WALIDOEA OFISI YA MKUU WA WILAYA

 

 
Adeladius Makwega-Musoma MARA

Tanzania inayo mikoa mingi, swali kwako wewe unayeyasoma makala haya ambaye ni Mtanzania, je unalifahamu jengo la Ofisi ya Mkoa wako lilipo? Kama unalifahamu jengo hilo kwa kuliona tu hilo ni jambo jema , lakini kuna chochote cha ziada unachokifhamu?

Nakuuma sikio msomaji wangu kuwa Mwanakwetu analifahamu vizuri jengo la Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuliona na historia yake maana ndiyo mkoa aliyokulia na kulelewa.Siku nyingine atakusimulia juu ya jengo hili la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam lakini siku ya leo siyo mada ya Mwanakwetu.

Chamno tangu Mwanakwetu awepo hapa Mkoani Mara amekuwa akijiuliza maswali mengi juu ya Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara,huku Mwanakwetu akisaka majibu huku na kule.

“Jengo hili lipo upenuni mwa Mlima Mkendo  na karibu na Mwalo wa Ziwa Victoria uliopo jirani ziwa hili na jina maarufu ni Lakeside.”

Alone Oddoa mkazi wa Mjini Musoma alipoulizwa aliyasema ;

“Mkoa wa Mara ulianzishwa rasmi mwaka 1959 ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa kwanza Mhe Theodore Msonge na aliifanya kazi hiyo hadi mwaka 1962. Simulizi ndani ya Mji wa Musoma zinadai kuwa Mhe. Msonge alitumia jengo la Mkuu wa Wilaya ya Musoma ambalo lilikuwepo kabla ya kujengwa Ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Mara. Mwaka 1963 alichaguliwa Mkuu wa mkoa Mpya ambaye alikuwa mhe Richard Wambura aliyeifanya kazi hiyo hadi mwaka 1963. Huku jengo la Mkuu wa Wilaya ya Musoma likitumika. Mwaka 1963 alichaguliwa Mhe John Samweli Malecela ambaye aliifanya kazi hii hadi mwaka 1965 na baadaye kuchaguliwa Mhe. Osward Mang’ombe tangu mwaka 1965 hadi mwaka 1966, huku kipindi chote hiki jengo la Mkuu wa Wilaya ya Musomo likiokoa jahazi. Mwaka 1966 hadi mwaka 1967 Mhe. Samwel Luangisha aliifanya kazi hii ya Mkuu wa Mkoa na baadaye kuchaguliwa Mhe Acland Mhina ambaye aliifanya kazi hii kwa muda mrefu tangu mwaka 1967 hadi mwaka 1975.”

Taarifa rasmi zinadokeza kuwa,Februari 19, 1968 Jengo la Mkuu wa Mkoa wa Mara lilikamilika na ndipo Mhe Acland Mhina Msambaa kutoka Tanga alihamia katika jengo hili baada ya kufunguliwa rasmi na Waziri wa Afya na Nyumba mhe A.K.E. Shaba.

Kwa hesabu ya namba jengo hili hadi mwaka wa 2025 lina miaka 57 na mwaka 2028 litatimiza miaka 60 lakini msomaji wangu hii miaka iwe 57 au 60 ina itilafu kidogo kwa jicho la Mwanakwetu maana jngo hili limejengwa mara mbili.

 

Kwa mujibu wa wenyeji wa Mji wa Musoma akiwamo Mzee Aloyce Mwitta Chacha mwalimu mstaafu, mkazi wa Majita Road-Musoma anasema haya,

 

 

“Jengo la awali limekamilika mwaka 1968 lakini jengo hilo liliongezewa jengo lingine la pili na kukamilika mwaka 2006 na uzinduzi wake kufanywa na Rais wa awamu ya Nne Mhe.Jakaya Kikwete, huku mkoa wa Mara ukiongozwa na Mhe .Isidory Shirima wakati huo , Rais Kikwete ambaye alikuja mkoani Mara kwa ziara ya Kiserikali mwanzoni mwa utawala wake, huku akizindua ukumbi uliyokuwa sehemu ya ofisi hii.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa mujibu wa maelezo haya Mwanakwetu anasema kuwa jengo la pili la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara lililofunguliwa mwaka wa 2006 hadi mwaka 2025 lina miaka 19. Jengo la awali kwa mwaka wa 2025 lina miaka 57 na pia msomaji wangu ndiyo kusema Mkoa wa Mara kwa mwaka 2025 umetimiza miaka 66.  Kwa hiyo kwa mwaka 2025 Mkoa wa MARA 19.57.66.

Kwa hakika natambua msomaji wangu umelifahamu vizuri jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.


 

Mwanakwetu upo?

Je makala haya niyahitaje? JENGO LA OFISI YA MKOA WAKO.?Walidoea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya?Mwanakwetu anachagua walidoea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257



 














 

 

0/Post a Comment/Comments