AdeladiusMakwega-MWANZA
Juni 22, 2022 ambapo sasa ni karibu mwaka mmoj a na miezi 5 tangu Mwanakwetu alipoandika makala haya.
...............................................................................................................................................................
Mwaka 2012 Chama Cha Mapinduzi(CCM) kilifanya uchaguzi wake tangu ngazi
ya mashina hadi Taifa. Katika kata ya wilaya mojawapo ya Tanzania Bara zoezi
hilo lilifanyika kukipa uhai chama hiki tawala nchini Tanzania vizuri sana
Kulikuwa na wagombea wawili akiwamo ndugu mmoja, akajaza fomu vizuri na
kuzirejesha ili kusubiri majina kurudi kutoka ngazi za juu, bahati nzuri jina
la ndugu huyu na wagombea wengine yalirudishwa na siku ya uchaguzi kupigiwa
kura.
Wapiga kura walimchagua kwa kishindo kikubwa ndugu yangu huyu, Mara
baada ya kura yeye na wenzake waliwashukuru wapiga kura kwa maamuzi hayo.
Akilini mwake aliyeshinda alijiuliza kwa nini ameshinda kwa kura nyingi? Jibu
hakupata lakini akaendelea kufanya utafiti wa ushindi wake huo wa kishindo.
Mwenyekiti wa Kata na Katibu Kata wakakaa chemba kuyajenga mambo yao,
Katibu Kata akamwambia Mwenyekiti hapa tumeshinda, hivi vyeo ni vya watu,
tutende haki, mimi mambo ya konakona siyawezi, nimeacha mashamba na ng’ombe
zangu kuja kufanya kazi ya watu tu.
Mwenyekiti alikuwa mzee aliyeridhika, hana tamaa tamaa, japokuwa alikuwa
na maisha ya kawaida mno.
‘Mie mwanangu, muda huu duniani ni kitu gani ambacho sikifahamu?
Ninachokitafuta ni nini zaidi ya haki. Sitaki kufa mufilisi, tutafanya kazi kwa
haki.’
Alisema Mwenyekiti wa CCM wa Kata hii.
Walianza kazi na kwanza kabisa walitembelea matawi yao yote moja baada
ya lengine kwa kutumia baiskeli, bodaboda na kwa miguu. Katika kutembelea
matawi ya wadi hii walikutana na matawi yasiyo na miradi na matawi yenye miradi
midogo na miradi mikubwa zaidi.
Katibu Kata akamwambia Mwenyekiti wake kuwa,
‘Chama siyo miradi, chama ni watu wale wanaokiunga mkono, miradi
inafuata baada ya uugwaji mkono. Siasa ni uungwaji mkono na watu, watu ndiyo
wanaopiga kura si miradi. Lazima kuwekeza kwa mtu mmoja mmoja.’
Miradi ya maegeso ya magari ilikuwa mitatu, sehemu za kuosha magari
zilikuwa nne na maduka kadhaa katika ofisi za CCM kwenye matawi hayo yaliyojaa
wapangaji yalikuwa mengi.
Msimamo wa Mwenyekiti na Katibu Kata unatakiwa kufikishwa kwa wajumbe wa
vikao vitatu vya kata maana kikao cha Mkutano Mkuu wa Kata ndiyo uliomchagua
Mwenyekiti kilishafanyika. Kwanza ni Halmashauri Kuu ya CCM ya Kata yenyewe
inawajibu mkubwa wa kujenga Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Pili
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Kata hii ndiyo inayotoa alama kwa
wale wanaogombea Uenyekiti, ujumbe na hata nafasi mbalimbali na alama zao
kwenda Wilayani kwa maamuzi. Mwisho ni Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Kata
hii mwenyekiti wake huwa ni Katibu Kata (Kikao cha Watendaji wa Chama).
Mwenyekiti wa CCM wa Kata alitoa dozi ya msimamo wake vizuri sana na
mwisho Katibu Kata akaitisha kikao chake cha sekretarieti kumaliza fitna.
Kukiwa na wajumbe wafuatao Katibu wa Itikadi na Uenezi na Katibu wote jumuiya
za CCM za kata.
Wakati vikao hivyo vinaendelea kata hiyo ilipatiwa shilingi 800,000/
kama mgao wake zikaingia na maelekezo ya Katibu wa CCM wa Wilaya pesa hizo
ziende katika matawi ili kuboresha uendeshaji wa chama hiki tawala.
Katibu Kata alipokuwa akizungumza na sekretarieti yake wale wajumbe wa
zamani hawakuridhishwa na msimamo huo. Katibu akawaelekeza huo ndiyo msimamo na
imeingia laki 8 inapelekwa matawini. Wajumbe wa zamani walipinga waziwazi
ajenda hiyo yenye maelekezo wakitaka pesa hizo wagawane sekretarieti tu, mbona zamani
walikuwa wakifanya hivyo?
Ajenda hii haikumalizika ikawekwa kiporo bila azimio.
Huyu Katibu Kata akashituka kuwa hawa jamaa wamemchagua kwa kura nyingi
ili mambo yao yaende sasa anayakwamishwa na yeye wanamkwamisha anafanyaje?
Alipotoka kikaoni akamshirikisha Mwenyekiti Kata akamuagiza ampigie simu
kumueleza changamoto hizo Katibu wa CCM wa Wilaya.
Katibu wa CCM wa Wilaya aliyekuwa muungwana na mzalendo alimpa mbinu
Katibu Kata huyu.
Kikaitishwa kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Kata jumamosi
moja saa tano asubuhi wajumbe wakaingia mjadala ukaanza.
‘Mbona Katibu Kata mwenzako alikuwa anaenda kuchukua fedha kwa matajiri,
kila kikao tunakula chakula na tunapatiwa posho, wewe unayafanya mambo yanakuwa
magumu sana.’
Katibu Kata akawajibu kuwa huyu tajiri ndiyo ni mpangaji wetu, kapanga
katika maduka yetu karibu yote, tukichukua pesa yake lazima turudishe au
atukate katika kodi ambapo mgao wetu bado hatujagawiwa.
‘Wewe ndiyo haufai unakiharibu chama chetu.’
Wajumbe wa Sekretarieti walilalamika. Katibu Kata akawaambia, hiki chama
chetu siyo chama ombaomba na hisani, hiki ni chama cha Ujamaa na Kujitegemea,
chama cha mapinduzi hata ya kimawazo.
Wakati mjadala umekuwa mkali, ikasikika honi gari nje ya ofisi ya CCM ya
kata.
‘Piiiii…Piiiiiii...Piiiii…’
Kwa bahati nzuri viongozi wa vijana walikuwa nje wakampokea wakampeleka
alipo Katibu wa CCM wa Kata kikaoni.
‘Hodi jamaniii …!Kidumu Chama cha Mapinduziii… !’
Mgeni alisalimia.
‘Kidumuuu…’
Wajumbe wa kikao walijibu.
Ndugu mgeni hawa unaowaona mbele yako ni wajumbe wa Sekretarieti ya
Wadi. Wakajitambulisha majina na vyeo vyao, naye Katibu Kata ambaye ndiye
mwenyekiti wa kikao hicho akataja jina lake.
‘Ndugu wajumbe wa kikao, mbele yenu ni Katibu wa CCM wa Wilaya yetu jina
lake ni…Katibu karibu sana.’
Katibu wa Wilaya alisema endeleeni na kikao tu.
Haya sasa wajumbe tunaendelea na ajenda yetu juu ya zile laki 8
zilizotoka ngazi za juu kama mgao wa kata yetu, Je tunagawana au tunazipeleka
matawini? Mwanakwetu wajumbe kimyaaa kama wamepigwa nusu kaputi.
‘Ndugu wajumbe maelekezo ya barua yenye kumbukumbu namba hiyo… ya Katibu
wa CCM ya Wilaya juu ya pesa hizi kwenda matawini yanapokelewa kwa ajili ya
utekelezaji.’
Wajumbe wa Sekretarieti ya Wadi walijibu.
‘Ndiyoooo…’
Mwanakwetu kikao kilikuwa kimya hakuna aliyetoa neno. Pesa hizo
kupelekwa katika matawi kwa maboresho ya chama hiki ndiyo likawa azimio.
Mwishoni Katibu wa CCM wilaya alisimama na kuwapongeza sana kwa kikao hicho na
kwenda zake.
Kumbe nyuma ya pazia Katibu Kata alipowasiliana na Katibu wa CCM wa
Wilaya awali aliweka mtego wa yeye mwenyewe (Katibu wa Wilaya) kuwepo wakati
ajenda hiyo inajadiliwa alipokuwepo wajumbe waliufyata.
Hali ya kisiasa ya kata hiyo iliendelea vizuri hadi mwaka 2017 uchaguzi
ukafanyika Katibu Kata huyu alikataliwa kabisa tena kuongoza kata hiyo lakini
chama wilaya waliingilia kati akawa katibu kwa mbinde na mwaka wa 2022 Katibu
Kata huyu hakugombea nafasi hiyo togombea nafasi hiyo tena.
.............................................................................................................
Mwanakwetu naomba kwa leo niweke kalamu yangu chini na kabla ya hapo nakuomba
msomaji wangu niyaseme haya;
CCM wanapaswa kuwekeza mno kwa wale wanaoshika nafasi ya uongozi ngazi
zote, wanaweza kuwa waliojaza fomu za uongozi wote siyo viongozi, mnawashawishi
wale ambao mnadhani watakuwa na tija kwa jamii na kama bado hawataki mnawafuata
viongozi wao wa dini kama vile Mashekhe, Wachungaji na Mapadri wawashawishi
wagombee hizo nafasi. Hili siyo kwa CCM pekee hata vyama vingine ili tuwe na
viongozi wazuri wenye kuyajali maslahi
ya walio wengi katika jamii kama Katibu Kata huyu ninayemsimulia.
makwadeladius@gmail.com
0717649257



Post a Comment