Adeladius Makwega – MBAGALA
Katika matini ya pili niliutazama mgogoro wa Tambaza na Shule ya Sekondari ya Muhimbili ambapo jambo hilo lilisababisha mengi hadi Shule ya Tambaza kufungwa na serikali, nyuma ya pazia kukiwa na madai kuwa viongozi kadhaa wa serikali wakati huo walikuwa wanaipendelea Shule ya Msingi Muhimbili kwa hoja kadhaa.
Mazungumzo kadhaa ya wanafunzi wa Tambaza yalimtaja moja kwa moja Waziri Mkuu wa wakati huo Ndugu Samweli Malecela kuwa yeye ni miongoni mwa walengwa hao. Hali hiyo ilikwenda mbali nakumtuhumu Mkuu wa Shule ya Tambaza Mwalimu Julius Mushi wakati huo kuwa na yeye aliingizwa katika sakata hilo kwa kupokea kitu kidogo kutokana na suala la uwanja huo kuchukuliwa na Shule ya Muhimbili.
Tuhuma hizo hazikuzungumza na wanafunzi tu kama nilivyokwambia bali walimu wa muda mrefu, watumishi wa muda mrefu wa Tambaza wakiwamo wapishi na hata baadhi ya wanafunzi waliosoma shule hii miaka ya nyuma ambao wengine walikuwa ni wazazi wa wanafunzi wa Tambaza kwa wakati huo.
Ndugu msomaji wangu kwanza kwa leo nakuomba nisilimalizie tukio hili la Ukuta wa Shule ya Muhimbili naliweka kiporo kidogo naomba sasa nilitazame tukio la Mgogoro huu wa Azania na Tambaza ambalo lilikuwa tukio dogo sana kati ya matukio kadhaa ya shule hii.
Ifahamike wazi kuwa rika za wanafunzi wengi wa sekondari ni rika la kupevuka kwa hiyo hapo urafiki baina ya mvulana na msichana huibuka na jukumu la mzazi na mwalimu ni kumkanya kijana/binti katika mambo hayo.
“Chanzo cha ugomvi kilikuwa ni nikugombea msichana wa Jangwani. Wanafunzi wa Azania hawakupenda kuona kijana wa Tambaza kuwa na hata mazoea na binti wa Jangwani Sekondari kwani waliamini wasichana wa Jangwani ni wao(Azania). Nao mabinti wa Jangwani sekondari walitambua kuwa wavulania wa Azania ni wao. Kwa hiyo akionekana binti wa Kisutu, Zanaki anamazoea sana na mvulana wa Azania jambo hilo lilileta tabu.”
Haya ananiambia mwalimu Selemani Sadalla ambaye wakati huo ailikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu Tambaza Sekondari.
Mwanafunzi huyo wa Tambaza akiwa na binti wa Jangwani alikutana na kundi la wanafunzi wa Azania, walimdhalilisha na kumpiga sana mbele ya binti wa Jangwani tukio hilo lilitokea Mtaa wa Mindu Upanga
Muendelezo wa tukio hilo, kijana wa Tambaza alikwenda kuwashitaki kwa wenzake kwa yaliyomkuta, hapo ndipo kilipotengenezwa kikosi cha wanafunzi kama kati ya 50-70 ambao ndiyo walifanya vurugu hiyo hapo Azania.
ili kuivamia Azania na kuwatia adabu. Kikosi kilisheheni silaha za mabomu ya petrol ambayo yalitengenezwa haraka haraka. Kisha kuelekea Azania. Wakiwa wanajiandaa kuondoka, Kutumia barabara ya Umoja wa Mataifa mwanafunzi mmoja aliwaambia kuwa pale mbele ya shule ya Azania kuna kituo cha Polisi.
Kwa hiyo waliamua kijana mmoja aende nje ya Hospitali ya Muhimbili palipokuwa na simu za TTCL za vibanda, mwanafunzi mmoja wa Tambaza alipiga simu Azania ya Mezani ya Mkuu wa Shule kuwa wako njiani wanakwenda kuiripua shule hiyo.
Simu hiyo iliwafanya Jeshi la Polisi kujipanga vizuri kupambana na ghasia hizo kwa hiyo Barabara ya Umoja wa Mataifa ulinzi ulikuwa mkali mno.
Kikosi maalumu cha wanafunzi wa Tambaza waliamua kubadili uelekeo na kuingilia Muhimbili Hospitali kisha kuingia Azania kwa mlango wa nyuma kutokea bonde la mto Msimbazi .
