Mwanakwetu juma lilipopita alisafiri kutoka Lushoto Mjini kuelekea
Arusha, kwa kuwa ilikuwa siku ya Jumapili aliona ni vema asali misa ya Jumapili
kabla ya kuianza safari ndefu kwenda huko aendapo. Misa ilipomalizika alikuwa
chakula cha mchana ndipo alianza safari hiyo muda wa mchana na kufika Mombo
majira ya jioni. Hapo Mombo alishuka na kupata gari ndogo ya vijana ambao walikuwa
wakielekea Arusha Mjini.
Vijana hawa walikuwa wanakwenda Arusha lakini walikuwa
hawakufahamu, kwa hiyo walihitaji mtu ambaye anaifahamu njia hiyo, kwa hiyo
Mwanakwetu alikuwa ni mtu sahihi sana. Vijana hawa walisema kuwa Mwanakwetu
atoe shilingi 10000/=, kweli alifanya hivyo. Kwa bahati nzuri walipatikana watu
watatu wanaoifahamu Arusha mmoja alipanda gari la mbele na wawili akiwamo
Mwanakwetu walipanda gari dogo la nyuma na safari ikapamba moto. Wakiwa ndani
ya gari hiyo, viti vya mbele alikuwapo dereva na binti mmoja, kwa kuwatazama
walikuwa ni wapenzi. Msomaji wangu niseme nisime? Hapo lazima unipe mji
nikusimulie , maana mwanzako nililipa shilingi 10000/ kuyaona haya .
Natambua msomaji wangu umenichagulia Mbagala-Temeke au Ulanga
Morogoro, huko nakupenda sana, ngoja nikusimulie uhondo.
“Watu wenye ndoa wakiwa pamoja ndani ya gari, mara nyingi
kila mmoja anakuwa na luake,wananuniana mno, hawawezi kuongea wala kucheka ,
wala kusomeana ujumbe, lakini wapenzi, wasio na ndoa au mtu kamuiba mke wa mtu
mwingine, Mwanakwetu wataongea mengi, mikumbatano na mabusi teletele juu yake
hao.”
Msomaji wa Mwanakwetu unahitaji mtama umwage katika kuku wengi
ujue kilichokuwa kinaendelea safarini? Natambua umeshaelewa. Mwanakwetu sasa ni
mzee hawa walikuwa ni rika za watoto wake wa kuwazaa kabisa yeye yake macho
ukawakaripia unarudishiwa nauli yako.
Kumbuka kuwa kiti cha nyuma alikuwapo Mwanakwetu, abiria mwenzake
na kijana mwingne ambaye alifanana sura za dereva. Safari iliendelea vizuri, walipofika
Hedaru hawa vijana wenye gari walisimama magari yote mawili wakashusha mzigo wakawapa
wahusika, hapo walikaa kama dakika tano hivi. Mwanakwetu na abiria mwenzake eneo
hilo walishuka chini kukanyaga ardhi ya Wapare wa Hedaru.Huku huyu abiria
mwezake Mwanakwetu akasema,
“Kaka naona hedaru inabalidilika sana na inaendelea kwa kasi
mno, maana sasa hata nyumba za maghorofa zinajengwa.”
Dereva na wenzake walirudi, wakaingia garini kuendelea na safari
yao Arusha, sasa walikuwa wakiitafuta Same Mjini. Hapo kando abiria mwenzake
Mwanakwetu akasema,
“Kaka unaiona Same? Sasa inatanuka mno, mji unazidi kuwa
mkubwa, nyumba mbalimbali za ibada zinajengwa za kila kona, shule na vyuo pia
zinainuka kama uyoga.”
Sasa gari hizo dogo ndiyo zinaingia Same Mjini, madereva waliingia
kituo cha mafuta ili waweke mafuta. Hapo Mwanakwetu na huyu abiria wakashuka
kuchimba dawa na kununua Korosho ,alafu wakawa kando ya gari hilo.
Mwanakwetu akamwambia huyu abiria mwenzake,
“Mimi nimesoma hapa mwaka 1994/95, palikuwa
duni sana, pakame, mno, ukitafuta hata ndizi, chungwa au embe ilikuwa tabu
kupata , kulipatika miwa migumu tu. Shuleni kwetu pale Same Sekondari alikuwepo
Mwalimu aliyefahamika kama Miss Yona ailifundisha somo ya Kiingereza na pia
alikuwa mwalimu wa darasa. Huyu alikuwa bibi mmoja wa Kipare, alinipenda sana
mwalimu wangu huyu. Mara nyingi kila wiki siku ya ijumaa tulikuwa na vipindi
vichache ananitumamjini kumchukulia nyama katika mabucha ya Chediel Mgonja-ambaye
alikuwa Waziri wa Elimu ya Taifa na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Same.Huku
nikipata nafasi ya kula nyama hiyo baada ya Miss Yona kuipika.Miss Yona alikuwa
mwalimu mmoja msafi sana huku akiwa na ania kadhaa za viatu, vile vya
kutembelea nje ya nyumba na vile vya kuvaaa ndani ya nyumba. Kwa kuwa nilikuwa naingia
ndani ya nyumba yake alinipa hata viatu vya kuvaa ndani ya nyumba yake
akinituma kwa mheshimiwa Chediel Mgonja.Baadaye nilibaini kuwa Miss Yona binti
yake aliyekuwa anasoma sekondari mkoa mwingine alikuwa na ubini wa Chediel
Mgonja.Kwa hakika kila siku ya Ijumaa maharage meupe kwa Mwanakwetu yalikuwa
likizo maana Miss Yona alinpa bakuri la nyama.”
Gari likaendelea na safari, huku kijana huyu akimuuliza Mwanakwetu
juu ya Miss Yona, mwalimu wake wa darasa yupo wapi? Mwanakwetu aliibu kuwa ni
miaka mingi sasa, hafahamu mama huyu yu wapi lakini anakumbuka tu mheshimiwa
Chediel Mgonja alifariki dunia.
Abiria mwenzake Mwanakwetu akasema kweli sasa Same hata kijani kibichi kinaonekana, safari inaendelea sasa wakawa wanakaribia Mwanga. Kijana huyu akaongeza kuwa Mji wa Mwanga hauendelei unabaki vile vile naona kuna dalili ya Same kuizidi Mwanga. Naye Dereva wa gari hilo akasema naona Mwanga barabarani hawana miti mingi, labda kule nyuma, huyu kijana abiria mwingine akasema hapa panaitwa Kisangara na wao wana maendeleo kidogo na huu ni mji wa matajiri wa Mwanga.Safari inaendelea huku dereva huyu akawa na nidhamu kidogo kwa kutambua kuwa kumbe ndani ya gari wamepanda wazee.
Mwanakwetu akasema,
“Mimi naifahamu Mwanga na Same ya vipindi tafauti, maana
miaka 1980 nilikuwa napita na mama yangu kuelekea Kilimanjaro Babu yangu mzaa
mama alikuwa akifanya kazi, ukipita na treni pale Same usiku unakutana na taa
chache cha eneo hilo hasa stesheni , Shule ya Sekondari Same na Gereza la Same
wakati ukipita Mwanga zilikuwa nyingi .”
KIjana huyu abiria mwenzake aliungama kwa Mwanakwetu kuwa
yeye ni Mpare wa Mwanga, hapo ni nyumbani kwao.
“Ninafanya biashara Moshi Mjini, shida ya Mwanga ndugu zangu
hawa wanataka kufanya biashara wenyewe, hatutaki kuwakaribisha wageni, hilo
ndilo changamoto. Kama unataka eneo liendelee tunatakiwa kuchangamana na
wengine mathalani kama mnachagua hata viongozi wa vijiji au nyumba za ibada
wachanganike mgeni-mwenyeji, mwenyeji -mgeni.”
Kumbuka msomaji wangu safari inaendelea Mwanakwetu akatamani
kufahamu kati ya Mwanga na Same Halimashauri zao zina hali gani ya kimapato?Aliiingia
hapo,
Kubaini kuwa,
“Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halimashauri ya Mwanga ilikusanya
asilimia 97 ya makusanyo yake yote ikiwa ni shilingi 3,074421,566.97 (Bilioni
3.07) wakati malengo yalikuwa shilingi 3,166,000,000 (Bilioni 3.17) na Same walikusanya
asilimia pia 97 ambapo mapato yao ya mwaka ni shilingi 2,508,407,143 (Bilioni 2.51) wakati malengo
yalikuwa ni shilingi 2,589,000,000 (bilioni 2.51).”
Hapo akilini mwake alikumbuka kuwa kuna
wakati Halimashauri ya Same iliongozwa na mwanasheria Anne Clear Shija(dada wa
Mwanakwetu) na mkuu wa Wilaya alikuwa
Mhe.Rosemary Senyamule ambaye ndiye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo hii.
Mwanga iliizidi Same kwa tofauti ya milioni 500 kwa mwaka huo
wa fedha huku malengo ya Mwanga yakiwa zaidi ya Same, huku uchumi wa Mwanga
ukiwa juu ya hiyo nusu bilioni.Huku Mwanga wakiwa na kiwanda cha Spirit na Same
wakiwa na Mkonge na mbuga ya Mkomazi. Walipofika Moshi Mjini abiria huyu alishuka
na kwenda zake naye Mwanakwetu na hawa wenye gari waliendelea na safari
kuitafuta Arusha Mjini.
Mwanakwetu aliona wazi kuwa Anna Clear Shija na Mhe. Rosemary
Senyamule walifanya kazi kubwa kuisuka Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wakati
huo na kuna kila dalili Same itaivuka Mwanga ndani ya kipindi cha miaka mitano
kuanzia sana hilo Mwanakwetu analitabiri wazi wazi.
Mwanakwetu alifika Arusha Mjini na kuuchapa usingizi kungoja
kuche aendelee na safari yake huko aendapo akiitafakari mno wilaya ya Same na
Mwanga, mawazo yake pia yalimkumbuka Miss Yona mwalimu wake wa darasa na somo
Kiingereza huku Nyama ya Mheshimiwa Mbunge na waziri zamani ikimjia akilini
mwake wakati ule akiwa mwanafunzi pale Same sekondari.
Mwanakwetu wakati anaandika matini haya alitambua fika wapare wa Mwanga watasema tu Mwanakwetu anaisifia Same kisa kala nyama za Chediel Mgonja, hiyo ni kweli lakini amekula nyama kupitia kwa mwalimu wake Miss Yona,isitoshe Mwanakwetu kasoma Same pia hakuna ubishi Same inakua kwa kasi mno.
Mwanakwetu upo?
0717649257
Post a Comment