Adeladius Makwega-MBAGALA
Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni Makala ya Uchambuzi wa Katuni mbalimbali kama zilivyochorwa na kuzingatiwa na wachoraji wetu. Kuianza safari ya makala haya katika muktadha wa siasa Mwanakwetu anaikamata katuni ya kwanza kabisa iliyochorwa na Masoud Kipanya, katuni hii inaonesha vilima karibu vitano huku vilima vitatu vikubwa vikubwa, lakini viwili ni vilima vidogo.
Mwanakwetu alipotazama nchi hii yenye vilima vitano akakambuka katika Biblia juu ya nchi ile yenye vilima saba katika Sura ya 17 ya Ufunuo huo wa Yohane. Mwanakwetu akajiuliza hii katuni inaonesha njiwa akiruka juu kutoka kilima kimoja kwenda juu kuvisaka vilima vingine, je hii nchi yenye vilima vitano ni ipi?
Mwanakwetu anaamini hii ni Afrika Mashariki na mchoraji wake anazuga kwa kuchora yaani anafanya fumbo mfumbie mjinga mwerevu atang’amua tu, lakini pia inawezekana vilima vingine vitatu vimezibwa na vilima viingine maana Afrka Mashari ina mataifa nane.
Sasa huyu njiwa ni nani? Mwanakwetu anaamini kuwa huyu ni Baba Askofu Josephart Gwajima ambaye ni Mbunge Kawe kupitia CCM na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa. Hapa kunaoneka Juni 2, nadhani ya 2025, tarehe hii imebandikwa ikionesha siku la tukio la kufungwa kwa Kanisa la UFUFUO NA UZIMA kwa amri ya serikali . Mchoraji wa Katuni anajenga dhana kuwa Askofu Gwajima yupo katika Taifa mojawapo la Afrika Mashariki.
Mwanakwetu anaikamata katuni ya pili ambayo inaonesha taswira mbili za Tembo ambaye anapita darajani huku taswira ya pili ikionesha tembo akijinasibu kwa mwenzake akisema mwana si unaona namna tulivyokinukisha tulivyotikisa lile Daraja?
Mwanakwetu anaitazma katuni hii kwa jicho pembe ambayo inaonekana imechorwa Mei 30, 2025 na kuweza kuielewa katuni hii ni vizuri kukumbuka ni matukuo gani makubwa yalitokea tangu Mei 30,2025 kurudi nyuma nchini Tanzania? Kikubwa na mara baada ya wanaharakati kutoka Kenya kukataliwa kuingia nchini Tanzania na matukuo mengine yaliyofuata ikiwa pamoja na vijana wa Kenya kuanza kurusha maneno dhidi ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwanakwetu sasa anaikamata katuni ya tatu ambayo imechorwa na Masoud Bin Kipanya ambapo kunaonekana Jamaa waliyovalia mavazi ya CCM, huku wakipambana na jamaa waliyovaa mashati ya rangi nyingine, vita ikipamba moto wakirushina makonde na magumi mazito mazito, mara mateke na magongo. Huku wapiganaji waliovaa mashati mengine kwa ujumla wao wakipokea kichapo lakini wapo katika uwanja wa vita hawajakata tamaa.
Mwanakwetu anapoitazama hii katuni ni hali ya siasa za Tanzania ambapo ni mapambano baina ya CCM na Wapinzani lakini pia mpambano pia upo baina ya CCM na CCM wenzao, mapambano haya yanatoa taswira hata changamoto ambazo wapinzani wanazipitia kwa sasa ni nzito lakini CCM ya yenyewe ipo njia panda ambapo vita ndani ya CCM imeonekana sasa kuiva.Mwanakwetu anasema ebu tuone hadi mwisho hali itakuwaje?
Mwanakwetu anaikamata katuni ya nne ambayo imechorwa na Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji DW Kiswahili hapa kunaonekana gari inaendeshwa nje ya barabara. Gari hii inaendeshwa na mama mmoja aliyevalia Hijabu ya njano na kijani huku ndani ya gari hii ndogo aina ya motokaa kuna jamaa wawili, mmoja anasema hoya mwambie tumeacha njia apunguze kasi, jamaa mwingine anasema wewe unataka nishushwe? Gari likiendelea kutokomea machakani. Katuni hii inadokeza siasa za Tanzania za sasa huku kinachopigiwa chapuo kunaonekana hata wanaongozwa wanakuwa waoga kueleza ukweli wa mambo kuogopa kutumbuliwa na mabalaa mengine.
Kwa jicho la mtayarishaji wetu huyu, dereva ni Rais wa Jamhuri ya Tanzania na hali ya siasa ilivyo. Swali la Mwanakwetu Je ni kweli wasaidizi wa Dkt. Samia wanaogopa kumwambia ukweli?Hili ni swali ambapo Shirika la Utangazaji la Ujerumani Mwanakwetu anaamini wanaliibua katika katuni hii.
Jambo la Msingi kwa msomaji wa Mwanakwetu ni la pande mbili kwa wale wanaombiwa kama kweli wajirekebishe ili kusaidia wachoraji wa katuni kupata nafasi ya kuchora katuni yenye mtazamo mwingine hapo baadaye.
Basi hadi hapo, ndiyo na mimi natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo kumbuka nilikuwa katuni nne; ile ya nchi yenye vilima vitano, ile ya wanyama watikisha daraja , na ya tatu ni hii ya varangati baina ya CCM na CCM na CCM na wapinzani naya nne nay a mwisho ni hii ya dereva wa motokali iliuyochepuka njia. Hapo ndiyo nukta ya makala haya siku ya leo. Je makala haya niyaitaje? Nchi ya Vilima Vitano? Dereva Aliyechepuka Njia?Mwanakwetu anachagua Nhi ya Vilima Vitano.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment