EMBE DODO UPANDE

 


 


Adeladius Makwega-MWANZA

Chama cha Mapinduzi kinapofanya mikutano yake ya ngazi za chini na ile ya kitaifa kimekuwa na taswira mbili fofauti zinayojengeka machoni mwa yule anayefuatilia mikutano hiyo.

“Unapoutazama mkutano wa kitaifa unakutana na picha za wajumbe wote wakiwa wamependeza sana na sare zao zinawakawaka na wakisindikizwa na bashasha katika mapaji ya nyuso zao.”

Wajumbe hao wakizungumza kwa furaha na ni mara chache mno kuona mjumbe wa CCM katika mikutano hiyo  ya kitaifa akipinga jambo hadharani, utamaduni huo huwa ni ni mwiko kwa vikao hivyo kusikia msamiati hapana mara nyingi mambo huwa ni ndiyo.

Swali la kujiuliza Je taswira ya mikutano ya kitaifa ya CCM ndiyo taswira ya mikutano ya CCM ngazi za chini?

 

“Taswira ya wajumbe katika vikao vya chini huwa ni wale waliovalia sare zilizochaka, kupauka na kuchujuka mno, huku wengine wakijaliwa kuwa na labda kofia ya CCM tu, mwingine akijaliwa kuwa na shati tu rangi ya kijani au njano huku sketi au suruali ikiwa ya rangi nyengine.”

Hizo ni sura mbili tofauti lakini chama cha siasa kile kile chenye bendera moja yenye kijani tupu lakini ina nendo yake za nyundo na jembe.

 Loooo salaleeee! hiki ni chama cha Mwanakwetu.”



Panapomalizika vikao hivyo vya chini hoja ya kuwarejesha wajumbe mashinani kwao ikiwa ngondo, wengine wakirudi majumbani mwao kwa miguu, pengine kukosekana kwa mtu wa kutoa hisani ya wajumbe hao kurudi majumbani kwa kutoa basi au lori. Huku jambo la msingi la wao kukamilisha akidi ya kikao likiwalimefanyika. Wajumbe na viongozi wa CCM kutokana ngazi za chini hata wao wanapoitazama taswira ya mikutano ya kitaifa ya chama chao inawavutia mno na wao kutamani kuwa miongoni mwa wajumbe hao,

Mwanakwetu hiyo kwao huwa ni fahari ya macho tu wanaona katika kideo tu, kuomba kura na kufika huko ni kazi nzito mpaka kuwaona wajumbe wote na kuwapatia maboresho ni zoezi zito ambalo Mwanakwetu haliwezi, zoezi hilo linaitaji mtu awe mfuko uliojaa mapesa.

“Mwanakwetu fukara wa kutupwa, hapo lazima uwe Lodi.”



Mwanakwetu akiwa katika tafakari nzito juu ya chama hiki kilichozaliwa na TANU na ASP vyama viliyowakombea wanyonge anafananisha taswira hiyo ya chama hiki na EMBE DODO UPANDE.

Msomaji wangu pengine wewe ni mgeni wa Embe Dodo Upande !

“Kuna aina mbili za embe dodo; Dodo ya Kawaida ambayo huwa embe kubwa chachu kidogo ikiwa mbichi na ikiiva ni tamu sana, pande zote hadi kokwa. Aina ya pili ni ya Embe Dodo ni Embe Dodo Upande hii huwa inafanana na Dodo ya Kawaida bali chachu sana ikiwa mbichi na hata ikiiva huwa na uchachu na utamu kidogo.Ukifika maeneo ya pwani kama vile Mkuranga, Mkamba, Kiziko, Kisere, Magoza, Kiparang’anda na mwanadilatu Dodo Upande inatumika sana kutengeza siki na chachandu ambayo kidogo inakuwa  kiungo cha kuongeza hamu ya kulia chakula tu. Hiyo ndiyo kazi kubwa ya Embe Dodo Upande kutengeneza siki na chcahandu ya kulia chakula, thamani yake siyo sawa na Embe Dodo la Kawaida.”



Mwanakwetu Upo?

Ndiyo maana Wazaramo, Wakwere, Wandengereko, Wamakonde, Wapogoro na Warugulu hii Embe Dodo Upande hiyo ndiyo kazi yake.

Jukumu la viongozi wa sasa wa CCM bila ya kutafuna maneno wanayo kazi ya kuubadilisha huu Muembe Dodo Upande uwe Muembe Dodo wa Kawaida, kazi kwao. Mwanakwetu kwa mapenzi ya dhati kwao anawapa mbinu moja waubatize huo muembe mara moja ili matawi yake yasizae Embe Dodo Upande tena.

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257








0/Post a Comment/Comments