Adeladius Makwega –Tarime MARA
“FEASSSA ni mashindano ya Shule za Sekondari na Msingi Afrika ya Masharatiki sasa hivi yanafanyika Kakamega nchini Kenya, Timu yetu ya Tanznaia inaweka kambi Wilayani Tarime Mkoani Mara.
Hivi punde wamefika viongozi wa timu hii ya Tanzania wamekagua hali ya maeneo yote watakayoweka kambi ikiwamo malazi na viwanja vya kufanyia mazoezi.
Shabaha ni waweke kambi jirani na eneo ambalo mashindano haya yanafanyika maana kutoka Tarime Tanzania hadi Kakamega nchini Kenya ni umbali kama wa KM 200 . Kwa hiyo mkoa wa Mara unataraji kupokera ugeni huo wa kitaifa wanafunzi wanamichezo 500 ma walimu 132 jumla kuu ikiwa watu 632, wakatakaa Wilayani Tarime katika mabweni ya Chuo cha Ualimu Tarime , Tarime Sekondari na Tagota.
Wametudokeza kuwa watawasili mapema Agosti 2 na kuondoka mapema Agost 12, 2025 kuelekea huko Kakamega.”
Haya yakiwa maelezo katika Kikao cha Alhamisi Julai 17, 2025 cha Utawala cha Mkoa wa Mara ambapo yanatolewa na Afisa Elimu Mkoa wa Mara mwalimu Makwasa Bulega juu ya maandalizi ya mashindano haya ambapo timu ya Tanzania inakita kambi kwa siku karibu dazeni moja hapa mkoani Mara.
Katika kufahamu zaidi juu ya mashindano haya ya FEASSsA kwa msomaji wa Mwanakwetu, hapa hapa alimtafutwa Mwalimu Isdory Francis ambaye ni mwalimu kutoka Shule ya Moja ya Msingi , mkoani Simiyu nchini Tanzania ambaye ana Astashahada ya Ualimu , ana Stashahada ya Mazoezi ya Viungo na pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Michezo mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Kampala nchini Uganda;
“Mashindano haya yanahusisha watoto na wanafunzi wetu kutoka Afrika Mashariki kwa michezo kadhaa. Mchezo ambao haupo Mpira wa Mikono hasa kwa shule za msingi.
Ushiriki wa Tanzania katika michezo hii unafanyika kila mara lakini katika hoja hii si kushiriki tu, hoja ni baada ya mashindano haya kumalizika je huku kwetu kinafanyika kipi na kwa mataifa ya wenzetu linafanyiki lipi? Kwa wenzetu wanakuwa na ligi baada ya mashindano haya hapa Tanzania kinyume chake tunawaacha vijana hawa hadi wanapotea tu mitaani, mtindo ni ule ule msimu ukifika-Tunaenda , Tunashiriki na Tunarudi.”
Mwalimu Isidory Francis kidogo sana anazo chembembe za matumaini;
“Kidogo kuna muelekeo maana hivi punde imeisha ligi ya mpira wa kikapu na naona mpira wa hata Voleball Taifa Cup ambapo Timu ya Mtwara imeshiriki mashindano yaliyokwisha lakinia vipi kwa michezo mingine? Ili tuone wanatumia michezo hiyo kung’ara huku tuone hawa wanamichezo wananunuliwa kama ilivyo kwa soka na hata walimu wanaopati timu za kufundisha michezo hiyo hata nje ya nchi.”
Msomaji wangu bila shaka sasa unamuelewa vizuri mwalimu Isidory Francis akichambua kwa kina haya mashindano aya FEASSSA, kumbuka huyu siyo mchambuzi wa kujitengeneza na kuongea ongea tu bali huyu ni mwalimu kwa taalumu, anayo pia Stashahada ya Mazoezi ya Viungo na sasa anaitafuta Shahada yake ya Michezo.
Kwa hakika kama unamuhitaji kumpata msomi huyu wa michezo nchini Tanznaia unaweza kuwasiliana na Mkurugenzi wa Miundo Mbinu ya Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo ndugu Alex Mkenyenge na anatakupatia mawasiliano yake kijana huyu Mtanzania kutoka Mkoani Simiyu.
Mwanakwetu alizungumza mengi na mtaalamu huyu wa michezo ambapo kama yote akiyaweka katika makala haya inaweza kumchosha msomaji wake lakini kubwa na mwisho aliloliuliza ni juu ya timu hii ya Tanzania inapata faida gani kuweka kambi Mkoani Mara jirani na eneo ambalo michezo hii inafanyika? Kwa nini wasifunge safari moja kwa moja hadi huko Kakamega nchini Kenya?
“Unajua kubwa zaidi ni kuweza kuizoea hali ya hewa, lakini umuhimu wa kufanya mazoezi eneo hilo inakupa mazoea, hata nyumbani kwako kitanda chako kikiondolewa katika chumba chako na kuwekwa chumba kingine, haya yatakuwa ni mazingira magumu kwako wewe kulala yatakuwa mageni mno, kwa hiyo ili kuzoea mazingira mageni kuna umuhimu mkubwa wa kufanya mazoezi jirani na uwanja wa mashindano husika kabla ya mashindano.”
Kwa hakika Mwanakwetu alimaliza kuongea na mtaalamu huyu mwalimu Isidory Francis na kuagana naye ambaye kwa hakika mtaalamu huyu ameisaidia sana kuyajenga makala haya ya michezo ya siku ya leo.
Mwanakwetu kwa makala haya anakitakia heri ya maandalizi mema ya mashindanoa haya ya FEASSSA kikosi hiki cha Tanzania huku akiwakaribisha mkoani Mara na makala haya yatumike kama chachu ya kufanya vizuri kwa timu hii ya Tanzania.
Mwisho Mwanakwetu anakitakia safari njema kikosi hili kuelekea huko Kakamega wakati ukifika. Kwenu wale mnaosimamia michezo muyachukue makala haya kama hamira ili michezo yetu ifanye vizuri nchni Tanzania, lakini watoto wetu wakumbushwe kushiriki michezo na wasisahau kusoma kwa bidiii maana kusoma ndilo lengo la msingi na michezo ifanikishe masomo.
Mwanakwetu upo? Kumbuka
“Tunaenda, Tunashiriki na Tunarudi.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment