ANABAKI MSHINDI

Adeladius Makwega-MBAGALA

“Hii hali inatisha sana, mimi nilikuwa na desturi ya kudamka kila asubuhi kusali misa za asubuhi na jumapili nilikuwa nasali ibada ya misa ya kwanza iwe ya 12.00 au 12.30. Utekaji umenitisha. Hivi punde nimeacha kusali kwa utaratibu nilijiwekea lakini pia nimeacha hata kusali jumuiya maana ndani ya hizi jumuiya hizi nina mashaka , hakuna uhakika wa usalama kabisa, watu ninaokutana nao watu wana nia tofauti, wengine wanaweza kutumia jumuiya hizo kukusoma na kisha kunaweza kukuingiza katika shida. Nilikuwa natafuta akaunti ya Parokia yangu angalau niweze kuwa naweka fungu langu la kumi na pesa ya maendeleo, nikiipata nitafanya hivyo. Wana jumuiya wanaweza kuona kama ninanitenga lakini siyo hivyo. Kwa hali ilivyo ni vigumu kuweza kumjulisha Paroko wangu hali hii maana uelewa wa hali hii ya sasa unategemea sana kila mtu anavyoitazama hali hii ilivyo. Wako watu wapo katika hatari ya kutekwa kutokana na kazi zao na misimamo yao ya kisiasa pia. Nilipokuwa naongea na Mke wangu alinishauri angalau niwe nasali kwa kubadisha makanisa, nikamjibu kuwa kwa hali ilivyo watu wa siojulikana wanaweza kukufuata popote pale ulipo, lakini kuweka usalama binafsi ni jambo la msingi.”

Wadau wanatoa ushahidi huo lakini je Kanisa lenyewe linatambua hali hii? Jambo zuri Askofu Dkt. Gwajima ameliwakilisha vema kanisa na hii si kwa bahati mbaya nadhani kutokana nayeye kuwa katika Kanisa na kuwa ndani ya Bunge na kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.Kwa hakika Tanzania sasa inao viongozi wengi wa dini lakini wanashinda kuona na kuyafahamu mengi kutokana na kuwa nje ya mfumo wa siasa, ukiwa ndani ya siasa unaona hadi sura za hawa wanaofanya maamuzi, wana msimamo gani katika hili na lile ndani ya vikao vya ndani na sura zao na misimamo wao wakiwa nje ukoje ? 


 

Je wana nia njema? Hapa Askofu Dkt Josephart Gwajima ameitumia vizuri fursa hii, ameitumia vizuri karata hii.Kwa wale Wakristo Wakatoliki nawaomba wakumbuke kisa hiki,

“Padri Ernesto Cardenal ambaye alijiingiza katika siasa za taifa lake la Nicaragua hadi akawa Waziri wa Utamaduni wa taifa hili yeye na nduguye ambao wote walikuwa mapadri, hali hii ilisababisha Kanisa Katoliki Ulimwenguni enzi ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II (Mtakatifu Yohane Paulo II ) kuwasimamisha utume wao Padri huyu na nduguye na badaaye Padri Ernesto Cardenal alipohojiwa juu ya hili alisema ni kweli amesimamishwa lakini Kanisa lilikuwa na wajibu wa kuona zaidi  ndani ya wanasiasa kuna nini? Hasa namna wanavyofanya siasa zao na hali ya taifa ya matifa yao zilivyo lakini baadaye Padri Ernesto Cardenal alirejeshewa Utume wake lakini akiwa kitandani mgonjwa siku chache kabla ya kufariki dunia.”

Msomaji wangu nakuomba ufahamu kuwa Padri Ernesto Cardenal aliadhibiwa na Kanisa Katoliki kwa kuchanganya dini na siasa na Baba Askofu Dkt Josephartt Gwajima anaadhibiwa na chama chake kwa kile kile anachanganya dini ya siasa.


 

Kwa sasa yako maneno ambayo hayana maantiki kuwa hata kama Baba Askofu Dkt. Josephart Gwajima angefanya kosa basi angefungiwa yeye na siyo kanisa. Haya maneno haya maana yoyote maana hauwezi kulitenganisha kanisa na binadamu na ndiyo kile kile hauwezi kumtengaisha mwanadamu na dini siasa haya mambo yanakwenda pamoja, iwe kumfungia mtu au kufungia nyumba ya ibada yote hiyo ni kosa ambalo halipaswi kuhalalishwa na mtu yoyote yote anayeheshimu uhuru wa kuabudu.Mwanakwetu anaamini Kanisa ni watu yaani mimi na wewe na lile jengo ni pahala tu tunapoingia kusali maana hata familia yako wewe, mkeo na watoto ni kanisa. Mwanakwetu anaamini kulifunga lile jengo ni kosa na hata kumgusa na kufanya chochote kuhani wa Mungu ni kosa maana kwa alichosema Baba Askofu Dkt.Gwajima ni kitu cha haki,kumnanga, kumsonfa kidole au kumkebehi Dkt Gwajima ni shambulio dhidi ya uhuru wa kuabudu.Kwa hali ilivyo sasa hadi sasa, nakwambia hadi sasa Mwanakwetu anaamini Mshindi ni Baba Askofu Gwajima.

