MZEGAMZEGA WA MAHINDI

 



Adeladius Makwega-MBAGALA.

Ilikuwa majira ya jioni ya siku ya katikati ya wiki, Mwanakwetu alikuwa akirudi nyumbani kwake, begi mgongoni, shingo upande, moyo mnyonge, akitafakari dunia. Akiwa njiani akaamua kupitia njia moja ambayo kuna mama mmoja mchoma mahindi mabichi, shabaha ya Mwanakwetu apite hapa ili anunue mahindi matatu mabichi, arudi nayo nyumbani kwake ayachemshe na kiwe ndiyo chakula chake cha jioni hii siku hii.

Mwanakwetu alifika kwa mama huyu wa Kijaluo, akatoa shilingi ya Kitanzania 2000/- na kumpa, kisha mama huyu kumrejeshea Mwanakwetu shilingi 500/- ya sarafu na kufungiwa mzegamzega wa mahindi haya na kisha kuanza kupiga hatua moja mbili kuelekea kupanda bodaboda.

Akiwa anakwenda zake kwake,mara akasikitia sauti inaita,

“Kaka Makwega!, Kaka Makwega! Mwanakwetu! Kazimbaya wa Mbagala Vipi? Upo huku! Tangu lini kaka upo huku?”

Mwanakwetu akacheka mno kisha kumjibu maswali haya vizuri ndugu huyu ambaye walisoma naye Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa Mwaka 2005-2008, wakati Mwanakwetu anasema Shahada ya Sanaa na Habari(BAJ) huyu ndugu alisoma shahada ya Uongozi wa Biashara(BBA).

“Makwega bado upo CCM?Au umeachana na siasa?”

Mwanakwetu akayajibu maswali haya vizuri sana. Jamaa huyu huku akicheka mno.

Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba nikueleze kwa kina juu ya ndugu huyu aliyekutana naye.

“Ndugu huyu tangu tunasoma alikuwa ni mwanachama wa CHADEMA na baadaye alirudi kwao Chalinze akawa anagombea Ubunge kupitia CHADEMA, baadaye ndugu huyu alikubwa dhoruba gani akarudi CCM na kuachana na siasa kabisa na sasa ni mtumishi wa umma katika shirika moja la umma kama Mkaguzi wa Ndani Ngazi ya Juu.”

Mazungumzo haya yalikuwa mengi, kumbuka umbali aliyokutana naye huyu ndugu ni jirani na yule mama ambapo Mwanakwetu alinunua ule Mzegamzega wa Mahindi matatu ya chakula chake cha jioni siku hii, mazungumzo haya yalitumia karibu saa tatu.

Jamaa huyu akasema maneno haya,

“Kama Makwega, mimi nakufahamu wewe ni mwanasiasa mzuri na wa siku nyingi tangu tunasoma, na unaifahamu hii CCM, lakini kaka wa sasa kuna jambo linafanyika ambalo ni baya sana hawa vijana wa bodaboda kila mikutano na shughuli zenye kuhitaji umati mkubwa yapo madai kuwa wanakuwa mbele huku wakifanya mikogo na kupamba mikutano hiyo kwa malipo ya kuwekewa mafuta lita kati ya lita 10-15 ili waweze kushiriki kupamba shughuli hizo na baada ya hapo wakipewa posho kati ya 10,000-30,000 na viongozi wa bodaboda wakipewa mafungu zaidi kwa kupamba mikutano na shughuli hizi. Jambo hili linawafaya hawa vijana kutambua kuwa haya mambo yanawezekana, pesa ipo, na jambo hili litafanyika kwa muda na upande husika ukifikia malengo yake ya kujaza mikutano hii, shida Inakuja , shida haipo mbali- hawa vijana umri unakwenda,nguvu zinaisha, je wataishi hivyo hadi lini? Kumbuka hawa ni binadamu wamebeba watoto katika viuno vyao, siyo tasa siyo wagumba, maana yake wanazaa na wana watoto, hiki kizazi chao kinahitaji maisha , ipo siku vijana hawa wataona mambo yao ni magumu na nguvu zitakuwa zimewaishia na hawawezi kuendesha tena bodaboda na hawawezi kufanya mikogo kama awali katika shughuli za umma kwa hiyo fursa ya awali na kuwekewa mafuta na kupewa posho imeondoka, ndugu yangu, ndugu yangu hawa vijana watakuwa maadui wakubwa, hapa ndipo shida kubwa itaibuka.

Kaka Makwega, mimi naangalia, mimi nafuatilia na ninaona hakuna mtu yoyote anayewatazama hawa vijana kama bomu kubwa hapo mbeleni, kujiokoa na hili lazima wawekewe mazingira mazuri, fursa nzuri na hili halipo katika fikra za watu wetu kwa sasa.”

Mwanakwetu alipomaliza mazungumzo aliagana naye na kurudi kwake kwa bodaboda, alipofika kwake Mwanakwetu alichemsha Mzegamgeza wa Mahindi yake matatu akayafakamia, akashiba akauchapa usingizi. 


 

Siku iliyofuata Mwanakwetu alipopita kwa mama yule Muuza Mahindi-Mahindi ya Mzegamzega akamuuliza Mwanakwetu, Baba nilikuona jana ulikuwa unaongea mno na rafiki yako, inaonekana mnaeleewana naye sana.

“Mama yule ni ndugu yangu, nilisoma naye Chuo Kikuu tukiwa vijana wadogo, sijakutana naye miaka mingi lakini sasa tunazeeka, ndiyo maana niliongea naye sana, niliongea naye muda mrefu.”

Mwanakwetu alimjibu huyu mama.

Siku ya leo Mwanakwetu anaamua kuyaweka mazungumzo yake na ndugu huyu katika makala haya.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Wanasiasa wetu wao wanafikiria tu kujaza mikutano ya kisiasa, kujaza umati katika shughuli zao lakini siku ya leo Mwanakwetu anaibua tafakari mpya ambayo inajengwa na ndugu huyu Mkaguzi wa Ndani aliyesoma na Mwanakwetu, Chuo Kikuu kuwa wanasiasa na Wapanga Sera kuweni makini na hawa vijana wa boda boda watakuja kuwatoa machozi, mawazo yenu lazima yahame kufikiri kujaza mikutano ya kisiasa, bali fikirieni kuhakikisha maisha ya vijana hawa waendesha bodaboda yanaboreshwa ili kuinua vizazi vyao, vinginevyo hatari kubwa ipo mbeleni. Vinginevyo vinginevyo ni hatari kubwa.


 

Mwanakwetu Upo? Je makala haya yaitwaje

Mkaguzi wa Ndani Aliyesoma na Mwanakwetu! Boresheni Maisha ya Vijana wa Bodaboada au Mzega Mzega wa Mahindi! Mwanakwetu anachagua Mzega Mzega wa Mahindi.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Makala haya yametayarishwa na MwAnAkWeTu kwa heshima ya Binamu yake Mpendwa Mwalimu Msekwa Njema anayefanya kazi Jijini Dodoma.


 



0/Post a Comment/Comments