Adeladius Makwega-MWANZA
Aprili 30, 2023 Mwanakwetu alipokuwa Kanisani misa ikikaribia
kumalizika umeme ulikatika, kanisani kukawa giza, lakini mshumaa wa pasaka na
mishuma miwili ya altare iliokoa jahazi, Padri alitoa baraka ya mwisho na
waamini wote kutoka kanisani kurudi majumbani mwao.
Hapo Mwanakwetu alishindwa kufanya kazi zake katika kompyuta
yake, hivyo aliamua kwenda katika soko la Malya kuhemea. Akilini mwa Mwanakwetu
akiwa njiani sokoni alisema,
“Eneo hili umeme unakatika sana.”
Alipofika sokoni aliona kuwa siku hii ilikuwa kuna gulio,
huku vitu kadhaa vikiuzwa, Mwamakwetu alivutiwa mno kununua makatambuga ambayo
yanatengenezwa kwa kutumia matairi ya gari, misumari na shanga.
Alipouliza bei kijana muuzaji alisema yanauzwa kati ya shilingi
2000/=-4000/=, Mwanakwetu alitoa shilingi 2000/= hapo hapo lakini muuzaji
alikataa fedha hiyo kwa kuwa ilikuwa imeungwa.
“Kaka nikipokea pesa hii nitagombana na bosi wangu na
atanikata katika malipo yangu ya siku ya leo jioni, nakuomba kama una pesa
nyingine nilipe .”
Mwanakwetu alitoa pesa nyingine na kurudishiwa chenji yake,
alichagua makatambuga hayo alafu akaanza kuondoka. Kijana muuzaji ambaye aliongea
Kiswahili chenye sarufi nzuri lakini chenye matamshi ya Kisukuma alimuita na
kusema haya,
“Wewe ni mgeni wa Malya na mgeni wa makatambuga. Ukinunua
haya unawajibu wa mimi kukurekebishia, ona hii misumari imesimama, ukivaa
itakuumiza bure.”
Msomaji wangu kijana huyu alifanya hivyo vizuri sana na kuvikabidhi
viatu kwa Mwanakwetu. Mwanakwetu alimuuza kijana huyu je kwa siku anauza katambuga
ngapi? Kijana alijibu kuwa inategemea na hali ya soko lakini ni kati ya 10-20
na ana jozi 500 ndani ya mifuko miwili.
Mwanakwetu alimuuliza maswali mengine: ; Je ameanza kazi hiyo lini? Na analipwa kiasi gani kwa siku?
“Ninalipwa shlingi 10,000/= huku shilingi 6000/= ni yangu, 1000
ni ya chakula cha mchana na huku 2500/= ni ya kupakia katika lori kwenda na kurudi
gulioni. Kazi hio nimeanza baada ya kumaliza mitihani ya kidato cha nne mwaka
jana, maana sasa nangoja kwenda kidato cha tano na nimefanya vizuri .”
Mazungumzo hayo na kijana huyo alisema bayana kuwa amesoma
shule ya kanisa, amepata daraja la kwanza na atasoma kidato cha cha tano
Fizikia, Kemia na Hesabu. Mwanakwetu akaagana naye na kwenda zake.
Mwanakwetu akiwa anarudi njiani alikutana na mama mmoja mtu
mzima sana, akacheka mno kwa Mwanakwetu kununua makambuga aliyokuwa ameyashika
mkononi, alafu akamuuliza sasa mbona hawajakupa mfuko wa kuwekea? Pole, sasa umekuwa
msukuma. Mama huyu mwenye mvi akavichukua viatu vya Mwanakwetu alafu akasema
unaona viatu hivyo vimevishwa shanga tatu? Mwanakwetu akajibu ndiyo, akaulizwa
je unaelewa maana yake? Mwanakwetu akacheka, alafu akasema sielewi.
“Sasa lazima uwe Msukuma, Shanga tatu maana yake viatu hivyo
vinavaliwa na watu watatu; Baba, Mama na mtu mwingine, huyo mwingine akilini
kichwani mwako. maana hivi ni viatu vya kuogea.”
Mwanakwetu alicheka sana, alafu
akamuuliza jina lake bibi huyu ambaye kwa umri kwa mtazama ni kati ya miaka
70-80 akataja jina lake alafu akisema yeye ni mwalimu mstaafu.
Mwanakwetu aliagana nae mama huyu na kuelekea nyumbani kwake,
hata alipofika kwake umeme ulikuwa bado haujarudi hadi saa nane ya mchana ndipo
ulirejea. Umeme uliporudi akaamua kuandika hekima hii ya shanga za katambuga na
mgeni wa katambuga.
0717649257
Post a Comment