Jambo hilo lilikuwa gumu sana kwa vijana wa Jeshi la Polisi kudhani hilo lingefanyika, wanafunzi wa Tambaza walifanya hivyo kwa kuwa walikuwa wenyeji zaidi ya vijana wa Jeshi la Polisi. Tambaza walipita eneo la usawa wa wodi ya wagongwa wa akili na kuingia Azania. Jambo hilo lilisababisha taharuki kubwa shuleni Azania
Kwani tayari polisi walikuwa na taarifa na ulinzi uliimarika sana, hawakutegemea tena ujio ule baada ya kuridhishwa na ulinzi wa polisi imara wa wakati huo. Kuona hivyo Azania walianza kukimbia hivyo kuelekea upande wa shule ya jangwani huku wakipiga mayowe.
Tambaza kwa upande wao waliwakimbiza huku wakiwavurumishia mikwaju, mateke na ngumi. Kuona hivyo polisi waliwahi kuingia na kuwazingira baadhi ya wanafunzi wa Tambaza. Tambaza walilazimika kutumia silaha yao kubwa ili kujinusuru na kichapo cha polisi. Ndipo walipoamua kulipua mabomu yao katika maabara ya Azania.
Tatizo lilijitokeza katika zoezi hilo kwani waliopangwa kushika mabomu wakajikuta wako mbali na wenye vibiriti na kufanya zoezi kuwa gumu, lakini kama miujiza mmoja wao aliweza kurusha kibiriti hewani na kudakwa na mripuaji ambaye aliripua mabomu mawili, kuona hivyo polisi walivurugwa na kutoa mwanya kwa wanafunzi wa Tambaza kuponyoka kukimbia kupitia Bonde la Mto Msimbazi kwa kuogelea.
Kupitia Mto Msimbazi na kuibukia Magomeni ambapo zoezi la kurejesha taarifa kwa waliobaki shuleni ili kujinusuru na polisi lilifanyika.
Kwa wale wanafunzi wa Tambaza waliokuwa wanakaa Kariakoo walipofika nyumbani kwao walivaa sare za wadogo zao za shule zingine na kwenda Tambaza kupitia katikati ya jiji na kuingilia Palm Beach kuwajulisha wenzao juu ya hali ya hatari.
Hapa sasa Mwanakwetu hatua kadhaa zilichukuliwa.
Mosi, Kuvua sare na hasa mashati na kubaki na fulana za ndani, wakati mwingine walilazimika kuazima suruali kwa baadhi ya wanafunzi wa bweni wa Tambaza wa kidato cha tano na sita ili kurudi nyumbani salama.
Pili, Kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wa Tambaza anatembea kwa miguu kupitia njia za vichochoroni bila kutumia daladala ili kurejea nyumbani maana polisi wenye sare na askari walizagaa vituoni mithili ya siafu kuwasaka wanafunzi wa Tambaza.
Jeshi la Polisi lilikuwa linasimamisha daladala na chai maharage kisha kuanza kukagua kama kuna mwanafunzi yeyote wa Tambaza ili wamkamate.
Baadhi ya wanafunzi wa Tambaza walilala katika mabweni ya Kidato cha tano na sita na wengine kulala madarasani Tambaza na kurudi nyumbani siku ya pili ili kuacha mambo yatulie katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Huku wengine wakilala kwa wanafunzi wa Tambaza waliokuwa wakitokea Upanga, Muhimbili Palm Beach na Kariakoo, Posta na Keko.
Msomaji wangu hapo nilizungumzia suala la fulana za ndani, hizo zilikuwa na kazi kubwa mbili ya kwanza ni hiyo ya kujihami wakati wa vurugu na jingine ilikuwa jezi maalum kwa ajili ya kwenda kupigania chakula bwaloni wakati wa kula, kumbuka kuwa serikali wakati huo ilikuwa inatoa chai na chakula cha mchana kwa shule zote za kutwa za umma nchini.
Sasa ili shati isichafuke kila mwanafunzi wa Tambaza huvua shati kisha kubaki na fulana, tayari kupambania chakula, ukiwa wa kwanza unapata chakula kingi.
Mwanakwetu hayo yalikuwa maisha ya kawaida sana shuleni Tambaza na wengine walikuwa wanaenda mpaka Shule ya Forodhani, Kisutu na hata Zanaki kufuata chakula maana wao walipewa chakula kizuri kama cha nyumbani.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Haya ni maisha ya wanafunzi wa Tanzania muda mchache kabla ya mfumo wa vyama vingi haujatamalaki nchni Tanzania.
Mwanakwetu anajaribu kukusimulia yale aliyoyashuhudia wakati huo.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka,“Mgogoro wa Azania na Tambaza III.” Kipi kitaendelea subiri matini ijayo.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment