Lucas Masunzu - TABORA
Shule ya Sekondari Urambo imeendelea na zoezi la kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano kwa mwaka wa masomo 2025. Katika wiki ya kwanza baada ya shule kufunguliwa, Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Haji Said Simba alitaarifu kuwa zoezi la mapokezi ya wanafunzi linaendelea vizuri kwa kufuata utaratibu uliopangwa. Vilevile, Mwalimu Simba alieleza kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wapya wanapokelewa katika mazingira salama na rafiki kwa ajili ya kujifunzia.
Kwa mwaka huu wa masomo 2025, Shule ya Sekondari Urambo inatarajia kupokea mamia ya wanafunzi wapya kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania. Wanafunzi hao watajiunga katika tahasusi za HGL, HGK, HKL, HGFa , HGLi pamoja na CBG. Katika hatua nyingine, Mkuu wa shule, Mwalimu Haji Said Simba, aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi kupelekea shule kupata matokeo mazuri ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita kwa mwaka 2025 ambapo kuna divisheni I- 96, divisheni II -133, divisheni III-28, Divisheni IV na O hakuna. Alieleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano, bidii na moyo wa kujituma wa walimu katika kuwafundisha na kuwaandaa wanafunzi kitaaluma.
Hata hivyo, Mwalimu Simba alisisitiza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna haja ya kuongeza juhudi zaidi kwa lengo la kuimarisha matokeo ya shule kwa miaka ijayo. Akisisitiza dhamira ya shule kuendelea kusonga mbele, alikazia kwa kusema; ninawashukuru sana na kuwapongeza wote kwa matokeo haya ya ACSEE 2025, hakika kazi mmefanya na imeonekana. Kazi kubwa bado ipo mbele yetu, tujipange na ninawaamini tunaweza kuvuka viunzi.
Kwa upande mwingine, Ofisi ya Elimu Mkoa –Tabora na Ofisi ya Elimu Sekondari Wilaya –Urambo ilitoa pongezi kwa walimu waliojituma, juhudi zao zimezaa matunda hayo. Mtayarishaji wa taarifa hii anaamini kuwa malipo pekee ambayo mwanafunzi wa Kitanzania anaweza kuyatoa kwa serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufuta ada ya shule ya sekondari, ni kufanya vizuri kitaaluma. Ikumbukwe kuwa kupitia sera ya elimu bila malipo, serikali ya Dkt Samia iliondoa ada, moja ya kikwazo kikubwa kilichozuia vijana wengi kupata elimu hasa wale wanaotoka familia zenye uwezo duni. Hivyo, ni wajibu wa kila mwanafunzi wa kitanzania kujituma darasani, kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika mitihani. Serikali imetupatia daraja la mafanikio; sasa ni jukumu letu kulipita kwa bidii na moyo thabiti. Karibu Shule ya sekondari Urambo, Kwa heri kwa sasa.
0762665595
Post a Comment