Adeladius Makwega-MWANZA
Aprili 27, 2023 Mwanakwetu alifanya mazungumzo na Philemoni
Kelvin Felix ambaye ni miongoni mwa Watanzania waliosoma Shule ya Sekondari ya Tambaza
hapo zamani na miongoni mwa kaka zake. Felix pia alisoma Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kushiriki karika kulicheza kabumbu la Tanzania, uchezaji wake huo wa
soka akikutana na watu wengi maarufu katika soka na siasa za Tanzania.
Katika mazungumzo hayo kwa njia ya simu yaliyotumia dakika 16
na sekunde 43 mengi yalizungumzwa likiwa hili,
“Katika kile kipindi chetu sisi, huyu Charles Kitwanga ambaye
aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, huyu huyu, yeye alikuwa anacheza
mpira wa kikapu na yeye ndiye alikuwa Waziri wa Michezo katika Serikali ya
Wanafunzi pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.”
Hawa vijana wa UDSM wakati huo walimchagua Charles Kitwanga
kuwa Waziri wao wa Michezo kwa hoja mojawapo, alikuwa anacheza mpira wa kikapu,
yeye alikuwa miongoni mwa wanamichezo hapo chuoni.
Mwanakwetu kwa sasa hajaonana na Mzee Kitwanga kwa muda, kama
akikutana naye atamuuliza vipi bado anacheza mpira wa kikapu? Kwa wale ambao
hamfahamu Charles Kitwanga kwa namna alivyo mrefu, kwa hakika alikuwa mchezaji
mzuri wa mchezo huo , japokuwa wapenzi wa mpira wa kikapu walikuwa wachache
pale UDSM, Mpira wa Kijapu ukitazamwa kuwa mchezo wa mabishoo siyo mchezo wa
magangwe kama soka na ngumi.
Japokuwa tangu Kitwanga na wenzake waliyohitimu UDSM sasa ni
miaka mingi lakini vijana wote wa wakati huo hapo UDSM wanamkumbuka Kitwanga
kama kiongozi wao hodari wa michezo hadi leo. Huku wakikumbuka hata shule
alizosoma kabla ya UDSM,
“Charles Kitwanga alikuja UDSM, awali alisoma sekondari za Same-
Kilimanjaro na baadaye hapo Tosamaganga Iringa.”
Kwa mtu ambaye hakusoma naye kiongozi huyu hapo UDSM kama ilivyo
kwa Mwanakwetu anamtambua ndugu huyu kwa nafasi zake alizokuwa nazo za Mkurugenzi
Msaidizi pale Benki Kuu na Uwaziri wake wa Mambo ya Ndani ulivyokuwa. Ndiyo
kusema yule aliyekuwa naye UDSM anamfahamu katika sura nyingi zaidi kama ilivyo
kwa ndugu Felix,
Kwa mtu anayelifahamu jambo katika sura mbili ni mtu mzuri zaidi kulielezea tafauti na yule anayeliona kwa sura moja, jambo linapotazwa katika sura mbili hapo unapata picha kamili ilivyo. Inawezekana ukayafahamu mazuri mengi, huku pia ukipata picha ya kuyafahamu mabaya zaidi. Kubwa na la msingi ni kulifahamu jambo kwa kina, siyo kwa kubabiababia. Ndugu Philimone Kelivin Felix anawakumbuka wanamichezo kadhaa wa wakati huo hapo UDSM huku akiwataja mmoja baada ya mwingine.
“Pale Chuoni tulikuwa na mtu anaitwa Charles Gasper, huyu pia
alikuwa anachezea Yanga, yeye ndiye alikuwa beki nambari tano wa Chuo Kikuu
lakini pia akichezea timu ya Yanga ya Dar es Salaam, hapo alikuwapo pia Lawrence
Mwalusako ambaye alikuwa nyuma yetu, kwa mwaka mmoja, wao walitakiwa kumaliza
mwaka 1989, walipata shida ya kumtukana Rais Ali Hassan Mwinyi wakapewa adhabu
ya kuhitimu mwaka 1990. Katika kundi letu walikuwepo Mtemi Ramadhani, na Leodger
Tenga, huyu Tenga yeye alisoma Shahada ya Uhandisi lakini alikuja pale kusoma
Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara(MBA), kwa maana alikuwa Mkurugenzi wa
Land Rover Tanzania. Pia kulikuwa na jamaa mmoja aliyeitwa Shah Hanzuruni
(marehemu sasa), wakati huo alikuwa anachezea Waziri Mkuu ya Dodoma, alikuwa ni
mchezaji mzuri sana, alikuwa mchezaji muhimu na hata katika timu ya taifa alikuwa
anaitwa kuichezea Taifa Stars. Hata huyu Mtemi Ramadhan na yeye alitokea Dodoma
kabla ya kwenda Simba, hao walikuwa wachezaji muhimu sana, wachezaji wengine ni
Jaji Francis Mutungi yeye alikuwa kipa wetu, huyu Msajiri wa Vyama vya Siasa. Jaji
Mutungi alikuwa kipa tangu Tambaza na tulisoma naye. Kipa mwingine alikuwepo
kijana mmoja aliyesoma Forodhani Sekondari Endrew Maro (kaka wa Anna Mkapa),
wachezaji wengine waliokuwa wanaingiaingia ni Erick Shitindi aliyekuwa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Kazi, amestaafu akiwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.”
Msomaji wangu maelezo haya juu yanatoa picha ya vijana hao wa
Tambaza na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam namna walivyokuwa wanashiriki michezo
na namna walivyokuwa jirani tangu wakiwa wanasoma. Kwa kutazama kwa kina majina
hayo yote yameshika nafasi mbalimbali za Kitaifa lakini aliyeongoza katika
michezo ni Leodger Tenga Pekee.
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini ?
Katika utafiti wake amebaini kuwa japokuwa Charles Kitwanga
alikwa waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini hakuwai
kuwa waziri wa michezo katika serikali yetu. Hilo Mwanakwetu anaona kuwa hakuna
aliyeona kuwa ndugu Kitwanga anaweza kuifanya kazi hiyo vizuri.
Mwanakwetu anayasonta makosa yetu katika hilo akiamini kuwa tulikosea mno, maana Kitwanga alikuwa na uwezo wa kuifanya vizuri kazi
hiyo ya Uwaziri wa Michezo kuliko mtu yoyote kwa hoja nyingi sana, leo msomaji
wake anakutajia moja ambayo ni kuwa na mahusiano makubwa na wanamichezo wengi wa
wakati huo ambao aliwaongoza pale UDSM katika michezo akiwamo Leodger Tenga
ambaye aliongoza vizuri TFF na BMT.
Mwanakwetu anaiweka chini kalamu yake siku ya leo akisema kuwa
Charles Kitwanga ni kiongozi wa michezo ambaye tumempoteza njiani.
0717649257
Post a Comment