
Adeladius Makwega-Musoma MARA
Ni majira ya asubuhi ya Ijumaa ya Juni 6 ya 2025, Mji wa Musoma ukibarikiwa kuwa na mvua kubwa ambayo haikujulikana ilitokea wapi, na ikiwa vigumu kueleza ni mvua ya masika, mvua ya vuli au mvua ya kiangazi. Dereva wa Boda boda aliyopanda Mwanakwetu akisema hii mvua inakuja sasa wakati mahindi yamekauka? na kuharibika kabisa. Ingekuja wakati mimea bado midogo, sasa inakuja kufanya nini kama siyo Mvua ya Kuozesha Dagaa? Mwanakwetu akamjibu huyu kijana kuwa hii ni mvua ya kuondoa vumbi.
Mwanakwetu aliagana na bodaboda huyu kisha kukaribishwa na mandhari ya watu wengi kila mmoja na miavuli, wengine na makoti na naye Mwanakwetu akiwa na sweta lake kaba shingo la rangi ya khaki, huku akijongea katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.Gafla Mwanakwetu anaiona kwa mbali Kwa mbali Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huu, wale wenye sare na wale wasiovaa sare. Hapa hapa Kanali Mtambi akiwa kando, huku akinyeshewa na mvua hiyo , gafla anampokea Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde naye Kanali Mtambi kuyasema maneno haya,
“Karibu sana Mhe waziri, Mhe Waziri kitaifa tunatambua mchango wa Sekta ya Madini ni asilimia 10 lakini kwa mkoa wetu Sekta ya Madini inachangia asilimia 18 huku wilaya zote za Mkoa wa Mara zina madini. Kumekuwa na changamoto za uelewa lakini kwa sasa uelewa upo na changamoto zote zinatatuliwa, kwa bahati nzuri sheria ya madini ya Tanzania ipo vizuri. Binafsi nimewahi kufanya kazi huko Afrika ya Kati , niliwahi kufanya kazi katika taifa moja ambapo wananchi hawaruhusiwi kuchimba ardhini mita tatu tu, na kibaya zaidi hata hiyo mita tatu mali siyo ya serikali bali ya taifa moja la ulaya.”
Mara baada ya Kanali Mtambi ambaye ndiye Mkuu wa Mkoa wa Mara kuyatoa maelezo haya katika kikao cha ndani, huku kikishuhudiwa na dazeni mbili ya viongozi akiwamo Katibu Tawala Mkoa wa Mara ndugu Gerald Msabila Kusaya, hapa hapa Mhe Waziri Mavunde alichukua usukani wa mazungumzo haya na kuyasema haya ;
“Kwanza nawajulisha kuwa Serikali inanunua hedikopta moja mpya ambayo itatumika kufanya utafiti wa awali wa uwepo wa madini ardhini na hivi karibu zoezi hili la ununuzi litakamilika.”
Waziri Mavundo aliendelea kuunyonga vilivyo usukani wa mazungumzo haya na kuyagusia na haya,
“Tumefanya makubaliano na kampuni moja binafsi ambayo itakuwa inakodisha mitambo kwa wachimbaji wadogo wadogo kwa maeneo yote ya madini, pia tumeongea nao hawa jamaa wa kuleta mashine ndogo ndogo kutoka China ambazo zitakopeshwa kwa wachimbaji hao hawa wadogo wadogo.”
Mara baada ya mazungumzo haya Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi alimuongoza Waziri wa Madini katika Maandamano kuelekea kilele cha Kongamano la madini lililoanza Juni 3, 2025. Mwanakwetu upo? Kumbuka tu
“Serikali Inanunua Hedikopa ya Kutambua Maeneo yenye Madini Ardhini.:
Ahlan wa Sahlan
0717649257
Post a Comment