TABIA ISADIFU NAFASI UTAKAYOAMINIWA

 


Adeladius Makwega-MSAMVU-MOROGORO

“Mnakaa Dar es Salaam, mkumbuke na kwenda kuwasalimia Babu na Bibi zenu Manyoni Singida, najua kweli hapa Dar es Salaam wako ndugu zenu upande wa Baba lakini mkumbuke na kwetu.”

Haya yalikuwa maneno ya Mama wa Mwanakwetu Mwalimu Dorith Mlemeta wakati wa Krisimasi ya Mwaka 1995. Mama huyu wa alimwambia kijana wake maneno haya na wakati huo Mwanakwetu alikuwa amemaliza Kidato cha Nne anasubiri matokeo yake.

Mwanakwetu anakumbuka wakati huo alikuwa anafanya kazi Bandarini kama mpagazi, wakati  huo Bandari ya Dar es Salaam kulikuwa na meli kutoka Uingereza ilikuwa na jukumu la kuchukua sukari. Kazi yao ilikuwa ni kuikata ile mifuko yenye sukari kutoka Morogoro alafu akina Mwanakwetu wanaisambaza katika magenge ya meli hii ya Uingereza. Huku bandarini wakisema kuwa kila mwaka meli hiyo huwa inakuja kubeba mzigo mkubwa wa sukari. Kwa hakika Mwanakwetu alikuwa na vijisent vya kuweza kusafiri atakapo na ndiyo mama mama yake mzazi akampa huo ujumbe.


 

Siku chake kabla ya Noeli Mama wa Mwanakwetu na wanawe kadhaa alisafiri nao hadi Kilimantinde Manyoni Singida ambapo Babu wa Mwanakwetu Reverent Hezron Mlemeta alikuwa akihudumu kama Kanoni na Chaplini katika Chuo cha Uuguzi Kilimantinde kinachomilikiwa na Kanisa la Angilikana la Tanzania. Akiwa hapo Mwanakwetu alijenga ujirani na mabinti wengi wanachuo wauguzi, wauguzi kamili madaktari wa mazoezi na madaktari kamili.Mwanakwetu akakaa pale hadi matokeo ya kidato cha nne yalipotoka kasha akarudi zake Dar es Salaam kuendelea na masomo.

Ukapita mwaka 1996, ukaja 1997 na baadaye 1998, mwaka huu 1998 Mwanakwetu akahitimu kidato cha sita. Siku moja akiwa Mtoni Relini akakutana jamaa mmoja na begi lake mgongoni, wakasalimiana naye, jamaa akasema kwema? Mwanakwetu akajibu kwema. Jamaa akauliza unanikumbuka ? Mwanakwetu akajibu,

“Ehhe wewe ni daktari tulikutana Chuo cha Uuguzi Kilimatinde.”

Jamaa akajibu ndiyo na wewe ni yule mtoto wa mchungaji?

Mwanakwetu akajibu yule mchungaji ni Babu yangu mzaa mama, jamaa akasema umefanana naye sana. Jamaa huyu Daktari akasema nimeshahitimu chuo kikuu sasa hivi ninakwenda zangu huko bondeni kumuona jamaa mmoja, jamaa akaaga na naye Mwanakwetu kuendelea na maisha yake.

Miaka kumi na miwili baadaye yaani mwaka 2010 Mwanakwetu alishiriki uchaguzi wa Kura za Maoni CCM Jimbo la Kigamboni ambalo lilikuwa sehemu ya Mbagala, kura hizo za maoni zilikuwa nawagombea wengi na malalamiko mengi, huku ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi na vitendo vya rushwa vilikuwa wazi wazi mithili ya kwamba Tanzania haikuwa na chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa. Jambo hili lilikuwa kero kubwa kwa wagombea vijana akiwamo Thadeus Musembi na Kazimbaya Makwega.


 

Malalamiko yalipozidi ilibidi Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam Kilumbi Ngenda afike wilayani Temeke na kufanya mazungumzo na wagombea wa kura za maoni kwa majimbo  yote mawili ya Wilaya ya Temeke wakati huo yaani Jimbo Kigamboni na Jimbo la Temeke. Wagombea wa Jimbo la Temeke ambao Mwanakwetu anawakumbuka ni Chikago Matelefoni , marehemu Richard HIzza Tambwe na nadhani huyu Abbasi Mtemvu.

Kilumbi Ngenda Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu wa CCM mzoefu akasema nataka leo mseme kila kitu, maana bila nyinyi hakuna CCM kama kila mmoja wenu akachukua fito yake na kutokomea nayo, wapinzani hatuwezi kupambana nao CCM inasema UMOJA NI USHINDI, ili kuondokana na hili na CCM kufanya vizuri leo mseme kila kitu.

Msomaji wangu kumbuka hapo kura zimeshapigwa washindi wa Jimbo la Kigamboni na Temeke wanajulikana. Thadeus Musembi, John Kibaso kuna jamaa mmoja alikuwa anaitwa Kiboko,pia alikuwapo mama mmoja alikuwa anaitwa Mwalimu Ingawaje na Richard Hiza Tambwe walisema maneno makali mno kwa ushahidi wa vitendo vya rushwa wakati wa kura za maoni majimbo yote mawili.

Katibu Kilumbi Ngenda ana hekima sana akasema jamani kuna watu mbona hawaongei na ninawajua huwa ni waongeaji wazuri? Mimi nitawalazmisha wasema.

“Kazimbaya Makwega ni kijana wangu, nimemlea mwenyewe, alikuwa Katibu Mwenezi mzuri sana alipokuwa Chuo Kikuu, Makwega katika kura maoni naona amepata kura 246, mwenezi wangu mbona upo kimya ? Sisi hatutaki watu waondoke na fito, nyumba itaanguka, Makwega mbona hausemi kitu? “

Wagombea wanacheka wakisema Makwega kumbe hadi Katibu wa CCM Mkoa anamtambua? Katibu Mkoa akajibu sana kijana wangu. Haya Makwega tuambie.


 

Kumbuka msomaji wnagu ule ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi za CCM zilikikukwa mno, Makwega alikata tamaa sana. Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam akasisitiza Makwega aongee.

“Ndugu Kilumbi Ngenda, mimi nashukuru sana kwa kunipa wasaa huu, mimi ndiyo nimemaliza Chuo Kikuu kuja kufanya siasa, sasa ninakutana mambo ya aibu, tofauti kabisa na nilichokuwa ninakiota, inakatisha tamaa. Kwa bahati nzuri mimi namfahamu Masoud Ali Masoud (Bedui) aliyekuwa mbunge Temeke zamani ambaye ndiye Mkongwe kuliko wote hapa kikaoni. Katibu kabla ya kikao hichi imenibidi nimuuliza Mzee Ali Masoud, ‘ Hivi haya ndiyo mambo ya CCM tangu Ujamaa?’ Mzee Ali Masoud yupo hapa ni mgombea Mwenzetu akasema zamani hali haikuwa hivi ya sasa hii ni kufuru maana zamanai ukitoa mipesa yako utaeleza ulipoitoa.

Katibu sikuishia hapo nikamuuliza Mwichumu Abdul-rahaman Msomi ambaye ndiye mbunge anayeondoka, akajibu kuwa hali kama hii ilionekana mwaka 2005 lakini CCM Taifa iliingilia kati baada ya Yusuf Manji kumwaga fedha.

Katibu Mkoa kwanini CCM Taifa inaingilia kati baada ya matokeo, inatakiwa CCM Taifa iingilie kati haya mambo mapema. Kwa hakika yanakatisha tamaa na ipo siku watu wataondoka na fito zao, mchana kweupe. Ndiyo mwenzetu Dkt Faustine Ndungulile kashinda uchaguzi huu kwa kura tele lakini mgombea anafika katika kata ambayo mimi ni kwetu anawagawia fedha makundi makundi ya watu, kweli Katibu unatarajia huyu aliyeshinda kwa rushwa akiwa Waziri mimi nitamuheshimu?Au mwingine alishuhudia haya atamuheshimu?

Kwa hakika mimi nitamdhalau na hata nikimdhalau na hilo litakuwa la haki yake na hiyo ndiyo haki yake. Katibu Mkoa hapa Thadues Musembi amesema siyo kwamba tunamchukia Dkt Ndungulile la hasha.

Mimi binafsi  niseme hapa hadharani naweza kuwa ni miongoni mwa watu ninaomfahamu ndungu Ndungulile tangu akiwa daktari tarajiwa nilimuona kule Chuo ch Uuguzi Kilimatinde mwaka 1995/ 1996 na namna alivyokuwa akiishi na kufanya kazi na wauguzi katika chuo na Hospitali ile, jamani tunahitaji ushindi wa halali na hapo tutampa mtu heshima yake.”

Baada ya kikao hicho Katibu wa CCM mkoa aliandaa kikao cha pili ambapo wagombea wote wa kura za maoni CCM Dar es Salaam waliitwa kikaoni Wilayani ilala wakiwamo akina Shy Rose Bhanji , Musa Zungu , Iddi Azan na wengine wengi ambapo Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa John Guninita Mkiti CCM Mkoa wa Dar es Salaam ambaye sasa ni marehemu na hapa yalizungumza mengi.


 

Mwisho wa siku Uchaguzi mkuu ulifanyika na Jimbo La Kigamboni akashinda Dkt Faustine Ndungulile baadaye Jimbo la Mbagala kuundwa na kutenganishwa na Kigamboni, miaka ikasonga hadi Dkt Ndungulile akawa Naibu Waziri wa Afya baadaye akawa Waziri wa Mawasiliano .

Kwa hakika Mwanakwetu kila alipokutana na Dkt Ndungulile akiwa hana watu wengi, yeye mwenyeweDkt Ndungulile anasema Kazimbaya kwema? Mwanakwetu anajibu kwema kaka? Hapo hapo Mwanakwetu alikuwa anamwambia Dkt Ndungulile jamani badilikeni, mkibadilika nyinyi na hili taifa litabadilika, hata muwe na vyeo vikubwa namna gani jamani lazima mbadilikeni.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Jamani eee mbadilike, mara baada kuona taarifa ya kifo cha Dkt Faustine Ndungulile hayo yote yaliyoandikwa juu yalikuja akilini mwa Mwanakwetu alikumbuka hayo yote akaamua kuyatayarisha makala haya.

Kikubwa wenye nafasi wanahitajika mno kuibadilisha hii nchi yetu.Kwanza kabisa viongozi wetu wabadilishe mienendo yao, wengine wataiga, kufanya hivyo kunaweza kulisaidia taifa hili lakini kinyume chake ni msiba.

Kwa sasa baadhi ya Watanzania wanaaminiwa katika nafasi kubwa kimatifa, lakini je hao wanaominiwa ikifika nyakati za kura za maoni CCM tabia zao zinasadifu ukubwa wanaominiwa au ukubwa watakaoaminiwa hapo baadaye?

“Inaweza kuibuka hoja kuwa watu wanavunjiwa heshima lakini kumbe watu wanajivunjia heshima wao wenyewe.”

Mwanakwetu anasema kwa kunong’ona katika masikio ya kila kiongozi kwa kutumia mbiu yake ya mgambo ya makala haya, Jamani Mbadilike Dkt Faustine Ndungulile ni jamaa wa Mwanakwetu, yeye ametumika kama kioo cha kila kiongozi kujitazama namna anavyofanya siasa za Tanzania.Hawa watoto wa Chipukizi tukiondoka watatuzamaje?Tunawaachia kipi cha kujifunza?


 

Jamani ngoja nimeze mate.

Kumbuka,

“TABIA ISADIFU UKUBWA  UNAOAMINIWA.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 

0/Post a Comment/Comments