
Adeladius Makwega-MBAGALA
Juni 6, 2025 Mwanakwetu aliamka mapema kidogo na kisha kuivuta simu yake vizuri na kutembelea ukurasa wake mmoja wa mitandao ya kijamii. Katika ukurasa huo, ulionekana sura za marafiki zake kenda, wakiwa katika makundi matatu matatu.
Kwa hakika msomaji wangu hao jamaa tisa, kila mmoja alimtazama na kukumbuka simulizi tele kwa namna alivyokutana nao kwa vipindi tofauti na maeneo tofauti , maana maisha ni safari. Mwanakwetu akawa anasema hivi hawa jamaa wote nikitaka kuwaandikia makala je nitakuwa na simulizi gani? Mwanakwetu akawatazama mmoja baada ya mwingine akikumbuka simulizi tele huku akicheka. Mwanakwetu akawa anataka kumchagua rafiki mmoja kati ya hao ili amuandikie makala, je amchague nani? Mwanakwetu likamjia akilini mwake hili,
“Ukitazama chati yenye picha ya marafaiki hao tisal wanawake ni watatu na wanaume sita. Kati ya hao wanaume sita, wanaume Wakristo wapo watano na Muisilamu ni mmoja ambaye ni Abdallah Msabaha. Ukija kwa marafiki wa jinsia ya Kike kati kundi lao hao watatu, Wakristo wako wawili lakini Muislamu ni mmoja tu ambaye ni Zarina Nassoro.”
Mwanakwetu akasema kati ya Mwanaume na Mwanamke achaguliwe yupi kuandikiwa makala? Mwanakwetu akamchagua Bi Zarina Nassoro. Natambua msomaji wangu tupo pamoja hatua hatua kwa namna ninavyompata Bi Zarina Nassoro kumunadikia makala. Je Mwanakwetu anasimulia nini juu ya Binti huyu? Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba utambue kuwa Bi Zarina Nassoro ni Binti kutoka Kabila la Wazaramo ambayo ni mwanasheria kwa taaluma, Mwanakwetu anapenda kumuita Wakili Mzaramo.
Msomaji wangu unaweza kuwa na maswali mengi, lakini haya niliyokwambia yanakutosha sana. Nilipokuwa natafakari namna nitakavyotayarisha makala ya Bi Zarina Nassoro akilini mwangu zilinijia simulizi tatu kisha nikatumia dakika tatu kuchagua simulizi moja kati ya hizo, huku simulizi mbili zikibaki kibindoni.
Siku ya kwanza Mwanakwetu anamfahamu huyu Wakili Mzaramo ilikuwa kupitia Wakili mmoja mkongwe, Bi Zarina alipouliza na Mwanakwetu wewe ni mtu wa wapi? Alimjibu yeye ni Mzaramo wa Mkoa wa Pwani. Mwanakwetu akasema kumbe wewe ni Wakili Mzaramo, Zarina akajibu ndiyo huku akicheka. Mazungumzo na Zarina yalikuwa juu ya kazi moja ambayo alipewa na Mwanakwetu na aliifanya vizuri sana , mwanzo mwisho na kisha Mwanakwetu akalipa pesa na kila mmoja kuendelea na mambo yake. Wakati Zarina anaifanya hiyo kazi akilini mwa Mwanakwetu alikumbuka kisa hiki cha kweli kabisa cha mwaka wa 2009/2010
“Wakati huo Mwanakwetu alipewa kipindi kinachoitwa Biashara na Uwezeshaji na wakubwa wake pale TBC Taifa . Kipindi hiki kilikuwa kinaendesha na Dkt. Jacob Nduye , huyu Daktari wa Falsafa alihama TBC kwenda taasisi nyingine ya umma, hivyo basi vipindi vyake kugawiwa watumishi wengine. Mgao wa Mwanakwetu alipewa kipindi hiki cha Biashara na Uwezeshaji.”
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu kapewa jukumu jipya la kufanya kazini kwake.
“Siku moja Mwanakwetu akaenda Mkuranga kurekodi makala juu ya zao la Korosho, akazunguka akaongea na wakulima, maafisa biashara kisha akaenda kuongea na Mkurugenzi Mtendaji, wakati huo ni huyu Bi Sipora Liana . Wakati Mwanakwetu yupo katika benchi la kuelekea kwa Mkurugenzi Mtendaji kukawa na wazee kama wanne na kijana mmoja wanalalamika mno dhidi ya Serikali.”
Katika lile benchi mzee mmoja ambaye alikuwa amevalia kanzu nzuri na nywele zake zinapendeza akamuuliza Mwanakwetu wewe mwenzetu ni nani? Unakwenda kufanya nini kwa Mkurugenzi Mtendaji? Mwanakwetu akajibu ,
“Mimi ni Mtayarishaji Vipindi, Mtangazaji na Mwandishi wa TBC Taifa, nimekuja kufanya vipindi vya Biashara na Uwezeshaji nimeongea na wakulima , nimeongea na maafisa sasa namalizia kwa Mkurugenzi Mtendaji ili nirudi redioni.”
Huyu mzee machachari akasema nilijua wewe ni askari, sasa wewe ingia kwanza sisi tutaingia baadaye. Mwanakwetu akasimama akaingia ofisini kwa Bi Sipora Liana akaongea naye kisha kutoka. Wakati wa kutoka jamaa wakawa wanaingia kwa Mkurugenzi Mtendaji. Mzee Yule mwneye kanzu akamuomba Mwanakwetu awasubiri ili waongee naye jambo. Mwanakwetu akajibu sawa lakini Mwanakwetu akiwa ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji aliambiwa aende kwa Mhasibu atapewa shilingi 35,000/= ya nauli. Kwa hiyo wao wanaingia kwa Mkurugenzi Mtendaji nayeye Mwanakwetu anakwenda kuchukua pesa kwa mhasibu, kisha akarudi kuwangoja hawa wazee getini. Hapo akakaa kama nusu saa wazee wakaja wakamsimulia kisa hiki,
“Mwandishi sisi tumedhulumiwa Lori lenye Korosho zetu zilikuwa njiani kwenda kuuzwa Dar es Salaam Mkuu wa Wilaya akachukua gari na mzigo wenyewe, tunaambiwa sisi wahujumu uchumi, wanasema kwanini hatuhuziuza kwenye Stakabadhi Gharani? Wewe Mwandishi tunaomba ushauri wako.”
Mwanakwetu akawajibu, Nitawatayarishia makala lakini kwanza ngoja nimsikilize Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga anasema nini? Mwanakwetu akawaacha pale wanamngoja akamuhoji Mkuu wa Wilaya na akakiri kilichotokea. Akarekodiwa kisha kurudi walipo wazee wale. Lakini akawaambia hii makala haiwezi kuwasadia sana tafuteni Wakili.
Yule Kiongozi wa wazee hawa alikuwa akiitwa Ustadh Kumbirwa ambaye alikuwa na akilini sana, huku akizungumza lugha nyingi, akasema hawa jamaa hawana pesa ya kulipia wakili na huku Mkuranga hakuna, Wazaramo wote Marofa hakuna Wakili Mzaramo, kungekuwa na wakili Mzaramo angeweza kuanza mapambano na kesi huku na sie tunauza korosho zetu zilizobakia majumbani.
Mwanawetu akaongea nao vizuri wakakubaliana wachange pesa ya kutafuta wakili Dar es Salaam . Kweli mazungumzo yalipokwisha tukaachana na wale wazee watatu na kijana mmoja wakarudi Kiparang’anda na Mwanakwetu na yule Mzee kiongozi Ustadhi Kumbirwa tukapanda gari kuelekea Mbagala. Mwanakwetu akafanya makala yake vizuri , Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani wakaisikia makala hiyo, wakamtafuta Mwanakwetu na kuomba mawasiliano na wazee wale wakapewa lakini wakati hawa wazee wakiwa tayari mahakamani kupinga lori na mzigo wa korosho zao kutaafishwa. Mazungumzo nje ya mahakama yaligongwa mwamba, ndugu hawa walikuja kushinda kesi mwaka 2016, wengi wakiwa wamefariki dunia.
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yu kitandani kwake haya yote anayatafakari Asubuhi ya Juni 5, 2025 mara baada ya kuona picha ya rafiki zake tisa akiwamo Zarina Nassoro Wakili Mzaramo. Na alikumbuka namna Ustadhi Kumbirwa alivyosema,
“Wazaramo wote Marofa hakuna Wakili Mzaramo .”
Baadaye Mwanakwetu akaamua kuyatayarisha makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kikubwa nilitaka msomaji wangu ufahamu kuwa Wakati huo Mkuranga haikuwa na Wakili Mzaramo, mawakili wengi walikuwa Dar es Salaam na wa makabila mengine lakini hivi sasa Wazaramo mnaye wakili wenu, binti yenu anaitwa Zarina Nassoro, tena wakili mwenye akili, mkiwa kesi msisite kumtafuta ndugu yenu huyu sasa Mkuranga siyo ile ya Ustadh Kumbirwa ya kutafuta Wakili Dar es Salaam.
Jambo la mwisho ni la mawakili wote mkumbuka kusaidia jamii zenu, pesa inakuja baadaye Watanzania hawa ni masikini.
Mwanakwetu upo? Je Wakili Mwenye Akili au Wakili Mzaramo?AAAH Chaguo ni lako.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment