Adeladius Makwega-Musoma TANZANIA.
Siku hii ilianza kwa Mwanakwetu kuamka alfajiri sana, huku akifungua madirisha ya chumba alicholala maana hali ya hewa ilikuwa ya joto kali, hivyo basi aliamka kitandani na kuyafungua vizuri na madirisha manne ya chumba alicholala na kisha kurudi kitandani.
Kitendo hiki cha kuamka na kufungua madirisha kilimjulisha kuwa kumekucha maana anga lilikuwa jeupe na hata alipotazama saa yake ilidokeza kuwa ilikuwa saa 10.54 (0454)ya Alfajiri ya Afrika Mashariki.
Mwanakwetu alipotazama hali ya hewa ya Mji wa Musoma alibainia kuwa ni sentigredi 26, huku hali ya joto ya juu kwa juma zima ilikuwa ikionekana kuoana(kufanana) kwa siku nne mfululizo; Ijumaa, Alhamisi , Jumatano na Jumatatu kwa sentigredi 27. 20.
Mwanakwetu baadaya ya haya yote aliamua kusikiliza masomo ya jumapili hii na mahubiri yake kutoka kwa Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki inayojihusisha na Uinjilishaji wa Watu Ulimwenguni Kadinali Luis Antonie Tagle.
“Na tumtazame Yesu, Neno aliyefanyika mwili, akijifunua kwetu kupitia masomo ya dominika hii. Leo ni Dominika ya 17 ya mwaka C wa Kanisa, Julai 27, 2025. Katika Injili ya leo, Yesu anatufundisha mafundisho kuhusu Kusali. Funzo la awali ni kuwa tunapaswa kusali kama watoto wa Mungu, tukitafuta utakatifu wa jina lake na kuja kwa Ufalme wake. Kisha pili tunasali kwa ajili ya mkate wa kila siku, msamaha, na ulinzi.
Sala ya Bwana au Baba Yetu inatubadilisha na kutufanya kuwa watoto wa Mungu kama Yesu. Yesu pia anatufundisha thamani ya uvumilivu katika kusali. Imani yetu katika wema wa Mungu ni wito wa kuzingatia tabu na vilio vya jirani zetu kila siku.
Kama Mungu anavyotusamehe sisi wenye dhambi, vivyo hivyo nasi tunapaswa kuwasamehe wale waliotukosea. Kama Mungu anavyowapa watoto wake mema, hasa Roho Mtakatifu, nasi tunapaswa kujibu mahitaji ya jirani zetu kwa moyo wa furaha kulingana na uwezo wetu.”
Haya ni Kadinali Tagle juu ya dominika hii,nina hakika nawewe msomaji wangu umeyasikia haya hapo kanisani kwako.
Siku ya leo nakuomba utulie maana na hili la aya ya mwisho ya Injili ya Jumapili hii kutoka Injili ya Luka 11:1-13 inasema haya;
“Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Je Si Zaidi Ya Baba Yetu Aliye Mbinguni?”
Nakutakia Jumapili Njema.
0717649257

Post a Comment