ATI WAMEMROGA MKIMBIZA MWENGE

Adeladius Makwega Bunda MARA

Ni majira ya asubuhi ya Agosti 15, 2025. Mwanakwetu mbele na kikosi cha wanahabari wanaokaribia dazeni moja kutoka Mkoani Mara, wamelala Wilayani Bunda, lengo kuwahi kuupokea Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2025, maana sasa ulikuwa unapiga hodi Mkoani Mara, huku Mratibu wa Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Mara ni ndugu Fidel Balagaye na Msaidizi wake ni Bi Rebecca Mdodo.

Hali ya hewa ilikuwa ya joto usiku kucha wa kuamkia siku hii, lakini kulipokucha tu hali hii ilibadilika katika Mji huu ambapo Wilaya yake inayoitwa BUNDA Iliyoanzishwa mwaka 1978, ikimegwa kutoka Wilaya ya Serengeti.

Wilaya hii iliyopokea Mwenge kutoka Simiyu, mpaka leo hii kiongozi mkubwa mzaliwa wake ni Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na wa Makamu wa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyezaliwa katika Kijiji cha Nyamshwa.

Mwanakwetu yu Bunda alivaa sweta lake la rangi ya samawati na kuingia kazini. Mara Mwenge wa uhuru uliingia naye Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bi Prisca Kayombo alitoa maelezo ya utangulizi huku kukiwa na vijembe vingi kutoka kwa waendesha ratiba wa pande zote mbili.

“Mwenge wetu ulikimbizwa katika halmashauri sita, huku miradi 41 ikikaguliwa na kuzinduliwa.”

Wakati Bi Kayombo anaongea, Mwanakwetu alikutana na rafiki yake kutoka Simiyu, Mwanahabari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Pasco Michael na alimdokeza haya;

“Wakimbiza Mwenge wa mwaka huu ni wachapa kazi, waungwana, wakiwa ni vijana wanaojifunza mambo kwa haraka katika mazingira mageni.”

Mbio hizo kabla kipenga kulia na kukimbizwa, Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Mwalimu Gerald Msabila Kusaya aliupokea kwa heshima zote, akisema kuwa anawakaribisha wakimbiza Mwenge wa Uhuru mkoani Mara maana Mara ndipo alipozaliwa muasisi wa mwenge huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kazi ikaaanza kwa kasi ndani ya Wilaya ya Bunda ilibainika kuwa Kiwango Cha Maambukizi ya Virusi vya HIV na UKIMWI katika Wilaya ya Bunda kimepungua kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia 1.5 , hizo zikiwa jitahada za pamoja kwa ushirikiano thabiti, usiolelega baina wa Wananchi wa Wilaya ya Bunda na Serikali yao inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi(CCM).


 

Haya yakisomwa katika Risala ya Utii Kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Tawala Wilaya ya Bunda Ndugu Salum Mtelela, mbele ya Mwenge wa Uhuru wa mwaka wa 2025, mara baada ya kufungua na kuizindua miradi 8 yenye ubora mkubwa, yenye thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni Tatu na Ushehe, mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, ndugu Ismail Ali Ussi. Akizungumza miradini, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Ussi alisema miradi yote ya Halmashauri ya Bunda imejengwa kwa ubora wake, kwa kuzingatia vigezo vya serikali na wana Bunda Waendelee na Moyo huo huo na watembee kifua mbele.

“Huo ubora wa miradi yenu, ndiyo shabaha ya serikali yetu, jamani endeleeni kufanya kazi kwa bidii.”

Akizungumza karibu katika maeneo yote yenye miradi yalitotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwka huu, Ndugu Ussi alisisitiza suala la afya kwa kila Mtanzania ajitahidi kufuata kanuni bora za afya na maelekezo ya matabibu ili kila mmoja ajikite kufanya kazi zake za maendeleo.

“Tujikinge na VVU na UKIMWI na ndiyo maana kumekuwa na semina na mafunzo kadhaa kwa shule 37 na pia kutoa elimu kwa kutumia video, sinema na vipeperushi, huku kwa sasa kukiwa na mabanda ya kutoa ushauri wa afya ikiwamo upimaji magonjwa mbalimbali .”

Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Kaminyonge akizungumzia takwimu za upimaji wa magonjwa haya alisisitiza kuwa zoezi la Upimaji wa VVU na UKIMWI kwa hiari katika Mbio hizi za Mwenge wa uhuru linafanyika, hivyo basi mara baada ya Mwenge kwenda zake Wilaya nyingine, wilaya yake watakuwa na takwimu juu ya muitikio wa wananchi katika zoezi hili. Katika Halmashauri ya Mji wa Bunda Miradi ya Elimu, Afya, Maji, Mapambano dhidi ya Rushwa na Kituo Kikubwa cha Mafuta cha NM kilifunguliwa.  Kituo hiki cha mafuta kilichozinduliwa kinaufanya Mji wa Bunda sasa kuwa na kituo kikubwa na cha kisasa cha uuzaji wa mafuta kadhaa ya nishati na kikiwa kituo mkombozi kwa vyombo vya moto vinavyoingia na kutoka Mkoani Mara.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu akiwa katika mapokezi wa Mwenge huu wa Uhuru hapa Bunda alivutiwa na mambo makubwa matatu; kwanza miradi mizuri ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, Pili wakati Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ndugu Ussi anawaaga Viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Ndugu Ussi aliwasifia mno Wakurugenzi wa Halmashauri sita za Mkoa wa Simiyu na aliwaita na kuwamwagia sifa kemkem, sifa lukuki, sifa kedekede na kuwapongeza kwa kazi nzuri. Yakiwa mazungumzo ya ndugu Ussi yanaendelea, mdau mmoja mbele ya Mwanakwetu ambaye alikuwa kama Chifu alisema maneno haya

“Ndugu Ismail Ali Ussi, hao Wakurugenzi wa Simiyu watakuwa wamekuroga na ndiyo maana unawasifia mno , Simiyu mabingwa wa kufuga FISI WATU wa Ulozi Baba Umerogwa”

Mara baada ya ndugu Ussi kutoa sifa kedekede kwa Wakurugenzi wa Simiyu, pia Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru aliimba Wimbo wa Taarabu kutoka Zanzibar unaoitwa YALAIT wa Bibi  Kidude na Seheb El Arry. Jamaa kama Chifu kando ya Mwanakwetu kwanza akacheka  na kisa kusema ;

“Lo Salale! Wakurugenzi Simiyu wameshafundishwa Ulozi wa Fisi na mwaka huu Wamemroga Mkimbiza Mwenge, lazima Mkimbiza Mwenge Aje Aaguliwe Hapa Mkoani Mara.”

Mwanakwetu alicheka mno kutokana na vijembe hivyo baina ya Simiyu na Mara vya Agosti 15, 2025 na baadaye Mwanakwetu kuamua kuviweka visa vyote katika makala haya.

Mwanakwetu upo? Kumbuka

“Ati Wakurugenzi Simiyu Wamroga Mkimbiza Mwenge.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257















































0/Post a Comment/Comments