Adeladius Makwega-MWANZA
Wakristo wameambiwa kuwa katika dominika ya nne ya Pasaka inawataka kuwa jasiri kama walivyokuwa mtume wa Yesu na kusimama mbele baada ya ufufuko wa Yesu alipoutoa uhai wake kwa ajili ya kundi lake, hivyo kila mmoja awe mchungaji mwema katika familia na jamii yake.
“Kristo ni mchungaji mwema, yu tayari kutuongoza, yu tayari kutuelekeza, maana yeye siyo mchungaji wa mshahara.”
Hayo yamesemwa na Padri Samson Masanja, Paroko wa Parokia ya Malya katika Kanisa la Bikira Maria-Malikia wa Wamisionari, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza katika misa ya kwanza ya dominika hii iliyoanza saa 12 asubuhi na kumaliza saa moja ya asubuhi.
Padri Masaja alisema,
“Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo umekuwa chanzo cha mabadiliko mengi duniani, sisi tulio wafuasi wake tunaoungama ufufuko wake, sote tunapokea uzima na uponyaji katika jina la Yesu na sio dhambi, sio uovu, sasa havina nguvu tena, je mimi na wewe tunalitamka vipi jina la Yesu?”
Padri Masanja alisema kuwa baada ya ufufuko wa Yesu, Petro alikuwa mtu mwingine, siyo yule aliyemkana Yesu Mkristo, huku akihubiri habari za Yesu Kristo kifua mbele baada ya kujawa na Roho Mtakatifu , hilo liwe pia kwa kila muamini.
Misa hiyo pia iliambatana na nia na maombi kadhaa
“Eee Mungu mwenyezi, mchungaji mwema alitoa maisha yake ili kutupa sisi uzima, Utusaidie kuthamini uhai tuliojaliwa kwa neema yako. Eee Bwana-Twakuomba Utusikie.”
Wakati misa hii inaanza umeme ulikatika gafla saa 12 na dakika 9 ambapo Somo la Kwanza, Shangilio na Somo la Pili yalisomwa huku kukiwa giza tele kwa kutumia tochi ya simu ,nalo kanisa nzima likiwa na vyanzo sita tu vya mwanga ambayo ilikuwa Mshumaa wa Pasaka, mishuma miwili ya altare, mshumaa mmoja wa tabelenakulo na tochi ya mministranti ambayo alitumia kummulikia msomaji wa masomo hayo na tochimoja ya muumini nyuma kanisani.
Baada ya dakika 11 yaani saa 12 na dakika 20 umeme ulirudi na mwanga kuongezeka ambapo taa tisa za balbu ziliongeza mwanga na spika za kanisa hili kufanya kazi tena
Balbu hizo tisa, tatu zilikuwa mkono wa kulia kama unaingia kanisani kupitia langu kuu, nne katikati ya kanisa na balbu mbili mkono wa shoto wa kanisa hili.
Kwa ujumla hali ya hewa ya Malya na viunga vyake kwa juma zima ilikuwa ya jua la kadili, mawingu kiasi nayo ardhi ya eneo hili ikiwa na siafu wengi huku wakulima wa mpunga wakiendelea kuvuna masuke ya mipunga yao mashambani.



Post a Comment