MAANDAMANO MENGINE

 


Adeladius Makwega-Musoma MARA

“Nimekwenda Halmashauri kupitishiwa barua yangu, sasa leo nakwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa kuchukua barua, naangalia barua hii badala yakupitishwa imeandikwa barua hii iingizwe katika mfumo wa maombi ya uhamisho wa elektroniki.

Nikajiuliza swali huyu mkubwa hakufahamu kwanini barua hii ilikwenda kwake ikiwa nakala ngumu? Inakuwaje wenzako wote katika nafasi nne wamepitisha barua hii ikiwa nakala ngumu?

Makwega!

Hata wa kumuuliza hilo sikumuona na ndiyo maana nakupigia simu nifanyeje?”

Haya ni majira ya asubuhi, Mwanakwetu yu katika Mji wa Musoma, gafla anasikia simu yake ya mkononi inaita na kuelezwa jambo hilo kama lilivyo.

Mwanakwetu akatoa ahadi ya kumuagiza ndugu huyu akamuone mheshimiwa mmoja na yeye ambatane naye ili kumpata mhusika angalau barua hiyo ipitishwe ikiwa na nakala ngumu, maana mijadala ya Nakala Ngumu na Nakala Tepe hayana maana kwa mtu anayekwenda Manispaa anataka huduma katika ofisi ya umma na siyo vinginevyo.

Siku iliyotangulia Mwanakwetu aliandika makala juu ya Akiunyea Mkono Msiukate kwa hiyo mawasiliano na mama huyu yalimkumbusha Mwanakwetu kutaka kujua juu ya binti jirani na mama huyu ambaye ana nasaba naye, aliyepata ujauzito mwaka 2022 na hakufanya mitihani wa kidato cha nne na mwaka huo huo ulipotolewa Mwangozo wa Kuwarejesha Shuleni Wanafunzi Waliokatiza Masomo Katika Elimu ya Msingi na Sekondari kwa Sababu Mbalimbali, binti mwenye nasabu na huyu mama alikuwa mmojawapo wa wanufahika hawa ni ndugu wa Mwanakwetu.


 

Mwanakwetu aliuliza binti yetu anaendeleje na masomo?Mama huyu alijibu kwa hasira;

“Hataki kusoma, yupo nyumbani na mtoto wake na mimi sitaki hata kuyauliza haya mambo .”

Mjadala huu ulijengwa na kisa hicho, huku pande zote mbili za mazungumzo haya zilianza kulitazama jambo hili kwa kina. Hoja ya kwanza ya mazungumzo haya ilijengwa juu ya wanafunzi waliopata ujauzito kwa nini wasisomeshe bure katika vyuo vya Ufundi vya FDC na VETA ambavyo sasa vimeanza kutapakaa nchi nzima?

Kwa maeneo ya mijini watoto hawa waliopata ujauzito wanaweza kupewa nafasi kusoma FDC/VETA bure huku Halmashauri husika kwa kuwapatia fedha za mapato ya ndani ziwapatie pesa na nauli ya kwenda na kurudi chuoni kila mwezi na vyuo vya FDC /VETA vya bweni vingewasaidia mabinti hawa hata wasionane tena na wale wanaume waliowapa ujauzito.

“Ni kweli sasa hivi FDC/VETA vyuo vipo vingi na hata huyu binti tulitaka kumpeleka huko akasome, lakini hapa Makwega hakuna msomaji. Hata hizo shule zenyewe za mabinti waliopata ujauzito zipo wapi? Hapa Mbagala ambayo huyu binti alikuwa anasoma ilikuwepo moja tu huku Mbagala Chamazi. Shule zenyewe hazipo, Shule zenyewe ni tatizo.

Shule hizo zilitakiwa kusimamiwa na TRC(Vituo vya mafunzo) Shule hizo hazipo, je hawa mabinti wanasoma wapi? Mwanafunzi anakwenda anakuta mazingira hayaeleweki anakacha.

Labda jambo hili lilitakiwa kuondoa siasa na kuanza kuwekeza fedha katika hili na pia kutumia nguvu ili mabinti wetu waliopata ujauzito wachague moja kati ya haya kurudi kusoma what is Biology? au  Kutosma FDC/ VETA.”

Mwanakwetu katika mazungumzo haya anakukumbusha msomaji wake kuwa wanawasiliana kidugu na mama huyu na hili nakujulisha msomaji wangu kutokana na umuhimu wa mabinti waliopata ujauzito kuendelea masomo bila masharti maana Mwanakwetu ni mzazi ana mabinti wakubwa, huku binti yaagu mkubwa ana umri wa miaka 25 na kwa hakika naungama hadharani mabinti wote wa Watanzania wanaopata ujauzito shuleni iwe msingi au sekondari ni mabinti zangu.


 

Mazungumzo na ndugu yanaendelea na tukiwa tunatoka kijiji kimoja cha Mbagala na kusoma wote. Mwanakwetu akamwambia huyu mama;

“Hivi kama tusingekuwa tumesoma wote shule ya msingi na baadaye sekondari na hata kama tusingekuwa tunakaa wote Mbagala, utaratibu ungekuwa kama ule wa zamani kila mmoja anakaa katika chaka/ msitu wa koo lao , hivi tungefahamiana kweli?”

Mama huyu akasema utaratibu wa maisha ya Watanganyika kila mmoja wakati huo alikuwa anakaa katika chaka lake, hakukuwa na dhana hii ya vijiji, kata, tarafa , wilaya au mkoa, kila mtu alikuwa kivyake na luwake. Dhana ya Vijiji vya Ujamaa ilijengwa kwa shuruti huku akina Rashidi Mfaume Kawawa walilalamikiwa na kubebeshwa mizigo ya lawama kwa kuwatoa Watanganyika hao katika machaka/ misitu yao hadi katika Vijiji vya Ujamaa ili Watanganyika wapate huduma za kijamii kama vile tiba na shule , ndiyo kusema hata hili la wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni ni chaka ambalo viongozi waache kufunga sala wasione mambo ni safi, hapana lazima wafanye ushinikizaji wa kuendelea na masomo KWA LAZIMA kila aliyepata ujauzito na halipaswi kuachwa hivi hivi kwa kufanya siasa waliopata ujauzito kujiamulia watakavyo.


 

Mwanakwetu akasema, Tanzania inahitaji baada 20 ijayo tumpate Waziri Mwanamke ambaye alipata ujauzito Shuleni na akanufahika na huu mwongozo na kupata elimu hadi ngazi ya juu ili aje kuwasaidia Watanzania wenzake wenye changamoto hizo. Mjadala huu mkubwa uliibua kisa hiki;

“Mwaka jana mwezi wa 10-11 binti mmoja kidato cha kwanza kapata ujauzito, mama mtu kamleta mtoto pale shuleni. Mama mbele, mtoto katikati na mjumbe nyuma yao, hili la mkoani Morogoro.

Mjumbe mwanamke kaambatana nao, kwa hoja kuwa usalama wa mama huyu ulikuwa hatarini, Mkuu wa Shule akatuita, binti mjamzito wa kidato cha kwanza akaandika maelezo, zoezi hili likiendelea, mama huyu alizimia.

Haya mbebeni mumpeleke hospitalini mkuu wa shule anasema, mama mwenyewe ana mwili mkubwa, Mungu bahati baada ya muda alizinduka na alipotoa maelezo alieleza hali yake ya usalama ipo hatarini kutokana ujauzito wa huyu bintiye, mumewe kasema anamuacha kisa huu ujauzito.

Mama huyu alihakikishiwa kuwa mtoto huyu ataendelea na masomo, kwanza akajifungue. Sina hakika kama binti huyu atarudi kuendelea na masomo.

Binti huyu hawezi kurudi shuleni, ni ngumu labda kungekuwa na shinikizo la watoto wote waliopata ujauzito, iwe lazima iwe lazima warudi shuleni kwa kutumia hata polisi.

Sasa hivi polisi wetu tunawatumia sana kwenye kuukimbiza Mwenge, kuzuia maandamano lakini je Watanzania hivi sasa tunafahamu kuwa suala la ujauzito shule ni Mwenge mwingine? Ujauzito shuleni ni maandamano mengine ambayo madhara yake yatakuja kulikumba taifa hili hivi punde? Vyombo vya ulinzi na usalama vitumike kupambana na waliopata ujauzito na kurejeswa mashuleni, tukiishirikisha TAMISEMI, WIZARA YA ELIMU na WIZARA YA JINSIA na huku sheria ndogo ndogo zikitungwa.


 

Simu hii ya ndugu wa Mwanakwetu ilikata, hapo hapo Mwanakwetu akabeba begi lake kuelekea kazini, akiwa njiani akarejea nakala ya Mwongozo wa Kuwarejesha Shuleni Wanafunzi Waliokatiza Masomo Katika Elimu ya Msingi na Sekondarri kwa Sababu Mbalimbali hasa ibara yake ya 1.0 kukiwa na maelezo haya,

“…utoaji wa elimu kwa wote bila ubaguzi. Katika Mukutadha huo. Dira ya Elimu inalenga kuwa na Mtanzania aliyeeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mtazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa…”

Mwanakwetu anasema nini?

Hoja ya msingi kwa leo ni kuwa kila Mtanzania anahitajika katika kuchangia nguvu kazi kwa kipawa chake  kama alivyojaliwa na Mungu na Kusoma katika kuleta maendeleo ya taifa, kwa hiyo utoaji wa elimu kwa mabinti waliopata ujauzito lazima, lazima utolewe na viongozi wetu jukumu lao ni kulitilia mkazo hilo kwa kushirikisha taasisi zote na tuache siasa, kwa hakika ni aibu ati tukisema oooohhh….

“Tunatilia mkazo hili ati kwa sababu taifa letu limesaini mikataba ya kimataifa, eboo, shabashi

Hao wenye mikataba ya kimataifa ndiyo watoto huku Mbagala? Hao ndiyo wanaowatia ujauzito binti zetu? Hao ndiyo wanaowazaa hao mabinti? Hoja ni mimi, wewe, yule na wewe kiongozi unayetuongoza ni wetu sisi, sote tupambane ili tuweze kufichiana hizi aibu zetu za mimba za utotoni nchini Tanzania.”

Makala haya yametayarishwa kwa heshima zote na Mwanakwetu kwa kuheshimu ibara ya 5.15 ii cha Mwongozo wa Kuwarejesha Shuleni Wanafunzi Waliokatiza Masomo Katika Elimu ya Msingi na Sekondari Kwa Sababu Mbalimbali, kipengele hicho kinachosema hivi;

“Wajibu wa jamii ni kubadilishana uzoefu na elimu kuhusu ulinzi wa watoto dhidi ya mimba na ndoa za utotoni, matumizi ya madawa ya kulevya, ajira za utotoni pamoja na madhara yatokanyo na vitendo hivyo…”

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“HAYA NI MAANDAMANO MENGINE.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

NB -Makala haya yameandikwa kwa heshima zote kwa marehemu mwanahabari BI Leila Sheikh ambaye akiwa hai mwka 2006 aliwahi kumtafuta Mwanakwetu ili ajiunge na TAMWA, wanahabari wa mkoani Iringa wakamjibu kuwa Adeladius Francis Makwega yupo Iringa , ni mdau wa habari za akina mama lakini ni mwanaume huwa ni mdau  tu wa makala za ukombozi wa Mwanamke, maana wanawake ndiyo waliyomzaa.


BI Leila Sheikh enzi za uhai wake.




 

 

0/Post a Comment/Comments