WAPI JAMANI MNATUPELEKA

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Ni wakati mwingine siku nyingine, Mwanakwetu anakualika tena msomaji wake katika Makala ya Katuni, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi yanayoteua katuni nne, kisha moja baada ya nyingine kuelezewa namna ilivyo, alafu katuni hiyo inaelezewa namna ilivyo kiuchambuzi kwa jicho la mtayarishaji wetu.

Kuyaanza makala haya siku ya leo Mwanakwetu akiwa kidhania katika geti la kuingia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya ndugu Juma Zuberi Homera, hapa hapa getini anaikamata katuni ya kwanza iliyochorwa na ndugu Msamba ambayo inawaonesha jamaa wawili wanazungumzia jambo. Mmoja anasema, haya mauwaji yafike mwisho na mwezake anajibu ili tuwajibike na kufungua ukurasa mpya wenye amani.


 

Mtayarishaji wa makala haya anaona fika kinachopigiwa chapuo ni kukomeshwa suala la Watanganyika kutekwa, kupotea na kuuwawa na jambo hili limekuwa kero na hata Jumuiya za Kimataifa zimeanza kulitazama taifa la Tanzania katika jicho lingine. Mathalani hivi karibuni Bunge la Umoja wa Ulaya limejadili suala hili na hata kuyataja majina ya viongozi wa Tanzania wenye dhamana ya uongozi na Watanzania waliotekwa, kuuwawa katika matukio haya haya ya utekaji na kumekuwa kimyaaa ziiii hakuna aliyekamatwa.

“Euro milioni 160 zimetumwa kwa ajili ya msaada kwa Tanzania, Euro milioni 107 za ziada kwa taifa hili linaloongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan anayeongoza chama cha kijamaa katika taifa hili la Afrika Mashariki tangu mwaka wa 2021.Wakati Rais Samia anaingia madarakani hakuwa hivyo alivyo sasa, japokuwa tunatoa msaada wote huo, alitekwa na kuuwawa Ali Mohammed Kibao mwanasiasa wa Upinzani.

 

Kama hilo halitoshi Mwanasiasa wa Upinzani kutokaa CHADEMA Tundu Lissu amekamatwa na kutupwa Kolokoroni kwa tuhuma za uhaini ambayo hukumu yake ni kunyongwa. Kwa utulivu wa taifa hili , utulivu wa nchi husika na kwa maslahi yetu vile vile , ili kuilinda nchi hii dhidi ya umaskini wa kutisha, unaoisumbua, ili kutulinda na uhamiaji na ukimbizi kutoka nchi hiyo, inabidi tupime ni aina gani ya msaada unaotolewa kwa Tanzania hasa kwa kuzingatia haya kwa hili tunalolijadili, asante sana.”

 

Haya ni maelezo ya Profesa Thomas Fischer Mkuu wa Idara ya Mikakati ya Kisiasa katika Bunge la Umoja wa Ulaya, humo humo Bungeni Mei mwaka wa 2025.


 

Mwanakwetu sasa anaingia kidhaani getini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Wa Mbaye huku akikumbuka kupotea kwa kijana Shedrack Chaula Agosti mwaka wa 2024. Hapa hapa Mwanakwetu anapiga hatua ya kwanza, anapiga hatua ya pili na anapiga hatua ya tatu alafu anafungua kapu lake la katuni, leo hii anaikamata katuni ya pili iliyochorwa na King Kinya, hapa kunaonekana kijana aliyevalia fulana yake vizuri, huku mkono wa mtekaji aliyevalia suti maridadi ukiwa umemziba mdomo. Mwanakwetu kwa kumtazama kijana huyu aliyezibwa mdono labda ni mwana habari ambaye pengine anayoandika na kuyatangaza hayamridhishi aliyevaa suti na hivyo kufanikisha kumziba mdomo ndugu huyu baada ya kumteka.


 

Kwa kuitazama katuni hii hasa kwa kutumia jina la mchoraji nadhani hii ni Tanzania ya mwaka wa tangu 2015 hadi 2025 ambapo matukio ya utekaji yamepamba moto. Mwanakwetu anauliza Jamani Tunakwenda Wapi? Jamani Mnatupeleka WapI?. Mtayarishaji wa makala haya leo hii anaipaza sauti yake kwa kiwango cha juu na kusema kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama na hata vile vya uchunguzi vitimize wajibu wake ili kuipa utulivu jamii ya Watanzania, vinginevyo hali hii ya malalamiko isiyokwisha haina afya kwa taifa la Tanzania, maana taarifa za Watanzania wenyewe tunalalamika na taarifa za nje ni kilio juu ya matukio haya ya utekaji, upoteaji na mauwaji.  Huku Bunge la Ulaya likishangazwa na hali halisi ya yanayofanyika hivi sasa hapa Tanzania, jamani kuna nini?

 Ndugu zangu watu wa Ulaya, nilipokuwa mtoto mdogo, niliwahi kujifunza juu ya Tanzania maana baba yangu mzazi alikuwepo huku, baba yangu alijifunza juu huduma za matibabu kwa kutumia dawa za asili, kwakupitia huduma za madaktari wasio na mipaka wakiwatibu Watanzania.Baba alirudi nyumbani na picha nzuri na hata na mbinu za kizamani za matibabu, hii ilinionesha watu wa Tanzania wenye furaha, wenye utamaduni mzuri na wenye utajiri wa upendo walionao wenyewe kwa wenyewe. 

Tanzania yenyewe ikiwa kisiwa cha amani na utulivu. ukilinganisha hayo na sasa kwa Tundu Lissu, kiongozi wa upinzani amewekwa mahabusu, anakabiliwa na shitaka la uhaini na hukumu yake ni kifo na hiyo ni makosa . Siku zote hizo kwa moyo wangu wote naunga mkono uharaka huu wa jambo hili na nampa pongezi tele mwandishi wa taarifa hii hii muhimu.

 Huyu jamaa ni wa bunge la Ulaya anashangaa hiki kinachoendelea Tanzania, sivyo na alichokiona katika picha za Baba yake aliyewahi kufanya kazi na Waganga wa Jadi. Kwa hakika viongozi wa Tanzania ya leo watambue kuwa wapo watoto kutoka mataifa mengine wazazi/walezi wao wanaofanya kazi mbalimbali hapa Tanzania kwa sasa. Sasa macho yao yanaona maiti za watu waliotekwa na kuuwawa, je watoto hawa wakiwa wakubwa wataizunguimziaje Tanzania yetu ya tangu 2015-2025? 

 


Kwa  hili Mwanakwetu anasema wazi kuwa mambo haya lazima viongozi wetu wayafanyie kazi na tena kwa haraka.Mwanakwetu sasa anaingia kidhaania katika mapokezi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na hapo hapa anakutana na jamaa kadhaa katika foleni , hapa hapa tena  anaikamata katuni ya tatu iliyochorwa na Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, ambapo kunaonekana jamaa aliyevaa sare za Jeshi la Polisi la Tanzania. mkono mmoja wa huyu jamaa una maneno wachunguzi na mkono wa pili unasema tuhuma. Jamaa kando wanashangazwa inakuwaje mwenye kutuhumiwa pia ndiye mchunguzi? Askari huyu anasema tumeanza uchunguzi juu ya kupotea Mdude Nyagali.

Katika hili Mtayarishaji wa makalahaya anasema wazi kuwa suala hili linahitaji jitahada za pamoja baina ya
viongozi katika Mkoa wa Mbeya hasa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mwneyewe, maana Juma
Zuberi Homera ndiye mwenye dhamana na Ulinzi na Usalama wa watu wa Mkoa wa
Mbeya kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa. Mwanakwetu anaamini
kama Mkuu wa Mkoa wa Mbeya atambue kuwa akina John Mwakangali waliopambania
uhuru wa taifa hili ili wananchi wake wawe huru na usalama wa raia ni mojawapo
wa kipengele cha watu huru.

“Kweli Watanzania miaka 61 ya Muungano tunatekana? Tunauwana? Binadamu ni kiumbe kinachoweza kuomba msamaha, kulalamika, kuomba radhi, inakuwaje wewe bedui, wewe haramia unamua binadamu mwenzako?

Kwa sasa ndiyo maana Bunge la Ulaya limekwenda mbali hadi kusema Hukumu ya Kunyonga hadi Kufa nchini Tanzania iondoleww ambalo hilo ni hoja halali na hoja sahihi.”

Mwanakwetu anarudia kushauri kuwa kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi dhidi ya watu kupotea na kuuwawa akiwamo kijana Shedraki Chaula hapo mkoania Mbeya. Mwanakwetu sasa anakutana na katuni ya nne ambayo imechorwa na Masoud Kipanya ambapo kuna kaburi lililochimbwa vizuri, kisha yupo jamaa amelala katika kaburi hilo huku akisoma gazeti la michezo. Kwa kuitazama katuni hii kinachoonekana ni hali ya mchimba kaburi kamaliza kazi yake, huku juu ya kaburi rangi ikiwa juu imemwagika hovyo hovyo, mchimbaji akingoja maiti ya kuzikwa pengine ije. Swali la kujiuluza inawezekana pengine huyu huyu msomaji wa magazeti ya michezo akazikwa yeye, maana alitakiwa kukaa kwa umakini katika kaburi hili. 


Mwanakwetu anapoitazama katuni hii anakuja na taswira nyingi, je huyu aliyelala kaburini na akisoma gazeti ni mchimbaji wa kaburi au ndiyo maiti nyenyewe. Mwanakwetu hana majibu kikubwa na la msingi, inawezekana huyu msomaji wa gazeti la michezo ndiyo maiti.

Mwanakwetu upo?

Basi hadi hapo ndiyo na mimi natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka nilikuwa na katuni nne, hapa hapa kidhaania katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambapo katuni karibu tatu zinazungumzia suala la utekaji wa watu nchini Tanzania isipokuwa katuni ile ya mwisho inayogusia juu ya maiti inayohangaika kusoma habari za michezo gazetini.

Kumbuka

“WAPI JAMANI MNATUPELEKA WAPI”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius @gmail.com

0717649257

NB–Makala haya yametayarishwa siku ya leo na Mwanakwetu kwa heshima zote kwa  nduguye wawili; Mkomangi Gerald Mkundi, Mmatumbi wa MBAGALA na Bi Rebeka Rwetiko wa Dodoma Tanzania.


 

 







0/Post a Comment/Comments