Watu wengi siku hizi wanaelewa unapotaja kanisa wakimaanisha ni jengo. Huko si kuelewa kibiblia maana ya kanisa. Neno ‘kanisa’ maana ya asili yatokana na neno la Kiyunani ekklesia lililo na maana ya ‘kusanyiko’ au ‘walioitwa.’

Maana ya asili ya ‘kanisa’ sio lile jengo, bali ni watu. Mara nyingi unapowauliza watu jamani mnasali kanisa gani? Mara nyingi huwa wanajihushisha na jengo Kanisa Katoliki la Mitume la Mtakatifu Josefu Mfanyakazi, Kanisa Katoliki la Bikira Maria Imakulata , Kanisa la Angilikana la Mtakatifu Petro Bunda Mjini.

Kitabu cha  Warumi 6:5 kinanadi kuwa ‘Kanisa ni mwili wa Kristo, ambapo yeye ndie kichwa. Waefeso 1:22-23 yasema, ‘Akivitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.’Mwili wa Kristo umejengwa na wanaoamini katika Yesu Kristo toka siku ya Pentekosti, rejea kitabu cha Matendo Ya Mitume.

Haya msomaji wangu ni ndani ya Biblia kikubwa Kanisa ni mimi na wewe.


 

Nakuomba msomaji wangu nikurudishe kwa Baba Askofu Dkt. Gwajima yeye kwanza kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kwa ushahidi uliopo Watanzania wengi tunatambua msimamo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia ambaye mkoa anaotokea ni Mbeya na ndugu zake wawili Shedrack Chaula na Mdude Nyagali ni miongoni mwa waliopotea na hadi sasa haijulikani wapo hai au wamekufa, huku kwa kumbukumbu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaonesha masikitiko kidogo kwani wapo wabunge, wapo wabunge, wapo wabunge waliojaribu kuupenyeza mjadala juu ya watu wasiojulikana na hili limegonga mwamba na haya yalitokea kabla hata hawa ndugu zake wawili Chaula na mdude hawajapotea.

Baadaye jamii ya Mbeya na Songwe ilikutana na mpoteo wa Shedrack Chaula na Mdude Nyagali huku katika mojawapo ya mahojiano yake na vyombo vya habari Dkt Tulia ananukuliwa kwa sauti yake akiyasema maneno haya.

“Hoja ya ninasikia ninasikia, Bunge haliwezi kuketi na kutoa maamuzi, kwa hiyo ni hivyo…”

Haya ni ya hivi karibuni lakini sauti ya Dkt Tulia zimerekodiwa akiwa katika Bunge letu Tukufu mara kadhaa akiweka kigingi katika hoja ya utekaji na sauti yake ya mwanzo kabisa ilikuwa na maneno haya,

“Waheshimiwa Wabunge nawauliza, Wabunge, hili ni swali la Waziri Mkuu au la Kisekta? Leo asubuhi nimesoma kuna mganga amezika watu, je hivi ni vyombo vya dola? Haya mambo yakisemwa kwa hisia inaonekana watu hawajali, tusioneshe mazingira kuwa kila anayepotea ni chombo cha dola kimemchukua….ukitumia mihemko hautoi nafasi ya mambp haya kufanyiwa kazi…”

Katika hali kama hii Mwanakwetu anaamini kuwa hata kama Askofu Dkt. Gwajima angeitaka nafasi ya kulisema hili ndani ya vikao vya Bunge, nafasi haipo na mlango umefungwa kabisa na kufuli la shaba na hata kama Askofu Dkt. Gwajima kama aliomba hii nafasi Bungeni maana yake alinyimwa. 


 

Msomaji wangu kumbuka sana HATA KAMA mara mbili. Sauti za waliotekwa na kuuwawa na wale ambao hawajulikani walipo hadi leo zinabaki katika ulimwengu wa digitali huko zikiendelea kulia na kuwatoa machozi; ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote. Ndugu hawa kama wamekufa basi ni vizuri maiti zilipozikwa hawa zifahamike ili ndugu wa jamaa hao wapate nafasi ya kuzisalia maana kwa hali ilivyo kama hawa jamaa wamekufa basi wamezikwa kama mbwa, hapa tunanyima haki za kiimani za wanaopotezwa. Sauti za walipotea ni nyingi mojawapo ni ya Mdude Nyagali.

“Siku ya jumamosi kulikuwa na hakuna umeme mimi nilikuwa bize sana na laptop , nikaona gari nje, wakaja wakanikamata, nikajikuta nipo huku porini…”

Sauti hizi kwa hakika zinalia katika masikio ya Watanzania wengi lakini wapo Watanzania ambao pengine hawajabarikiwa kuvikisikia vilio hivyo japokuwa vinagonga katika ngoma ya masikio yao, lakini lakini na lakini Mungu bahati Baba Askofu Dkt.Gwajima Mungu amemjalia kusikia kilio hiki. Swali ambalo linabaki hali ya kutekana inaendelea huku viongozi wa dini zote sasa wanafikiwa na watekaji, je nani yu salama? Mwanakwetu anaamini kuwa watekaji bado wako kazini na yule anayejiona yu salama atambue kuwa hayupo salama, Tanzania imekuwa msitu tunawindana na kama wanyama?


 

Kwa hakika ndani ya siasa kuna mambo mengi, unapotazama kwa jicho la mbali kwa kusimuliwa unaweza ukawa na mtazamo mwingine na unapoyaona kwa ndani wewe mwenyewe unaweza kuwa,

“Kwa sasa Baba Askofu Dkt. Gwajima ni mwanaCCM, ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, hiki kikiwa kikao  cha juu namba mbili katika vikao saba vya ngazi za juu vya CCM taifa. Unapokuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa kwa hakika unaingia vikao vingi vya juu ya CCM pengine kuliko mwanaCCM yoyote Yule, ikiwamo Mkutano Mkuu wa CCM Taifa. Kitendo cha kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka hadharani na kulalamikia hoja ya utekaji kina maana kubwa kuwa CCM haijadili ajenda hii ya utekaji kabisa na kama ajenda hii ingejadiliwa katika vikao ambavyo Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa wanaingia, Wajumbe wenzake na Gwajima wangeijibu hoja hii na siyo mwenyekiti wa CCM Taifa na kujibu hoja hii kwa kuibeza.”

Mwanakwetu anaamini kuwa inawezekana Kamati Kuu ya CCM Taifa ambacho siyo kikao cha juu kabisa cha CCM Taifa, ajenda ya matukio ya utekaji na udhalilishaji na mauwaji  inajadiliwa na kuishia hapo na hilo ndilo kosa  maana Kamati Kuu siyo kikao cha mwisho cha CCM Taifa. Hata hivyo kamati kuu ni kikao cha watu wachache ambao peke yao hawezi kuisadia CCM kufikia shabaha yake wakati mgumu kama huu. Mwanakwetu anaamini kile kile kilichofanyika Bungeni ndiyo kilichofanyika katika vikao vya Chama kwa ngazi zote ambalo hilo ni kosa kubwa kwa Bunge na kosa kubwa kwa chama cha siasa kinachoitwa Chama Cha Mapinduzi.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kikubwa msomaji wangu tilia maanani mambo makubwa matano; kwanza hoja ya Utekaji Bungeni, Hoja ya utekaji ndani ya CCM, pia nafasi ya Baba Askofu Dkt.Gwajima ndani ya vikao vya ngazi ya juu vya CCM na nne tilia maanani msimamo wa Askofu Dkt.Gwajima juu ya kupinga utekaji na jambo la mwisho la msingi tilia maanani mno kupigwa mkasi kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima.


 

Msomaji wangu kumbuka kuwa miongoni mwa maneno muhimu sana yaliyosema na Baba Mtakafifu Fransisko akiwa hai ni haya;

“Mchungaji lazima anukiee harufu ya kondoo wake, kiatu cha Kanisa lazima kiwe na matope mengi.”

Kama inavyoonekna sasa mara Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Padri Charles Kitima kashambuliwa, mara kanisa la Ufufuo na Uzima limefungwa, mara mchungaji fulani katekwa. Haya yanatokea kama Kanisa linashugulika na mambo na waamini wake kama kanisa halifanyi hivyo haliwezi kunuka harufu ya kondoo wake na wala viatu vya kanisa haviwezi kuloanishwa kwa tope.


 

Mwanakwetu upo? Kumbuka

“BABA ASKOFU GWAJIMA ANABAKI MSHINDI.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257








 




 

 

 



0/Post a Comment/Comments