Adeladius Makwega-Korogwe TANGA.
Mwanakwetu yu Korogwe mkoani Tanga katika mafunzo ya Programu ya Shule Bora inayodhaminiwa chini ya Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza kwa miaka sita nchini Tanzania hadi Agosti 2027 ambapo kwa sasa imebakiza miezi 27 kupunga mkono wa kwaheri kwa Watanzania.
Mwanakwetu akiwa katika mafunzo haya amebaini kuwa hadi Julai 2024 Tanzania imepokea karibu shilingi Bilioni 68.4 katika Programu hii ya Shule Bora.
Mwanakwetu ni mwingi wa simulizi ameshakusanya simulizi tele ndani ya mafunzo haya, siku ya leo anakupa moja ya simulizi hizo nayo ni hii, hapa mafunzoni amekutana na Waingereza wawili ambao wametoa mada kadhaa akiwamo Daniel Harns na Bi Pia Arriola. Ndugu Daniel Harns yeye amekuwa na mada nyingi sana huku Bi Pia Arriola ametoa mada chache mno.
Miongoni mwa mada chache alizotoa Bi Pia Arriola ilikuwa namna bora ya kutayarisha mabango, vipeperushi na matangazo kwa njia bora na za kisasa kwa kutumia Programu inayofahamika kama CANVA inayopatikana WWW.CANVA.COM.
Msomaji wangu haya mambo kwa Mwanakwetu siyo mageni maana alisoma mwaka 2006 akiwa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Shahada yake ya Kwanza ya Sanaa ya Habari miaka 20 iliyopita kwa mwaka wa 2025 ambapo wakati huo Mwanakwetu alizifanya kazi hizo kwa kutumia program tatu; Power Point, Adobe Photo Shop na Publishers ambapo mhadhari aliyemsomesha Mwanakwetu alikuwa anaitwa Dkt Albert Wanga(PHD) huku jina la kozi hii lilijulikana kama Journalism 201 Editing and Design (CORE) ambalo Mwanakwetu alifaulu kwa kupata alama ya B PLUS mwaka wa 2006 BAJ II.
“Miaka inavyosonga maboresho ya tekinolojia yanakuja, hivyo haina budi kupata mafunzo kazini ili kuboresha kazi yako na wewe mtaalamu usitupwe nje ya mchezo na ili kuendana na wakati, hivyo basi huyu Binti wa Kiingereza anakutana na Mwanakwetu anampa ujuzi uleule kwa kutumia Programu mpya naya kisasa ya CANVA Julai , 2025.”
Wakiwa katika mafunzo haya kulikuwa na mazungumzo ya kidugu ya pande mbili yaani hawa Waingereza na Mtanzania Mwanakwetu, Mwanakwetu alizungumza na David Harns pamoja na Pia na wao kwanza walimuuliza Mwanakwetu ana watoto wangapi? Mwanakwetu alijibu kuwa anawatoto nane, wakiume watano na wakike watatu. Binti Muingereza Pia akauliza majina ya watoto hao, naye Mwanakwetu akajibu,
“Winfrida (22), Evona(20), Francis (17), Albert(15), Josephy(13), Joshua(10), Adrian(7) na Colleta(5).”
Pia akacheka sana huku akisema Mwanakwetu is a father of the Biggest family. Mwanakwetu akamjibu binti huyu Mwingereza kuwa ni kweli na hiyo sentensi yake ni sehemu ya wimbo wa mkongwe Michael Jackson.
Hapo hapo David akasema yeye ana mtoto mmoja, huku Pia akijibu kuwa yeye ameolewa akilingishia pete yake ya ndoa lakini akasema hadi sasa bado hajaamua kuzaaa.
Mwanakwetu akawacheka sana hawa Waingereza huku akisema,
“Pia ungekuwa Mtanzania kama umeolewa mwaka wa kwanza unapita haujazaa, mwaka wa pili haujazaa lazima ungekuwa umeshapigwa talaka, lakini nakuomba ukirudi kwenu Uingereza ukazae mapema, bila shaka umekutana na Mwanakwetu ili akukumbushe kuzaa maana pengine tumbo lako limebeba Waziri Mkuu wa Uingereza wa miaka ijayo.”
Hawa Waingereza walicheka sana huku wakisema tulidhani kuwa wewe hauongei kumbe ni muongeaji mzuri! Hapa tunastaajabu.
Kweli mazungumzo haya yalipokamilika hiyo ilikuwa Julai 7 muda mchana wakatoka kwenda kula chakula cha mchana.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika idadi kubwa ya watu katika ngazi ya familia na hata ngazi ya taifa inayo faida tele na hasara zake, lakini lakini lakini kubwa kabisa taifa husika kama litatumia fursa ya wingi wa watu vizuri linakuwa na nguvu kazi ya kutosha katika uchumi wake, lakini watu wengi wanaweza pia kusaidia kuwa na ubunifu mkubwa wa mambo kwa namna wanavyotatuliwa kutokana na changamoto zao, mathalani mataifa kama India, Indonesia na China idadi ya watu inawasaidia sana kwa sasa na wanakwenda mbali. Kinyume chake kukikosekana umakini, idadi hii ya watu inaweza kuwa ni bomu kwa ngazi ya familia na hata ngazi ya taifa, hapa umakini unahitajika sana.
Haya msomaji wangu ni mambo ya Korogwe katika mafunzo ya Programu ya Shule Bora nchini Tanzania.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Wewe Mwingereza Ungekuwa Mwanamke wa Kitanzania Ungeshapigwa Talaka.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment