Adeladius Makwega –MWANZA
Mwanakwetu alilala katika iji la Arusha vizuri na kuamka asubuhi
sana ya siku iliyofuta ambapo alitoka hapo nyumba ya wageni na kufika stendi,
alipokaribia stendi ya Arusha Mjini ambayo ni stendi ya miaka mingi,
haijaboreshwa alipokelewa na wapiga debe kadhaa, mpiga debe wa siku hii alikuwa
baba mmoja mnene, mrefu na mtu mzima.
Mwanakwetu alipoulizwa unakwenda wapi? Alijibu kuwa anakwenda
Musoma, mpiga debe huyu alisema kuwa mabasi yapo mengi yale yanayopitia Singida,
Mwanakwetu alijibu kuwa yeye anapitia Serengeti,naye mpiga debe alijibu haya,
“Njia ya Serengeti inaruhusiwa basi moja tu kwa siku, ngoja
tuangalie kama lipo kwa kuwa basi moja linatoka Musoma na lingine likitokea
Arusha, yanakutana katikati.”
Walitoka hapo hadi linaposimama basi hilo, palikuwa wazi,
hivyo Mwanakwetu alimuuliza mpiga debe huyu sasa ninafanyaje? Alijibiwa kuwa,
“Unaweza kupanda kwa kupitia Singida, njia ya Arusha Serengeti
Musoma ni fupi inakaribia KM 400 tu lakini kupitia Singida ni KM 1100.Hapo basi
linatumia mafuta mengi na hata nauli inakuwa kubwa sana, maana kama KM 400 na
barabara ni nzuri nauli ingekuwa kidogo, na piamafuta yangetumika kidogo.
Kumbuka wanyama wangekufa sana. Kama inatengezwa basi wangeweka sheria kali, na
taa nyingi bungani.”
Mwanakwetu alielekea na mpiga debe huyu upande zilipo basi za
Arusha Singida Musoma/Mwanza na alilipa shlingi 40,000/= na kupanda basi ya Arusha-Mwanza.
Basi hilo lilikuwa na jina Loliondo. Mwanakwetu akapewa kiti namba 46 kikiwa
cha mwisho mwisho.
“Nimekuona unatafuta mabasi ya Musoma kupitia Serengeti, pole
sana kwa kulikosa, njia hii ingewekwa lami ingetuingizia pesa nyingi sana,
lakini ndiyo hivyo tena, tuombe Mungu tu.”
Wakiwa wanazungumza Mwanakwetu na jirani yake katika kiti
chao, pembeni yao kwa mkono wa kushoto alikuwa amekaa dada mmoja na mara akaingia
dada mmoja mzungu. Dada huyu mzungu alimwomba dada mweusi ampishe katika kiti
chake cha dirishani. Dada mweusi alijibu kuwa kiti chake ndiyo cha dirishani.
Hapo yakawa mabishano kwa lugha ya Kiingereza, Mwanakwetu alipomtazama binti
mweusi alikuwa kama ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu huku akizijenga sentensi zake
za kiingereza vizuri sana.
Binti mzungu akasema ngoja nikae kiti cha nyuma akija
kondakta ataamua ugomvi huu, dada Wakitazania akasema ndiyo. Kumbuka Mwanakwetu
na jirani wanafuatilia ugomvi huo kwa kina, Msomaji wangu kumbuka unapokuwa na
mgeni kando kutoka taifa lingine wewe unakuwa balozi wa taifa lako.
Mwanakwetu akamwambia abiria mwenzake kwa sauti ya chini,
“Huu mjadala wa kiti dirishani atashinda mzungu, nakwambia , hawa
jamaa wako makini mno kwa mambo yao, kama anakidai kitu tambua ni haki yake.
Sisi unaweza ukamwambia kondakta nikatie kiti cha dirishani, wala uhakikishi,
ngoja tuone mchezo utaishaje?”
Kweli baada ya dakika tano alifika kondakta na kuangalia
tiketi zao na kumwambia dada mzungu akae dirishani, naye dada yetu wa Kitanzania
akakaa kiti cha pembeni mkabala na Mwanakwetu.
Abiria waliendelea kuingia ndani ya basi hilo, alifikia
kijana mmoja ana begi lake, akajaribu kulingiza katika sehemu ya kuweka mizigo
ndani ya basi hilo juu kwa nguvu, kondakta akafika na kuyatoa maneno haya,
“Wewe hauoni basi ni mpya, unataka kuvunja taa bure.Taa hizo ni
nzima kwa kuwa zimetunzwa”
Kijana aliyeambiwa hivyo aliuliza sasa aweke wapi mzigo wake?
Kondakta aliseme kauweke chini buti, kijana akapinga hilo akisema kuwa begi
lake halikai huko, mjadala ukawa mkubwa, kijana akaomba arejeshewe pesa yake.
Hapo kondakta alikuwa mzito kwa dakika tatu hadi nne, baadaye walimuwekea mzigo
vizuri na kijana akakaa katika kiti chake. Hapo huyu kondakta mkorofi akashuka hakuonekana
tena ndani ya basi. Kumbe basi hilo lilikuwa na kondakta binti mmoja mwelevu,
makini , mpole na anaipenda kazi yake.
Msomaji wangu kumbuka dada mzungu na dada mswahili wapo kiti
kimoja je wataongea safarini? Mwanakwetu safari ilianza wapo kimya safari nzima
kimya kikuu kila mmoja akichezea simu yake, jirani wa Mwanakwetu akasema,
“Dada huyu wa kizungu ningekaa naye
mimi, ningempa simulizi zote za Tanzania, kaja hapa kutalii ili aifahamu
Tanzania lakini kama akishuka Mwanza nitazungumza nae .”
Basi hili lilikata mbuga na kuvuka mikoa kadhaa na hata lilipofika
Singida dada jirani na mzungu alishuka, kwa hiyo kiti kile kikawa kitupu, hivyo
jirani wa Mwanakwetu aliamua kuhamia kwa dada mzungu.
Mwanakwetu kwa simu alizokuwa anaongea dada huyu wa kizungu alibaini
kuwa alikuwa Muitaliano maana maneno kama Monasela, Tuti, Caza na Bambino yalisikika mno katika sentensi zake
alizoongea kwenye simu.
Mwanakwetu akatulia tuli huku akiyafuatilia mazungumzo ya jirani
yake na dada mzungu, kwa kuwatazama huyu jirani wa Mwanakwetu na dada mzungu
walikuwa ni mzao mmoja, hapo mambo yalikuwa safi kabisa.
Mwanakwetu alitazama tabasamu la dada wa kizungu lilikuwa
kubwa, sasa akicheka pale huyu jirani wa Mwanakwetu akitupa maneno ambayo
Mwanakwetu hakuyasikia. Baadaye Mwanakwetu alianza kusikia mazungumzo yao na
huyu dada akisema anatokea Milano-Italia amekuja Tanzania kutalii na anakwenda
Mwanza.
Jirani wa Mwanakwetu alimuliza dada mzungu mbona umegombana na
jirani yako Je mnafahamiana ? Dada mzungu alicheka akisema hamfahamu dada huyo
aliyeshuka Siongida. Jirani wa Mwanakwetu akimwambia dada huyu mzungu kuwa hapa
Tanzania ukiwaona wanawake wanagombana fahamu kuwa wanamgombania mwanaume, Je umemchukuliwa
mumewe ? Dada mzungu alicheka sana alafu akasema maneno haya,
“Tanzania sijakuja na mume niko mwenyewe.”
Maneno yalikuwa matamu huku jirani ya Mwanakwetu aliomba
nafasi hiyo apewe yeye, dada mzungu alicheka sana akisema kuwa yeye hawezi
ugomvi kugombana ugenini, maana, jirani wa Mwanakwetu alionekana kama ana mke.
Mwanakwetu aliposhuka katika basi hilo akilini mwake
alifurahia mno namna kijana huyu wa KItanzania alivyotuwakilisha vema kwa binti
mtalii wa Kiitaliano kutoka Milano. Kijana huyu aliweza kuyafuta yote mabaya
kwetu kutoka wa abiria yule binti mwanzoni mwa safari.
Mwanakwetu upo? Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment