MAZINGIRA HUJILINDA YENYEWE

 

Adeladius Makwega-Musoma MARA.

Ni majira ya asubuhi ya Agosti Mosi, 2025 mwezi mpya umeanza, Mji wa Musoma ukiwa na hali ya utulivu sana, baridi kwa mbali, jua kwa mbali , huku watumishi wa umma ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakiendelea na majukumu yao.

Nayeye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, yu kazini na mara anawapokea wageni wawili, huku akizungumza nao na anahimiza wananchi wa Mkoa wa Mara kulima kilimo cha zao la alizeti maana kina faida mno kwa jamii ya Watanzania.

Kulingana na Jarida la Wizara ya Kilimo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye anuani –Mwongozo na Kalenda Ya Kilimo Bora cha Alizeti lililotayarishwa na idara ya Maendeleo ya Mazao la Januari , 2022 sura ya kwanza ukurasa wa awali linasema haya;

“Alizeti ni zao lenye thamani kiuchumi na lishe kwa binadamu na wanyama. Zao hili hutoa mbegu zenye thamani zenye vitamin A, B, E, K na madini ya Zinki, Kaisiam, Patasiam, Magneziam na madini ya chuma.

Alzieti hutoa mafuta ya kula, mashudu ya chakula cha mifugo na maua yake hutumika kama pambo na kutoa chavua kwa ajili ya nyuki ili kutengeneza asali, matumizi mengine ya alizeti ni kutengeneza vipodozi , madawa na utengenezaji wa nishati mbadala.”

Haya pia yakiungwa mkono na Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ndugu  Lepapa Ole Mollel mbele ya MwAnAkWeTu Agosti Mosi, 2025.

 

Kumbuka Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi yu kazini anazungumzana na mdau wa kilimo cha alizeti hapa Mkoani Mara Profesa Charles Majige, akasema haya;

“Natambua kuwa kilimo cha zao la alizeti kinatupatia faida tele lakini pia kilimo cha alizeti kinasaidia kuzuia tembo kufanya uharibifu jirani na makazi ya binadamu.”

Kanali Mtambi akiwaomba wananchi wa mkoa huu kuwaunga mkono wawekezaji wanapofika kuwekeza katika maeneo yao;

“Baadhi ya maeneo yetu, mtu akienda kuwekeza, madai yanakuwa huyu ni mtia nia, siyo kila anayewekeza ni mtia nia wengi wetu wanataka kuzikomboa jamii zao walipozaliwa.”

Akizungumza kwa msisitizo mkubwa, Kanali Mtambi alisema kuwa Mkoa wa Mara una wanyama wa kila aina, wengi wao wakipatikana katika Mbuga ya Serengeti, hifadhi ya Ikorongo na Guremeti hasa tembo;

“Mkoa huu una KM za Mraba 30,150 ambapo KM za Mraba 10,942 ni Ziwa Victoria likichukua asilimia 36 na aslimia 64 ni nchi kavu ikichukua KM za Mraba 19,000 na asilimia 49 ya nchi kavu ndiyo imebeba Mbuga ya Serengeti na hifadhi hizo mbili zenye wanyama tele.”

Akifafanua zaidi juu ya zao hili Kanali Mtambi alisema,

“Zao la Alizeti mara nyingi hulimwa msimu wa mvua za vuli katika kipindi ya mwezi Oktoba hadi Disemba ambapo maeneo yanayopata mvua hizi ni pamoja na Nyanda za Juu Kaskazini na Mashariki ambapo ni mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimajaro  Tanga na maeneo ya Kaskazini ya Mkoa wa Morogoro. Pia Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Baadhi ya maeneo ya Simiyu na mkoa wetu wa MARA.”

Kanali Mtambi alipigilia msumari wake wa mwisho kwa kusema kuwa mazingira yetu kama yakitunzwa vizuri mara zote yamekuwa na desturi ya kujilinda yenyewe, jukumu la binadamu anatakiwa kuiacha mimea katika uoto wake wa asili, ikue na ndiyo maana ziko aina kadhaa za matunda ya asili msituni sasa zinapotea, lazima tulinde mazingiya yetu kwa mbinu za asili ili matunda ya asili ambayo ni chakula na tiba yaendelee kuliwa na vizazi vyetu vijavyo.


 

Mara baada ya mazungumzo haya Mkuu wa Mkoa wa Mara aliagana na Profesa Majige na mwandishi wa makala haya kwenda kuyatayarisha makala haya.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kumbuka kupanda alizeti jirani na makazi yako, maana tembo anahofia alizeti kwani anajua nyuki huwa kando ya zao hili. Pia alizeti ni chanzo kikubwa cha vitamini kadhaa iwe kwa mafuta na hata asali inayopatikana katika nyuki.


 

Mwanakwetu upo? Kumbuka

“Mazingira hujilinda Yenyewe.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 



















 

0/Post a Comment/Comments