UWONGO WA ASKARI SI UKWELI WA RAIA

 

 

 

 UWONGO WA ASKARI SI UKWELI WA RAIA

Adeladius Makwega-Buigiri

Kwa wakati huo mwanakwetu alikuwa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Tambaza na shule za sekondari zote zisizo za bweni yaani za kutwa kwa jiji la Dar es Salaam zilikuwa chache mno, mwanakwetu anakumbuka kwa mwaka 1989 na 1990 jumla ya wanafunzi waliokuwa wakifaulu kutoka darasa la saba kwenda sekondari walikuwa hawazidi 5000 kwa mkoa mzima wa Dar es Salaam, yaani kila mwaka walikuwa hawazidi wanafunzi 2500.

Hiyo ilikuwa idadi ndogo sana kwa hiyo shule za sekondari zote za serikali zilikuwa katikati ya jiji hili. Kwa hiyo kwenda sekondari ilikuwa ni kwenda kuwa mjanja zaidi maana sasa ilikuwa unatoka shule za vichochoroni kwenda kusoma shule za Forodhani (Watoto wa viongozi/wazazi waliosoma-watoto wa kishua), Tambaza (Magangwe), Azania (John Kisomo-Wapenda kusoma), Kisutu (sister duu), Jangwani, (sister duu) , Zanaki (sister duu) na hata Kibasila japokuwa yenyewe ilikuwa shule pekee ya sekondari ya umma iliyokuwepo Wilaya ya Temeke na wakiwa wanafunzi watulivu  maana walikuwa mbali na jiji na harakati zake.

“Kwa muda wa jioni, kama umerudi nyumbani kutoka shuleni ulitumia muda huo kushinda katika shule za msingi ambazo tulisoma au shule zilizo jirani na maeneo yetu ya nyumbani. Nafasi hiyo tuliweza kukutana na kaka na dada zetu walio madarasa ya juu yaani kidato cha II, III, na IV huku wakitufundisha masomo mbalimbali na muda mwingine ulikuwa wakati wa kupiga soga na kufahamiana pia.” Mwanakwetu anautoa ushuhuda huo

Kama ilivyokuwa desturi yake ya kwenda shule ya msingi jirani kila jioni kujisomea, siku moja alienda shule ya msingi Mbagala, alipofika hapo alikutana na rafiki zake kadhaa ambao walikuwa wakijisomea pamoja na baada ya kumaliza kujisomea huko walikuwa wanatoka nje kutazama mazoezi ya mpira wa miguu kwa timu ya ABUJA FC (Kizuiani), TESEMA FC (Mbagala 77) na AGATON FC (Mangaya) zote hizo zilikuwa timu za Mbagala kutoka maeneo hayo kwa wakati huo.

“Unapokuwa unasoma katika madarasa haya kwa kuwa mimi ni mwanafunzi wa sekondari huwa pana wanafunzi wa shule za msingi hasa wale wa darasa la saba wanaojiandaa na mitihani yao na wao hujijengea utaratibu wa kusoma kwa hiyo mara nyingi wanakuwepo madarasani wakijisomea pia au wakikuona utasikia kaka tusaidie hesabu hii na ile basi hapo unakuwa mwalimu wa wao kila siku wanakuja kwako..

Hili kuepusha kusumbuliwa sana na wanafunzi hawa basi huwa mara nyingi ninakaa dawati la mwisho kabisa na kwenye kona, wenyewe enzi zetu tulikuwa tunasema unakaa nyuzi 90. Katika kona hiyo ya nyuzi tisini darasani ukiingia mkono wa kushoto kama mtu akiingia kwa haraka bila ya kutazama kwa kina hatoona kitu. Au pengine mtu akitoka nje na kuigia darasani akiwa amepigwa na jua kali machoni kwa muda mrefu anaweza kuingia akafanya kituko chake, wala hawezi kutambua kuwa darasani humo kuna mtu.” Mwanakwetu anasimulia.

 

 

 

Basi alikaa humo darasani akiwa anajisomea taratibu na hakuwa na ili wala lile. Gafla akasikia hatua za watu ko ko ko ko…hatua zao zikisikika, mara akasikia tii mizigo ikishushwa, akiwa ameyatoa macho yake aliona wanaingia katika darasa hilo watu kadhaa wenye mizigo na mtu mwingine akisema wekeni mizigo yenu hapa hapa. Kweli mizigo hiyo ikatuliwa chini katika mlango pembeni ili mtu akipita kwa nje asiwaone kama kuna watu darasa. Wakaambiwa chuchumaeni, kweli ndugu hawa walikuwa watiifu sana walifanya hivyo.

Mwanakwetu alipoziona hizo harakati alijua hapa pana jambo si bure, alishituka lakini akawa kimya kabisa. “Haya hapa kila mmoja anatakiwa kutoa shilingi hamsini hamsini, maana nyinyi mmezidi sana kila siku na tumewaambia muwache haya mambo yenu lakini bado.” Alisema mtu mmoja ambaye mwanakwetu hakuweza kumuona vizuri lakini mwili wake ulikuwa nusu ndani ya darasa na nusu nje ya darasa mlangoni. Basi wale ndugu waliokuwa wamechuchumaa walichangishana kimya kimya huku pesa zingine  za sarafu zikianguka chini.

Hapo darasani palikuwa kimya bali kwa mbali zilisikika sauti za ndege aina ya sholwe ambao wanapenda kujenga katika majengo za serikali tu mithili ya walinzi wa kudumu wa kujitolea wa majengo hayo. Jamaa hawajamjuona mwanakwetu huku yeye akiwa mtulivu na akifuatilia kinachoendelea mbele ya darasa, aliendelea kutazama sinema hiyo ya bure, akawaona watu kadhaa ambao kwa hakika wao walikuwa maarufu sana kwa kuuza gongo Kijijini Mbagala hasa Mbagala 77 mtaani kwao akiwamo mama Mwarongo Chongo. Pesa hiyo ilikusanywa vizuri kabla hawajamaliza mwanakwetu akawatazama vizuri jamaa hawa aliwabaini kamani askari polisi na mgambo hivi. Basi wakakabidhiwa wale jamaa pesa yao na wale waliokuwa wamechuchumaa wakaruhusiwa.

“Kimbieni haraka, hakuna kugeuka nyuma na hatutaki kuwaona hapa.”Hawa jamaa ambao mwanakwetu alidhani askari hawatambui kuwa bingwa yupo ndani ya darasa na bingwa huyu(mwanakwetu) anayafuatilia hayo manjonja (maigizo ) kwa kina.

Walibaki hawa jamaa kama sita, jamaa hawa kwa kuwatazama mwanakwetu alibaini kuwa wanatokea Kituo cha Polisi Mbagala Maturubai na namna walivyokuwa wakiongea na kuitana majina lakini sura hakuziona vizuri wakitanguliza neno afande.“Haya jamani haraka haraka, hapa kila mmoja hamsini hamsini.” Yule mmoja ambaye nadhani alikuwa mkubwa wao alisema hivyo.Wakati mgao huo ukiendelea kwa amani na utulivu darasani hapo na kama unavyotambua pesa ni uchawi wa kizungu na mwanakwetu akaamua kuwatia adabu hawa jamaa.

 “Ahhh jamani kwanini mnagawana peke yenu? Na mimi nataka mgao huo.”

Kumbuka hawa askari wako kwenye oparesheni mwanakwetu akasema kwa nguvu huku akipanda juu ya madawati.Mwanakwetu alisema kwa sauti ya juu, sauti ya kubongo jamaa wakapatwa taharuki, jamaa wana silaha wakataka kukimbia, mwanakwetu akawaambia hakuna kukimbia mtu yoyote ninawafahamu wote, nawajua wote hadi majumbani kwenu. Duu jamaa wakawa wapole jamaa walishituka sana huku vijasho vikiwatoka.

“Kumbe eeh humu ndani kumbe kuna mtu, wewe bwana mdogo vipi? Huyu bwana mdogo wa chipukuzi wa CCM huyu, wanafunzi wa mwalimu Mienjwa hawa.” Jamaa wakawa wanasema.Mwanakwetu akawa mkali akasisitiza anautaka mgao. Jamaa waliposikia maneno ya asakari mwenzao kuwa mwanakwetu ni miongoni wa chipukizi wa chama anaweza akawashiriki mbele kwa mbele maafande wakawa wapole sana. Mwanakwetu kumbuka jupo juu ya dawati akashuka.Maana Sasa walishatambua kuwa yote waliyoyafanya mwanakwetu kayaona na kwa umri mwanakwetu na inteligesia aliyotumia jamii jamaa wakahisi si bure huyu dogo kuna kitu.

Msomaji wangu tilia maanani silaha za mwanakwetu moja kumbuka nje ya darasa hilo mwanakwetu ni mwenyeji sana kwa maana uwanjani wako makaka wakubwa wengi kama akina Mwinjuma Kondo na Akina Linje wakicheza mpira. Wasingekubali mdogo wao aonewe lazima shauri hilo lingekwisha kwa amani bado kando uanafunzi wa chipukizi, alafu hawa akina Linje baba yao zamani alikuwa afande mkubwa.

Saikolojia ya binadmu ni kuwa anapofanya jambo lake baya akiwa anajua kuwa hakuna mtu anayemuona anakuwa na amani sana lakini jamaa hawa walikosa amani na kujiamini kabisa kwa kuwa kila kitu kilishuhudia. Basi afande mmojawapo nadhani alikuwa mkubwa akawaambia mpeni dogo shilingi 25. Jamaa wakasalimu amri, Ilikusanywa pesa hiyo harakaharaka kutoka kwa kila askari akakabidhiwa. Jamaa wakaenda zao. Hiyo shilingi 25 ilikuwa nyingi sana maana nauli ya basi kwa wanafunzi ilikuwa shilingi 1 na wakubwa walikuwa wakilipa kati ya shiilingi 7-10 kwa safari ya kutoka Mbagala hadi Temeke.

Akaweka pesa yake mfukoni, wakati huo TAKURU wala TAKUKURU hazikuwepo, wala wazo la Jaji Joseph Warioba la kuundwa kwa chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa halijatolewa. Maana mwanakwetu anakumbuka wazo hilo alilitoa Mzee Warioba katika Tume yake ya Rushwa ya mwaka 1997 ambapo alipewa kazi hiyo na Rais wa Awamu ya Tatu hayati Benjamin Mkapa. Akiwa na shilingi zake 25 mfukoni, je abaki aendelee na masomo au aondoke? Alijiuliza maswali mengi, je hawa jamaa wakirudi wakinibambikia kesi ya kukutwa na bangi nitapona? Maana uwongo wa Askari si Ukweli wa Raia. Akafungasha madaftari yake, akatoka nje na kutazama mazoezi ya mpira kiwanjani na kurudi nyumbani kwao mara moja.

Wale askari baada ya tukio hilo walikuwa rafiki mno wa mwanakwetu. Msomaiji wangu tambua kuwa rushwa inamshawishi kila anayeona tukio hilo kuutaka mgao na ndiyo maana Jaji Warioba alipewa kazi hiyo na Mzee Mkapa, kumbuka kwa sasa hilo usijaribu maana TAKUKURU wapo kazini na sheria wanayo,  kwa  sasa usiombe na wala usitake mgao.

Kwa heri.

 makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

0/Post a Comment/Comments