Adeladius Makwega-MBAGALA
Kwa siku kadhaa Mwanakwetu alikuwa kimawazo akifuatilia kwa kina Kikao kimoja huku Arusha ambacho kilikuwa kinawakutanisha jamaa kadhaa wanaojihusisha na mambo ya Sheria nchini Tanzania, wakiwamo Mawakili wa Serikali, ambapo kiongozi wao ni Wakili Mkuu wa Serikali ndugu wa Mwanakwetu, Dkt Ally Possi.
Msomaji wa Mwanakwetu unaweza kujiuliza ni yepi majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali?
Hawa jamaa wana kazi nyingi miongoni mwao ni;
“Kuendesha na Kusimamia mashauri yote ya Madai, Haki za Binadamu, Kikatiba na Usuluhishi zinazoihusu Serikali. Kutoa miongozo kwa Wanasheria na Mawakili wa Serikali ambao wanasimamia uendeshaji wa kesi za madai, kesi za haki za binadamu, na Kikatiba na mashauri ya usuluhishi yanayoihusu Serikali. Kuratibu Mashauri ya Madai, Haki za Binadamu, kesi za Kikatiba na Usuluhishi katika Mahakama na Mabaraza ya Usuluhishi kwa niaba ya Serikali. Kuandaa na kufungua mashauri ya madai ikiwemo Katiba, Haki za Binadamu na Usuluhishi kwenye Mahakama na Mabaraza ya Usuluhishi ndani na nje ya Tanzania. Kutoa ushauri wa Serikali kuhusu mashauri ya Madai na Usuluhishi na Kuratibu mwenendo wa mashauri ya Serikali yaliyopo Mahakamani na Mabaraza ya Usuluhishi ndani na nje ya nchi. Kuchukua jukumu la kuendesha mashauri au kesi yeyote yenye maslahi umma; na Kutunza kumbukumbu za mashauri au kesi zote za Serikali na kutoa taarifa mara kwa mara kwa wadau husika.”
Mwanakwetu akajiuliza kazi hizo za Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali je zinafanyika kwa Uweledi?
Kwa hakika kwa muda mrefu Mwanakwetu hakuona taarifa nyingi juu ya mashauri haya kutolewa hadharani , japokuwa Vyombo vya Habari vya Kimataifa vimekuwa vikiripoti baadhi ya mashauri hayo, jambo jema kidogo hivi punde ndiyo Mwanakwetu ameshuhudia taarifa kwenye vyombo habari juu ya mashauri ambayo Serikali imeshinda.
Mwanakwetu anaamini mashauri tunayoshindwa tuelezwe na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kwenda mbali zaidi kwa kutueleza hatua zote tangu mwanzo wa shauri hadi hukumu ya mashauri, kama tumeshindwa kwanini, ili tuwe na uelewa mpana wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na inafanya kazi namna gani?
Katika hili Dkt Ally Possi na Naibu wake Bi Alice Mtulo waongeze juhudi angalau tupate taarifa ya kila mwezi kwa mashauri haya moja baada ya lingine.
“Hii itasaidia hata jamii ya Watanzania kutoa mawazo yao juu ya mashauri tuliyoshindwa ili wakati mwingine tusiingie katika kulitia hasara taifa hili. Pia itatoa nafasi ya umma wa Watanzania kuwapongeza wale mawakili hodari wnaaofanya vizuri katika mashauri yenye maslahi mapana ya taifa, wakipandishwa ngazi isionekana wamependelewa.”
Mwanakwetu yu nyumbani kwake akawa anaitazama kazi ya pili ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo ni Kuchukua jukumu la kuendesha mashauri au kesi yeyote yenye maslahi ya umma.
Wakati Mwanakwetu anaitafakari kwa kina kazi hii, akapokea taarifa kutoka huku kwao Mkuranga.
“Mwanakwetu kwemaaa? Kaka siye Wazaramo Mungu anajua sana kutueleleza(kututesa) Nakupa taarifa kuwa yule Wakili Mzaramo Nassira Binti Nassoro sasa hivi ni Hakimu wa Mahakama moja huko Arusha, siyo Wakili tena. Sasa Mwanakwetu Wazaramo wa Mkuranga tuna mtihani mzito, itabidi Tumtengeneze Wakili Mwingine Mzaramo.”
Mwanakwetu akastaajabu Nassira Binti Nassoro kumbe sasa ni hakimu? Mwanakwetu akasema,
“Wazaramo Mmeula wa Chuya.”
Nikamjibu huyu jamaa kuwa unadhani hivi sasa kila mtu anapata kazi? Hata kwa baniani wanahitaji mtu makini sembuse mahakamani?
Mahakama inahitaji wenye akili ili wafanye maamuzi sahihi lakini naona faraja ipo kwa Shule za Kata, zipo nyingi zingine zina majina hadi ya Mizimu na Vinyamkera vya Machakani na kwenye mibuyu na mikuyu vya Wazaramo kwa hiyo ndugu zangu wa Mkuranga somesheni watoto mpate Wakili Mwingine Mzaramo.
Jamaa huyu akawa anacheka kweli kweli, wakati huo huo Mwanakwetu akapokea simu nyingine kutoka kwa kijana mmoja wa Sheikh wa Mkoa wa Mara akialikwa kula pilau la Iddi. Mwanakwetu kwa umelo wa pilau akaweka Kalamu yake chini, akapiga kanzu yake maridadi kwenda kupiga mpunga wa Idd.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika makala haya yana shabaha tele; Mosi Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inawajibu kujitahidi kutoa taarifa za kazi zake na majukumu yake ya kila siku kwa umma, hasa juu ya mashauri yote yanayohusu maslahi ya taifa iwe katika mahakama mbalimbali ziwe za ndani ya nchi na nje ya nchi ili wananchi tufahamu, kielezwe kinachoendelea hatua kwa hatua.
Pili makala haya yataendelea kufuatilia kwa kina shughuli za Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, hatua kwa hatua, hasa kwa sasa tunavyoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 ili kutoa uelewa mpana wa ofisi hii ya umma kwa jicho la kichambuzi. Mwanakwetu anaweka wazi kabisa Dkt . Ally Possi na Naibu wake Bi Alice Mtulo wakae mkao wa kula.
Tatu Mwanakwetu anamtakia kazi njema yule Wakili Mzaramo ambaye sasa ni hakimu huko Arusha. Nne Mwanakwetu anaipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kumpata mtumishi wao mpya Bi Nassra Nassoro na mwisho Mwanakwetu anawatakia Waislamu wote Iddi Njema.
Mwanakwetu upo?
Je makala haya niyahitaje? Mpunga wa Idd? Majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali? Wakili Mwingine Mzaramo? Wazaramo Mmeula wa Chuya au Mungu Anajua Kuwaeleleza Wazaramo. Mwanakwetu anachagua Mungu Anajua Kuwaeleleza Wazaramo.
Nakutakia Siku Njema.
makwadeladius @gmail.com
0717649257
Post a Comment