaa huko benki akiwa na mkopo mkubwa tele nyumba zake zitauzwa , akifukuzwa kazi mambo yataharibika.
Asubuhi ya siku hiyo Mwanakwetu na jamaa yake wakapita Saint Joseph wakasali Misa ya asubuhi kisha Mwanakwetu na jamaa kuelekea Manispaa kusikiliza hali itakuwaje kikaoni?
Meya wa Manispaa hii wakati huo ni huyu Mkurugenzi wa sasa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Yusufu Mwenda kakalia kiti, zikajadiliwa ajenda zote kisha ajenda ya jamaa wa Mwanakwetu na wenzake kufukuzwa kazi. Baraza likageuka kama Kamati kikawa kikao cha siri kisha kurudi tena kama Baraza, kikao cha wazi. Yusufu Mwenda akawaambia madiwani maneno haya,
“Jamani sote hapa ni watu wazima tunakubalina hili, pia tunakubaliana kuwa hawa wenzetu wamefanya makosa na inatakiwa wafukuzwe kazi lakini nawaombeni mtambue kuwa hawa jamaa mpaka wanakuwa watumishi wamepitia hatua nyingi tangu kusoma shule ya msingi, sekondari na hadi vyuo huku kote familia zao zimewekeza na serikali imewekeza, hapa wengine wana familia zenye mume , mke na watoto pamoja na jamaa.
Familia zao hazifahamu kuwa hawa jamaa wamefanya makosa wanategemea jioni ugali uwepo mezani, nawaombeni waheshimiwa mimi si ndiyo Meya wenu, hawa jamaa wote tuwape onyo la mwisho kisha waendelee na kazi.”
Baada ya kauli hiyo na Meya Yusufu Mwenda ambaye nadhani alikuwa Diwani wa Mikocheni, waheshimiwa madiwani wakajadili weee tamati ya yote azimio likalo hilo hilo, wapewe onyo la mwisho.
Mwanakwetu na ndugu yake baada ya azimo hilo wakaingi garini kurudi Mbagala ndugu wa Mwanakwetu akiwa na amani ya Bwana.
“Watumishi wote walirudi kazini wengine waliomba likizo bila malipo na kwenda taasisi binafsi kwa muda ili kusafisha nyota na baadaye wamerudi serikalini.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Makala haya shabaha yake inalengwa kwa wana CCM wote watakaobahatika kuyasoma au kuyasikiliza makala haya, watambue kuwa siyo kila mtu ni kiongozi, Uongozi ni Utu, mwingine anasikia raha wengine wakipata shida, mwingine hata kama mtu akifariki katika mazingira ya utata hashituki.Hashituki kabisa anaona ilimradi mambo yake yanakwenda hana shida, mambo ya jamii wanavyolia hayamuhusu. Wajumbe wa vikao vyoyote vya CCM kuweni makini, kiongozi ambaye hana utu hatufahi tambueni uchaguzi umekaribia, unaweza kuona mambo haya kama hausika lakini yanaweza kumkuta mtu yoyote yule.
Kwa hiyo Uteuzi wa Makamu Mwenyekiti CCM BARA akishakabidhiwa mikoba atambue kilio hichi ili hali ya kuaminiana irudi katika ardhi ya Tanzania, shida za watu wa siojulikana ni kero jambo hili lishughulikiwe.
Kwa hakika msomaji wangu linalosemwa kwa CCM linasemwa hata uwe ACT, Uwe CUF uwe NRA uwe CHADEMA kikubwa kumbuka Uongozi ni Utu na siyo kila anayesimama mbele ni kiongozi Wengine GENDAEKA..
Kwa hakika kisa cha Yusufu Mwenda akiwa Meya wa Kinondoni kitabaki kuwa kisa bora cha mfano kwa makala haya siku ya leo, Mwanakwetu hana hakika tabia za Yusufu Mwenda huko TRA zikoje kama bado ni nzuri basi ni jambo jema, kama zimebadilika Yusufu Mwenda Manispaa ya Kinondoni alikuwa hivyo kama alivyosimuliwa katika makala haya. Ikumbukwe kama jamii inayasimulia mazuri ya Yusufu Mwenda ambaye leo hii ni Mkurugenzi wa TRA hata wabaya mabaya yetu yanasimuliwa vizuri, iwe kwa CCM, iwe ACT iwe CHADEMA dunia haina siri. Kiongozi mkosa utu anapokonywa ridhaa ya wananchi bila ya mwenyewe kujua, watu hawawezi kukuamini, maana hakika ya hatima yao ipo mashakani.
Mwanakwetu Upo?
Je makala haya yaitwe Yusufu Mwenda wa Kinondoni, Uongozi ni Utu au Wengine Gendaheka Mwanakwetu anachagua Wengine ni Magendaeka
Nakutakia siku Njema.
07176492257
Post a Comment