BURIANI PROFESA MASAMBA

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Mwanakwetu kwa juma zima umeme umekuwa shida kubwa hapo Malya, hivyo kidogo imekuwa ngumu simu yake ya mkononi kuhifadhi umeme, hata kusoma baadhi ya taarifa imekuwa vigumu.

Jumamosi ilipita umeme ukiwa wa mashaka mashaka na ulikatika tena na ulirudi jumapili ya Septemba 3, 2023 Jioni.

Uliporudi umeme jumapili hii alifanya shughuli zake haraka haraka alafu akasema ngoja niingie katika mtandao ya kijamii na huko alikaribishwa na ujumbe huu,

“Nilikufahamu mwaka 1992. Tukafunga ndoa 1994. Tumeishi miaka 29 tu Mwenyezi Mungu amekutoa kwangu. Upumzike kwa Amani Mume wangu, mshauri wangu na rafiki yangu. Tutaonana baadaye.”

Ujumbe huo ulipachikwa katika ukurasa wa mtandoo wa kijamii wa Mtangazaji na Mtayarishaji Vipindi wa TBC, ndiye Mkuu wa wa Idhaa ya TBC Taifa kwa sasa Shida Masamba ambaye awali alikuwa akifahamika kama Shida Waziri, huku jina lake lilibadilika kuwa Shida Masamba baada ya kuolewa na Profesa Masamba nguli wa Kiswahili nchini Tanzania na ambaye ameshiriki kutayarisha kamusi nyingi za lugha hii.

Hapo Mwanakwetu alibaini kuwa kumbe Profesa Masamba Masamba amefariki dunia.

Mwanakwetu alimtumia ujumbe wa Pole Mtangazaji & Mtayarishaji Vipindi wa TBC Shida Masamba.

Taarifa hiyo ya msiba ilimbeba mzega mzega Mwanakwetu hadi katika mambo kadhaa ya miaka mingi nyuma.

Mosi,

“Mwaka 2003 Mwanakwetu alikuwa akifundisha somo la Kiswahili katika shule moja binafsi ya Kimataifa iliyokuwa na Shule ya Msingi na Sekondari kuanzia darasa la Saba na Kidato cha Kwanza hadi ya Nne. Huku Mwalimu Mwenzake mmoja kike akisomesha somo hilo Darasa la tatu hadi la sita. Profesa Masamba wakati huo alikuwa na Kijana wake wa kiume mwenye jina lake (Masamba Masamba), mwaka 2003 alikuwa darasa la tatu, Mwalimu mwezake Mwanakwetu aligafilika na kuweka  mkasi badala ya vema katika swali mojawapo la somo la Kiswahili. Hilo lilimtoa Profesa Masamba Chuo KIkuu cha Dar es Salaam na alifika shuleni hapo na kuidai alama ya kijana wake mdogo. Huku jambo hulo liliongeza umakini mkubwa kwa walimu wa shule hii akiwamo Mwanakwetu ambaye wakati huo alikuwa ndiyo amehitimu Stashahada wa Ualimu kutoka Chuo cha Ualimu Kasulu Kigoma sasa ni zaidi ya miaka ishirini iliyopita.”

Mzega mzega huo wa simanzi ulimbeba Mwanakwetu hadi akakumbuka kuwa alipokuwa mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania alikuwa akifanya kazi kwa karibu sana na Shida Masamba ambaye wakati huo alikuwa ndiye mpangaji vipindi vinayokwenda hewani na akiwa na jukumu la kuvisikiliza kabla ya kwenda hewani, pia alikuwa Mtayarishaji wa Kipindi cha Husia wa Baba.

“Kama siyo Juhudi zako Nyerere, kama Siyo Juhudi Zako Nyerere, Mshikamo tungetoa wapi.”

Msomaji wangu huyu huyu Shida Masamba ndiye aliyeundika ujumbe huo na mke wa Profesa Masamba ambaye leo hii amefiwa na mumewe. Mwanakwetu akakumbuka hata Wazazi wa Shida Masamba akiwamo Mzee Waziri mwenyewe walikuwa wakikaa Mbagala ambapo Mwanakwetu alishafika mara kadhaa.


(Shida Masamba)

Mwanakwetu alikumbuka hata baadhi ya vipindi alivyowahi kutayarisha na Bi Shida Masamba zikiwamo hata jingles za Mwalimu Nyerere ambazo hadi kesho zinachezwa na TBC Taifa, Ikiwamo ya Mgiriki aliyetiwa ndani ya Mwalimu Nyerere.

Mzegamzega huo wa simanzi uliendelea kumteka Mwanakwetu akakumbuka,

“Wakati wa Ramadhani ya kila mwaka, Shida Masamba alikuwa na utaratibu wa kila kumi la mwisho kuwaalikia baadhi ya wafanyakazi wenzake na majirani kwenea kufuturu nyumbani kwake Mwenge Dar es Salaam. Mwanakwetu japokuwa Mkristo kila mwaka alialikwa na hiyo fursa kila mwaka aliitendea haki ipasavyo. Huko Mwanakwetu alikutana na Profesa Masamba na mwanafunzi wake Masamba Masamba yule aliyepokwa alama akiwa darasa la tatu na wakati huo alikuwa Chuo Kikuu huko Uchina.”


Mwanakwetu akiwa na mzegamzega huo simanzi anasema nini?

Kwa heshima zote anatoa pole kwanza kwa Shida Masamba kwa kufiwa na mumewe, anatoa pole kwa mwanafunzi wake Masamba Masamba kwa kumpoteza baba yake mzazi ambaye alijali mno elimu ya mtoto wake japokuwa alikuwa Profesa wa Chuo Kikuu akiwa na majukumu mengi, Mwanakwetu pia anatoa pole kwa familia nzima ya msomi huyu popote ilipo kwa kumpoteza ndugu yao

Buriani Profesa Masamba.

makwadeladius@gmail.com

0717649257



0/Post a Comment/Comments