SHULE BORA YA MSINGI YA NEW KOROGWE

 


Adeladius Makwega-Korogwe TANGA

Ni majira ya asubuhi ya Julai 10, 2025 Maafisa Habari wa Mikoa,Wizara ya Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR –TAMISEMI), Wizara ya Elimu, na Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu wakiwa wameweka kambi kwa muda wa siku tano mjini Korogwe kwa ajili ya mafunzo ya kujengeweza uwezo yanayoendeshwa na Programu ya Shule Bora,Programu ambayo inafadhiliwa na Serikali ya Uingereza.Kundi la Maafisa Habari Ketto Mdoe, Raymond Kanyambo, John Mganga, Fransica Mselemu na Kazimbaya Makwega wanaingia katika Toyota Haice, gari maalumu chini ya rubani wao Daniel Mwambashi kueleka Shule ya Msingi New Korogwe kufanya kazi maalumu wasambaa wanaitwa NDIMA.

Kwa bahati mbaya kikosi hiki kilionewa kwa kuwa na dada mmoja tu Bi Fransica Mselemu ambaye ni Afisa Habari kutoka Makao Makuu ya nchi Dodoma, lakini kilifanya vizuri kazi yake.

Lo salale!!! kikosi kazi kinafika Shuleni ya Msingi New Korogwe ambayo zamani ilitambulika kama Shule ya Msingi Boma, ukiwa mwendo wa dakika tatu kutoka mahali yanapofanyikia mafunzo.

Shuleni hapa wanakaribishwa na mazingira mazuri, upepo mwanana na ndege wa hapa na pale, miti kila kona huku kando ya shule hii wanyama wa kufugwa wakisikika.

 



 

Mkuu wa shule hii Yusufu Madungalle anatoa neno la ukaribisho na kukieleza kikosi kazi juu ya Klabu ya Mazingira inayosimamiwa na wanafunzi wenyewe wakiwa na uongozi wao wa sasa na wa zamani.

“Mimi ni Katibu wa Klabu ya mazingira mstaafu, mabadiliko ya tabia nchi ni hali ya mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya kipindi cha miaka kati 25 na 30 na yana madhara makubwa kwa binadamu.”

Maelezo ya Abdallah Ismaili yanaonesha kuwa Shule ya Msingi New Korogwe ina uongozi bora wa mazingira kwa miaka mingi. Albert Shabani ni mwanafunzi wa shule hii na pia ni Mjumbe wa Klabu ya Mazingira shuleni hapa, anazungumza na timu ya Shule Bora akiwa amevalia kaptura ya bluu na sweta la rangi ya bendera ya Tanzania,yeye anaaamini;

“Mabadiliko ya tabia nchi yanatokana na  kuchafuliwa kwa hali ya hewa ambayo yanaharibu utando anga na hii ina madhara sana kwa kiumbe binadamu.”

Maelezo haya yanaonesha kuwa Shule ya New Korogwe hapa Mkoani Tanga ni mahiri katika mazingira, huku wakijaribu kutatua changamoto kadhaa wanazokutana nazo kwa msaada wa wadau mbalimbali,

“Unajua madarasa yetu mengi yanachangamo moja kubwa ya joto na wakati mwingine jasho linatutoka mno, tunashindwa kupumua vizuri hadi darasani kunakuwa na harufu ya kikwapa, mwalimu, akiingia anaweza kudhani wote tunanuka vikwapa, kumbe shida pengine ni mwanafunzi mmoja tu , hewa inakuwa hafifu kutokana na darasa kutokuwa na madirisha yanayopitisha hewa,na hiyo inafanya hewa kuwa finyu.”

Haya ni maelezo ya Mwasiti Adam ambayo yanatoa taswira halisi ya hali ilivyo katika shule hii, wazazi, jamiii nayo Serikali ikiingilia kati kutatua changamoto ya hali hii inayoathiri ujifunzaji kwa wanafunzi madarasani.

 

Mwalimu Madungalle anasema,

“Mradi wetu wa madarasa mawili yalianza kujengwa na wadau mbalimbali mathalani jamii yenyewe, mfuko wa jimbo karibu shilingi milioni 6 na huku Shule Bora wakichangia milioni 15 na ushee.”

Kando ya madarasa,mafundi wakiendelea na ujenzi wa madarasa mapya, mtendaji wa Kata ya Majengo Bi Salma Khalidi akisimamia zoezi hili na akitambua kinachoendelea.

“Kwa hakika sasa hata madarasa mengine ya shule zetu zote kwa mitaa mingine siyo hapa tu New Korogwe bali hata shule zingine zote tutajenga kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi, hili litasaidia wanafunzi kusoma vizuri.”

Kwa hakika Shule ya Msingi New Korogwe wataaanza kupanda miti ya matunda ambapo itasaidia zaidi kutunza mazingira,lakini pia kupatikana kwa miti ya matunda shuleni na wanafunzi watakula matunda hayo.

Baada ya kazi hii, kikosi kazi cha Shule Bora kiliingia darasa la nne kuangalia hali ya ufundishaji hapa wanakutana na mwalimu Margreth Myombo akifundisha somo la Kiswahili.

Hali ilikuwa hivyo huku darasa hili likiwa na shangwe tele.

Msomaji wangu haya yote ni ya maboresho ya Mazingira ya Kusomea hapa New Korogwe mkoani Tanga ambapo makala haya yanakamilikwa kupitia kikosi cha Shule Bora chenye wahusika hawa; Ketto Mdoe, Raymond Kanyambo, John Mganga, Fransica Mselemu na Kazimbaya Makwega

Nakutakia wakati mwema.

makwadeladius@gmail.com 

0717649257






 

 

 

0/Post a Comment/Comments