Adeladius Makwega-MARA
Mapema Agosti 16, 2025 Mhe Juma Chikoka, Mkuu wa Wilaya ya Musoma aliupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Bunda ambapo ulikimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda siku iliyotangulia yaani Augusti 15, 2025 na kukabidhiwa Musoma kwa heshima zote na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe Enock Kaminyonge.
Awali Gari walilopanda Wanahabari lilitoka Bunda Mjini kuelekea Musoma Vijijini na majira ya asubuhi kufika salaama, kisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka wa 2025 ndugu Ismail Ali Ussi kuanza ukaguzi wa miradi na kuifungua.
Kwa hakika Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, kwa mwaka wa 2025, Ndugu Ussi alimpongeza Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Musoma, Juma Miraji Kapiteni kwa namna anavyofanya kazi ya kuhamasisha vijana kupewa mafunzo ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa kuundwa kwa Kilabu za Rushwa Mashuleni, huku akihimiza Kilabu zote za Rushwa Mashuleni nchini Tanzania zitumike kujenga maelewano katika jamii yaani baina ya Wanafunzi , Walimu na Wazazi.
Akilinadi hili;
“Nimefurahishwa sana na namna vijana wetu wanavojifunza vita hivi dhidi ya adui rushwa , wakiwa wadogo, hawa ni askari wetu katika mapambano haya, hivyo basi lazima vijana hawa tuwape ushirikiano mkubwa, kama anavyofanya Kamanda Kapiteni lakini na wanafunzi wetu mashuleni waitumie fursa hii kuleta maelewano zaidi na siyo migogoro katika jamii yetu.”
Wakati Kiongozi huyu wa Mwenge wa Uhuru anaongea, simu ya Mwanakwetu ikapokea ujumbe huu;
“Usitoe rushwa ili ipige au usipige kura, piga 113 kutoa taarifa za rushwa.”
Ujumbe huu ulimkumbusha Mwanakwetu kuwa tangu kuanza kwa Kura za Maoni katika Vyama vya Siasa ili kupata Wagombea wa Udiwani , Ubunge na hata Urais , Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (TAKUKURU) imekuwa ikiwatumia ujumbe kwenye simu zao wananchi mbalimbali juu ya kuzuia na kupambana na Rushwa. Haya yakiwa sehemu ya mapambano dhidi ya adui rushwa. Mwanakwetu alibaki na swali je TAKUKURU kwa kufanya hivyo inatosha? Kulijibu swali hili nitaandika makala nyingine maana leo hii siyo wakati sahihi.
Sambamba na hili Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kwa mwaka wa 2025 Ndugu Ussi alisisitiza pia maelewano mazuri baina ya wananchi na watumishi wa umma wakiwamo walimu , madaktari na watumishi wengine, akisema kazi hizi ni ngumu, zinahitaji moyo mwema wa mtumishi binafsi, sisi wananchi hatuwezi kuzifanya kazi hizi zote, ndiyo maana watumishi wa umma wanakuja kwenu, hivyo basi tunapaswa kuishi kidugu, kwa maelewano ili watumishi wa umma waendelee kutoa huduma kwa jami pia ninawaomba mfahamu kuwa mnapaswa kuyatumia vizuri majengo ya taasisi za umma.
Haya yanasemwa na Kiongozi huyu wa Mwenge wa Uhuru kwa nyakati tofauti wakati ukikimbizwa katika Halmashauri ya Musoma Vijijini, huku miradi yote iliyopitiwa yenye thamani ya mabilioni kadhaa kukaguliwa na kufunguliwa bila dosari.
Akisoma Risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Tawala wa Wilaya hii Ndugu Ally Mwendo alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ina watu wanaokaribia 290,000, huku hali ya Mapato ya Ndani ilikuwa kama ifuatavyo.
“Kwa mwaka wa fedha wa 2024/ 2025 ilipangiwa kukusanya mapato ya ndani ya karibu Shilingi Bilioni 2.3 ambapo walivuka lengo hilo kukusanya karibu shilingi Bilioni 2.6 ni sawa na asilimia 119 ya shabaha.”
Kwa hakika ndani ya Halmashauri ya Musoma Vijijini, Mwenge wa Uhuru ulipokelewa na idadi kubwa ya watu wa rika zote, huku utunzaji wa afya za binadamu na mapambano ya magonjwa kama vile UKIMWI na Malaria yakipigiwa chapuo namna sahihi ya kupambana nayo.
Akizungumza katika shughuli hii, Mkuu wa Wilaya ya Musoma , mhe Juma Chikoka alimshukuru Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ndugu Ussi kwa kuifungua miradi yote ikiwamo Kiwanda cha Kuchangua Dhahabu, Shule za Msingi na Sekondari, Mradi wa Vizimba Vya ufugaji wa Samaki katika Ziwa Victoria na Vituo vya Afya pamoja na ufunguaji wa Kilabu ya Mazingira na ya Mapambano dhidi ya RUSHWA.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika siku hii ilikuwa nzuri kidogo na la kwanza wananchi wengi walijitokeza kwa vijiji vyote ambavyo Mwenge wa Uhuru ulipita na kulipambwa na idadi kubwa ya watu wa rika zote watoto na vijana wengi ikiwa jamii inayozaliana vizuri, jambo la pili lililomvutia Mwanakwetu ni miradi karibu yote ilikuwa mizuri sana na jambo la tatu ambalo lilimvutia Mwanakwetu mno kulikuwa na vijana watatu wakiume rika kama ya miaka 25-30 wakati Mwenge wa Uhuru ndiyo unapokelewa asubuhi eneo la Halmashauri ya Musoma Vijijini. Wakimbiza Mwenge wakawa wanatajwa majina yao mmoja mmoja wanavuka upande alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda na wanaenda alipo Mkuu wa Wilaya ya Musoma.
Mwanakwetu nipo upande wa Wilaya ya Musoma, vijana hawa kiume wakawa wanasema maneno haya,
“Katika hawa mabinti wanaokimbiza Mwenge wa Uhuru Wewe Unamkubali nani?”
Mwanakwetu akacheka, kisha akasema moyoni, hawa vijana vipi? Jamaa akajibu kuwa ngoja waitwe wote, kisha atamwambia anamkubali nani.
Gafla Mkuu wa Wilaya ya Bunda akasema maneno haya,
“Huyu anaitwa…ni mkimbiza Mwenge anayetokoa Mkoa wa Shinyanga.”
Bwana Mdogo aliyeulizwa swali akajibu ,
“Eheee ebu nimtazame kwa umakini mkubwa.moja mbili tatu, ahaa kaka mimi ninamkubali huyu Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Binti Kutoka Shinyanga huyu anatakiwa abaki Musoma nikamkabidhi vizimba vya kufugia samaki.”
Mwanakwetu nimejikausha mno kama siwasikiliza lakini kumbe akili yangu yote 100 kwa 100 ilikuwa kwao nikacheka sana moyo na ndiyo maana nimeamua kisa hiki kiwepo katika haya makala .Nikawa najiuliza hivi hawa vijana wakinisikia nacheka kisha wakiniuliuza Mzee Wewe unamkubali nani? Nitajibu nini? Nikasema Jibu ninalo Namkubali Binti Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kutoka Shinyanga.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Namkubali Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Binti Kutoka Shinyanga.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment