MKIWA WAKUBWA MSIFUNGIE MAKANISA

 


Adeladius Makwega-MBAGALA

Mwanakwetu nikaisoma barua hiii mara mbili mbili na kisha nikaweka mkazo katika majina ya aliyesaini barua hiii yakitajwa kwa majina ya wazi mawili na majina vifupisho mawili yaani Emmanuel R. M. Kihampa. Mwanakwetu nilitambua maana ya jina Emmanuel yaani Mungu pamoja nasi lakini jina la Kihampa lilinipa tafakari kubwa sana lakini nilitambua ni majina kutoka Tanga na wapo kwa akina Kihampa ninaowafahamu mimi hasa mazingira ya kazini.

Nilimkumbuka mama mmoja anayeitwa Edina Rajabu Kihampa aliwahi kuwa Mkuu wa Vipindi pale TBC, mama mmoja mwema, mkarimu, mcheshi hapendi ugomvi na mizengwe sehemu ya kazi na muda wote anafurahi na jambo lilipopelekwa kwake lilikwisha bila maneno. Mwanakwetu akajiuliza huyu Kihampa Mfunga Makanisa ni yupi? Ni Kihampa yupi? Je anayo nasaba ya yule mama ninayemfahamu?

Akili ya Mwanakwetu inajiuliza bila kupata majibu

Edna Rajabu Kihampa mambo yakifika kwake yanakwisha kwa amani? Hata Mwalimu Joe Rajabu Kihampa ni mtu wa suluhu huyu Kihampa aliyefunga Kanisa la Ufufuo ni yupi? Mwanakwetu akawa natafakari kwa muda mrefu, kumpigia simu huyu mama Edina Rajabu anatamani ampigie amuulize swali hili,

“Nyie akina Kihampa sasa mnafungia Makanisa yetu?”

Hapa hapa Mwanakwetu akajijibu mwenyewe akisema nikimpigia simu dada Edna Rajabu atasema,

“Wewe Makwega nitakusemea kwa mkeo bado haujaacha utundu tu , sasa hivi ushakuwa mzee?”

Mwanakwetu anatafakari mwenyewe jina la Kihampa akilini mwake ambapo leo hii msomaji wangu unabahatika kushirikishwa tafakari hii ya kweli kabisa. Siku zinasonga huku shauri la kufungwa Kanisa la Ufufuo na Uzima mara mahakamani, mara Waamini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima wanasali nje, mara wanafukuzwa na polisi, akilini mwa Mwanakweti Jina la KIHAMPA linatafakariwa kwa kina.


 

Juni 17, 2025 alfajiri ikamjia Mwanakwetu akilini mwake tukio moja la kweli kabisa la Binti Kihampa yaani Edina Rajabu Kihampa akiwa Mkuu wa Vipindi pale TBC nadhani mwaka 2011 naye Mwanakwetu akiwa ni Mtayarishaji Vipindi Mwandamizi Daraja la Pili.

“Makwega unaitwa kwa dada Edna.”

Unapoitwa kwa Edna Rajabu Kihampa unakuwa hauna wasiwasi maana unajua hakuna ugomvi, hata likiwa jambo gumu litakwisha kwa amani tu ya Bwana. Kweli nikatoka hadi ofisini kwake, nikafika nakumsalimu vizuri sana tunaelewana naye vizuri sana. Huyu mama ni mweupe sana baadhi ya wadau wa Radio Tanzania wakawa wanasema,

“Makwega Bwana hautosikia hata siku moja anagombana na Mkuu wa Vipindi.”

Wadau wanaongea, Mdau mwingine akasema Mkuu wa Vipindi ni mweupe, Mwanakwetu hagombanagi na akina mama weupe. Watu wengi wanapotaka jambo lao lifanyike linapitia kwa Mkuu wa Vipindi. Hapo Msomaji wangu nimeitwa ofisini kwa Mkuu wa Vipindi ambaye ana ubini wa Kihampa. Mama huyu akasema maneno haya,

“Mdogo wangu Makwega leo naona umepiga suti ya visanduku? Mkeo kaja nini kutoka Tanga? Haya niambie hii suti umenunua wapi ili na mimi nikamnunulie profesa?”

Mwanakwetu hapo anacheka tu huku akimjibu Bosi Edna Rajabu kuwa Suti hii nimenunua Euro 550 Ireland leta pesa nikuagizie. Hapo hapo bosi Edna Rajabu akasema maneno haya,

“Mdogo wangu Makwega! Tumejadili na wezangu  na tumekubaliana kuanzia kesho utusaidi kufanya vipindi ya Christiana Councel of Tanzania(CCT)  vile vya Inueni Mioyo , Kumekuchwa, Tumuabudu Mungu, Tumshukuru Mungu na Bibilia Yatuambia Nini? TEC wao Mtayarishaji wao yupo bali CCT Mchungaji John Magafu amepata tatizo huko CCT kwa hiyo hatokuja tena hadi atakapangiwa mchungaji mwingine, wewe jukumu lako watakuja wachungaji, utasimamia huku ukiweka yale maelezo ya kufungua na kufunga kipindi, maagizo haya nimeshawaeleza Injinia Tatu Ali na Joseph Masanja na sawa mdogo wangu ?”

Mwanakwetu akajibu sawa akatoka zake kwenda kutekeleza jukumu hilo.Wadau wanacheka Makwega jambo lako ukitaka alikubali muagize mama mweupe?Watu wanamtania Mwanakwetu.


 

Kwa hiyo jukumu hili alipewa Mwanakwetu na kazi ikaanza siku hiyo hiyo, Wachungaji wanatoa mahubiri yao,yanatayalishwa vizuri , Mwanakwetu anaweka sauti ya Mwanzo na Kufunga,, Mwanzo na Kufunga hadi alipopatikana mchungaji John Kamoyo na yeye akajifunza tekinolijia kidogo kidogo hadi akafuzu. Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu Mchungaji John Magafu alikuwa mtayarishaji mzuri sana wa vipindi vya dini Kutoka CCT huku akifahamu tekinolojia za kisasa, iwe kwa Redio na hata Runinga, kazi yote alikuwa anaifanya mwenyewe mwanzo mwisho.

“Unajua unapompa mtu mafunzo kisha unamuondoa ni hasara kubwa kwa taasisi husika.”

Mwanakwetu akatumika vizuri kiokoa jahazi baada ya kuondoka Mchungaji Magafu na aliyesaidia kuokoa jahazi hilo kwa kumshawishi Mwanakwetu alikuwa na Binti Kihampa, Edna Rajabu Kihampa ambaye pengine ni mdogo wake Emmanuel Kihampa au mtoto wa kaka yake, sijui ndiye aliyelifunga Kanisa la Ufufuo na Uzima? Kwa hiyo Mwanakwetu kila anapoisoma barua hiii ya Kufungwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima jina la Kihampa linampa tafakari nyingi sana kama hiyo ninayokusimulia katika makala haya siku ya leo… Makala ya Tafakari.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa familia zetu za Kikristo mtoto anapozaliwa hauwezi kuisha mwaka mtoto ajabebwa kwenda madhabahuni, kwa sisi wa zamani tulifungwa nepi au vipande vya khanga vilivyokatwa katwa vizuri unafungwa na pini na chupi ya mpira kanisa kwenda kubatizwa ili maisha yako ya duniani unatakiwa kuanza na Bwana. Lakini lakini tunapokuwa watu wazima tunajisahau mno. Mkiwa Wadogo Mnaletwa na Wazazi wenu madhabahuni kwa Unyenyekevu MKUBWA lakini Mkiwa Wakubwa na Mamlaka Mnafunga Makanisa.

Mwanakwetu kwa makala haya anatukumbusha tukumbuke hilo na inapokuja kesi dhidi ya nyumba ya ibada, iwe Kanisa iwe Msikiti jitahidi mno kwa nafasi yako kutumia hekima kulitatua jambo hilo, hili jina lako litafakariwe kama u mpatanishi. Ni kweli mamlaka tunayapata tukiwa duniani ni kipindi kifupi ni muda mchache sana kumbuka tukifa tunabebwa na kupelekwa kanisani kusaliwa.Kanisa nina hakika haliwezi kutukataa tunaweza kusaliwa vizuri sana lakini ni mbaya sana tukisaliwa huku watu wanasimanga. Tuwe makini kama dada yangu Edna Rajabu Kihampa alivyokuwa Pale TBC wakati Mchungaji John Magafu ameondoka CCT alivyomuita Mwanakwetu na kumuomba kuifanya kazi ile ya CCT yeye kama Mkristo na Mkuu wa Vipindi akiwa Mkristo mwenzake Mwanakwetu wakaifanya kazi hiyo na hadi leo hii inasimuliwa katika makala haya.


 

Mwanakwetu upo? Kumbuka tu

“Mkiwa Wakubwa na Mamlaka Mnafunga Makanisa.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 











0/Post a Comment/Comments