Adeladius Makwega-MBAGALA
Hivi karibuni Mchungaji Dkt. Godfrey Malisa alitoka hadharani na kueleza kwa kina namna alivyofanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa huko Dodoma, katika vikao kadhaa ambapo aliitwa juu ya kile alichokisema kukiukwa kwa Katiba ya CCM.
Mwanakwetu amefuatilia kwa kina maeLezo ya Dkt. Malisa ndani ya ukanda huo wa video wenye dakika 18 na sekunde 21. Ukimalizia na maneno haya;
“Mungu ibarikiTanzania Mungu kibariki Chama cha Mapinduzi.”
Katika maelezo yake Dkt. Malisa yako wazi ya kina, Mwanakwetu anakubaliana naye 100 kwa 100 kwa huo mkiuko wa Katiba ya CCM baada ya kumpitisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais mapema mwaka 2025. Katika jambo hili Dkt. Malisa anaonekana ni mtu makini sana ambaye anaujuzi wa matumizi sahihi ya silaha zake kwa utaratibu, upole, unyenyekevu na uvumilivu mkubwa huku akionekana kuwa muungwana sana mbele ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hata kile kitendo cha kuitikia mwito kwa viongozi wa CCM taifa na hadi kwenda Dodoma mara baada ya kuitwa japokuwa Uanachama wake ulikuwa tayari umepigwa mkasi na Chama Cha Mapinduzi Mkoani Kilimanjaro maana anagekuwa mtu muhuni angesema msinisumbue hangaikeni fupa lenu mlilolianzisha wenyewe… ”
Katika hali ya kutia moyo na mwangaza mpya ndani ya giza totoro la siasa za Tanzania ndani ya chama hiki kikongwe sasa maelezo ya hoja mpya ya Dkt. Malisa yamekuja
“…na hili halisemwi sana na hata katika kikao changu na viongozi wa chama hatukulizungumza(hatukulijadili) kabisa, (CCM) tumevunja katiba ya nchi, tumevunja katiba ya nchi… wale wanaoisoma Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania rejeeni Ibara ya 38 ibara ndogo ya pili A.”
Dkt. Malisa anaonekna ni mtu makini hata matumizi ya sentensi zake, anasema TUMEVUNJA KATIBA YA NCHI… yaani hata yeye mwenyewe anahusika kwa makosa haya ya wakubwawa CCM japokuwa CCM Kilimanjaro imempiga mkasi.
Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba niweka hapa hadharani ibara yote nzima ya 38 na vipengele vyake vyote kama ilivyo ili wewe msomaji wa Mwanakwetu uweze kulifahamu jambo hili kwa kina.
“38.-(1) Rais atachaguliwa na wananchi kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na kwa mujibu wa sheria itakayoweka masharti kuhusu uchaguzi wa Rais ambayo itatungwa na Bunge kwa kufuata masharti ya Katiba Hii (2) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, kiti cha Rais kitakuwa ki wazi, na uchaguzi wa Rais utafanyika au nafasi hiyo itajazwa vinginevyo kwa mujibu wa Katiba hii, kadri itakavyokuwa, kila mara litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:
-(a) baada ya Bunge kuvunjwa;(b) baada ya Rais kujiuzulu bila ya kulivunja Bunge kwanza:(c) baada ya Rais kupoteza sifa za kushika nafasi madaraka ya kuchaguliwa;(d) baada ya Rais kushtakiwa Bungeni kwa mujibu wa Katiba hii, na kuondolewa katika madaraka;(e) baada ya kuthibitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37 ya Katiba hii kwamba Rais hawezi kumudu kazi na shughuli zake;(f) baada ya Rais kufariki.
(3) Kiti cha Rais hakitahesabiwa kuwa kiwazi kwa sababu tu ya Bunge kupitisha hoja ya kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Ili kufahamika zaidi kosa hili lililofanya na Chama cha Mapinduzi naomba nitumie mfano wa michezo maana sisi Watanzania ni hodari sana wa kushabikia michezo japokuwa huko nako tunaboronga, hapa ubaoni mchezo ni mashindano yam bio fupi za mita 100.
“Sheria za mbio za mita 100 kwa kawaida huzingatia usalama, uchezaji wa haki, na kuhakikisha uadilifu mashindanoni. Sheria Kuu ni pamoja na kuanza kutoka kwenye vizuizi kwa mkao maalumu wa kuchuchumaa, kubaki katika njia iliyotengwa, na kutokuzuia washiriki wengine. Mwanariadha atakayeharibu mwanzo atakataliwa moja kwa moja kushiriki mbio hizo na mshindi ni yule wa kwanza ambaye kiwiliwili chake (bila kujumuisha kichwa, mikono, au shingo) kinavuka mstari wa mwisho.
Wanariadha hutumia vizuizi vya kuanzia na kuchukua mkao wa kuchuchumaa, wakisubiri amri ya mwamuzi kutamka maneno kama ‘jiandaye,’ ‘kaa tayari’ hutamkwa hadharani washindani na mashabiki wakisikia.
Ikiwa mwanariadha ataanza kabla ya ishara ya kuanza, ni mwanzo wa uongo. Mwanzo mmoja wa uongo unasababisha kufungiwa kabisa. Wanariadha wanapaswa kubaki katika njia zao maalum kwa muda wote wa mbio na hawaruhusiwi kuzuia au kuwazuia washiriki wengine. Kumzuia kwa makusudi mwanariadha mwingine kunaweza kusababisha kufungiwa moja kwa moja.
Mshindi ni mwanariadha wa kwanza ambaye kiwiliwili chake – bila kujumuisha kichwa, mikono au shingo kinavuka mstari wa mwisho. Ikiwa ni vigumu kubaini mshindi, picha maalum hutumika kuchanganua wakati halisi ambao kila mwanariadha alivuka mstari. Wanariadha hawapaswi kushiriki katika vitendo visivyo vya kiungwana au utovu wa nidhamu. Wanariadha wanapaswa kuwa waangalifu kuhusu mazingira yao na wanariadha wengine walioko kwenye uwanja wa mbio.”
Haya ni ya michezo michezoni na sasa turudi katika ulingo wa siasa.
Kwa hakika maelezo haya yote yanakuja kwa kuwa Dkt. Malisa kada wa CCM ambaye amepokwa uanachama wake anao uelewa mkubwa wa chama chake na ameongea. uhalisia wa mambo, wakubwa wamekosa lakini mazoea wakubwa hawakosei. Hali hii inaibua mengi kuwa hata stahiki anazopata mtu aliyekuwa anashika nafasi hiyo mara baada ya Bunge kuvunjwa zinatakiwa zisitolewa tena, kabisa kwake hadi hapo kama atakaposhinda nafasi hii, kama atakapotangazwa mshindi na kama ataapishwa, kwa sababu ziko hoja kuwa pengin kinachoonekana siyo kama kilichoandikwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo ho nao ni mkiuko wa Katiba.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza vizuri na kwa kina kuwa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa wazi kama mambo sita yatatokea;
“baada ya Bunge kuvunjwa; baada ya Rais kujiuzulu bila ya kulivunja Bunge kwanza; baada ya Rais kupoteza sifa za kushika nafasi madaraka ya kuchaguliwa; baada ya Rais kushtakiwa Bungeni kwa mujibu wa Katiba hii, na kuondolewa katika madaraka; baada ya kuthibitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37 ya Katiba hii kwamba Rais hawezi kumudu kazi na shughuli zake; baada ya Rais kufariki.”
Katika maelezo yake Dkt. Godfrey Malisa ndani ya ukanda huu unaweza kudhani kana kwambba anazungumza kwa kinyonge sana huku akitoa ilani kuwa kama hali hii itaendelea na hakutakuwa na hali ya kulitatua tatizo hili yeye atakwenda mahakamani ili mahakama ifanya tafsiri ya ibara hii ya 38.
Kwa watu makini wanaofahamu siasa Mchungaji Dkt. Godfrey Malisa anapaswa kuwa mshauri wa rais wa masuala ya siasa, sheria Katiba maana mshauri mzuri ni yule anayeiona kesho kabla wengine hamjaiona.
Kwa kuwa kama Tanzania iliweza kumchagua Rais mpya mwaka 2021 baada ya Rais Magufuli kufariki ambapo ni kipengele cha mwisho katika ibara hii, kwa hiyo nafasi ya Urais inakuwa wazi pale ambapo Bunge limevunjwa na kama tuliheshimu kipengele cha sita basi na tuheshimu kipengele cha kwanza.
Hoja kubwa hapa ni hii mchakato wa kumtafuta Rais Mpya kama ungefanya na mtu mwingine kwa siri, mapema Januari 2025 maana yake tungekuwa tunayasema mengine sasa nap engine safari za mahakamani zikimuhusu.
Kwa hiyo kumtangaza mgombea urais mapema mwaka 2025 CCM ilimekosea na lazima jambo hili lirekebishwe mapema, maana yake CCM inaonekana kuwa kwa mwaka 2025 imeanza kufanya kampeni yake mapema kabla ya wakati sahihi huku vyama vingine havijafanya hivyo na CCM kilitakiwa kuwa chama cha kupigiwa mfano. Kufanya harakati hizo mapema ni sawa na zile habari za mbio za mita 100 maana anaweza kushinda na ndiyo maana katika riadhaa anapigwa kadi nyekundu na kadi hiyo nyekundu haikuhitaji mjadala wa mashabiki ilikuwa mara moja baada ya maamuzi yale.
Mwanakwetu anakiomba Chama Cha Mapinduzi kizingatie hili na kinyume chake ni kukiweka rehani chama hiki kikongwe maana hakuna kadi nyekundu inayosubiri mjadala wa mashabiki.
Mwanakwetu Upo? Kumbuka,
“KADI NYEKUNDU INAYOSUBIRI MJADALA WA MASHABIKI.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257

Post a Comment