NATAMBUA NAMNA NILIVYOZALIWA

 

Adeladius Makwega- Mlali, Kongwa-DODOM

Aprili 9, 2018 nilifanya safari yangu kutoka Lushoto kuja hapa Dodoma nikiwa mimi pamoja na dereva mmoja anayefahamika kama John Kyando (Mhehe Mbondei). Safari hii ilikuwa ni kuitika wito wa Waziri wa TAMISEMI wakati huo Ndugu George Simbachawene. Kikao kilikuwa cha dakika chache sana hazikuzidi dakika 45 tukakimaliza ofisini kwa Waziri nikatoka nje. Tukakubaliana na dereva kuwa siku hiyo tusilale Dodoma bali tukalale Manyoni, tukiendelea na safari ya kurudi Lushoto, mkoani Tanga kwa kupitia njia ya Babati, Arusha Kilimanjaro kisha Tanga.


 

 

Tulipotoka pale TAMISEMI-Mkapa House saa 4.15 ya asubuhi, wakati huo Mji wa Serikali ulikuwa bado unajengwa na ilipotimu saa 5.20 asubuhi tukawa Manyoni Mjini, nikafika kwa bibi yangu mzaa mama ambaye anaitwa Elizaberth Mwimba(mdala Eliza) Ukapikwa ugali vizuri sana ukalika, nikawa naongea na bibi yangu hadi jioni, tukala chakula cha jioni naye dereva akaenda kulala Manyoni Mjini, mimi nikabaki kwa bibi tunaongea mambo mengi mengi ya dunia hii, kwa kuwa mama yangu mzazi wakati huo alishafariki, bibi mzaa mama nikiongea nae napata amani na faraja kubwa nikimkumbuka marehemu mama yangu mzazi, mazungumzo naye yalinoga sana.


 

 

Hapa tulipokuwa tumekaa palikuwa na runinga ya chogo ndogo tunatazama taarifa ya habari tukasikia,

 

“Askofu Zakaria Kakobe ahojiwa na uhamiaji juu ya uraia wake.”

 

Huo ulikuwa ni muhtasari wa taarifa ya habari, wakati msomaji wa habari hiyo anasoma muendelezo wa habari hiyo, Askofu Kakobe mwenyewe alionekana akieleza juu ya namna alivyoyajengea makaburi ya wazazi wake ndani ya nyumba yao ili yasipoteze ushahidi wa uraia wake.


 

 

Bibi yangu huyu mwenye uelewa mkubwa sana akaniambia unamuelewa Baba Askofu Kakobe anavyoelezea juu ya uraia wake? Nikamjibu nimesikia na nimemuelewa. Bibi akaniuliza kweli mjukukuu wangu umemuelewa Baba Askofu? Nikasema bibi nimemuelewa. Bibi akaniambia mtu anapotaka kujua uraia wako, tafsiri yake wewe unayeulizwa ueleze namna ulivyozaliwa. Akaniuliza wewe mjukuu wangu mtoto wa binti yangu wa kwanza unajua namna ulivyozaliwa? Nikamwambia mimi nafahamu baba yangu ni nani, mama yangu ni nani, tarehe niliyozaliwa na pahala nilipozaliwa. Bibi yangu akasema hiyo haitoshi, hata mkimbizi anaweza kuwa na hivyo vitu vyote ulivyovitaja na akasema yeye ni Mtanzania kumbe mgeni.

 

“Swali hilo ni gumu sana, si swali la heshima kuulizwa mtu mzima bali sasa hakuna budi kuulizana, mzazi anaweza kueleza namna mtoto wake alivyozaliwa, lakini si mtoto mwenyewe. kueleza namna alivyozaliwa kidogo inakuwa ngumu sana na wengi hawajui hilo.”

Mdala Eliza anaendelea kuongea.


 

 Aliyevaa shati jeusi na kaptula mikono mfukoni ni baba wa Mwanakwetu hiyo Mafia Krisimasi ya mwaka 1968

Nikamuuliza kwa nini? Akasema,

 

“Wakati wa ukoloni watu walikuwa wakisafiri umbali mrefu sana kwenda kutafuta vibarua vya kulima na kuchunga ng’ombe, binafsi baba yangu mzazi alifika maeneo ya Bonde la Ufa-Kilimatinde Manyoni jirani na Dodoma kutafuta kazi hizo akitokea huko Iringa-Uheheni. Alipofika hapo akapata kazi akaanza kuchunga ng’ombe na kulima, kwa kuwa alikuwa kijana akatafuta mchumba akamuoa ndipo nikazaliwa mimi (mdala Eliza) na kaka yangu mmoja.”

 

Nikamuuliza sasa bibi kwa hiyo wewe ni Mhehe akajibu ndiyo kwa baba Mhehe lakini mama ni Mgogo, bali Ugogo umekuwa na nguvu zaidi ya Uhehe kwa kuwa baba alikuja huku. Nikamuuliza wewe simulizi hii kakusimulia nani?Akanijibu bibi yake mzaa mama.

 

Hapo Mwanakwetu taarifa ya habari inaendelea. Nikamwambia bibi kama wewe ulisimuliwa na bibi yako habari hiyo basi na mimi nisimulie na mimi mambo yalikuwaje?

 

“Akacheka sana kasha akasema kati ya mwaka 1970 -1974 yeye(mdala eliza) na mumewe Hezron Mlemeta walikuwa wakifanya kazi Chuo Maendeleo Murutunguru sasa ni chuo Ualimu Murutunguru Ukerewe–Mwanza na binti yao mkubwa Dorith Mlemeta akisoma hapo badaye, alipomaliza mafunzo ya ualimu chuoni hapo binti yao alipata ajira ya serikali wilayani Mpwapwa-Dodoma katika Kijiji cha Ujamaa Tambi (sasa ni Kongwa).

 

Mwalimu Doroth akiwa binti mdogo akaripoti kituo chake cha kazi mwaka 1971, kumbuka wakati huo Julius Nyerere na harakati zake za vijiji vya ujamaa zinapamba moto. Mwalimu huyu mwaka 1971 akaanza kazi na kupata likizo yake ya mwaka, akarudi kwa wazazi wake Mwanza, mwaka 1972 hivyo hivyo na wakati huo likizo za watumishi wa umma zinalipwa kila mwaka hakuna kukopwa. Tangu mwaka1970 serikali ilikuwa inawapeleka walimu wengi wapya shuleni kuanzisha shule na vijiji vya ujamaa kila kona ya taifa letu lakini kwa kuwa wakati huo ulikuwa ni kipindi cha oparesheni vijiji vya ujamaa maeneo mengi hayakuwa na vijiji wala shule, kila mmoja akiishi pahala pale na shamba lake. Kwa hiyo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwatumia baadhi walimu wengi wapya ambao walipotoka vyuo cha ualimu walienda JKT, huko wakapangia mikoa ya kufanya kazi.

 

Kwa walimu hao wakatumika vizuri katika oparesheni vijiji vya ujamaa kuhamisha watu kutoka mashambani hadi vijijini. Katika zoezi hilo Mwalimu Francis Makwega alishiriki katika maeneo ya Handali na vijiji vinginevyo jirani mkoani Dodoma.Kazi hiyo ilipokamilika walimu hao wakapangiwa vituo vya kazi maana baadhi ya maeneo shule za muda zilijengwa. kuwepo, Mwalimu Francis Makwega akapangiwa Shule ya Msingi Tambi ikiwa katika Kata ya Mlali wilaya ya Mpwapwa.Kwa kuwa tulikuwa Mwanza na sisi tuna asili ya Singida–Dodoma, tunafahamu hali ya Dodoma ilivyo kuhusu mboga, kutokana na ukame, nilikuwa ninanunua samaki na dagaa ninawakaanga na ninawafunga katika mabokisi ninamtumia binti yangu(mwalimu Dorith) kwa njia ya posta hadi Tambi”

 

Mdala Eliza anasema alikuwa na desturi hiyo tangu mwaka 1971 naye bintiye akiwaandikia barua kuelezea hali ya maisha ilivyo na kuwa amepokea samaki waliotumwa huku wakimsaidia sana kwa mboga.


 Binti katikati ya wachungaji, gauni lenye madoa madoa na kilemba ni mama wa Mwanakwetu MWANZA 1972

 

Mwaka 1973 ulipita japokuwa mdala Eliza alituma mzigo wa samaki kwa bintiye hakupata majibu yoyote kuwa mzigo umepokelewa, likizo ilipofika bintiye hakwenda Mwanza, mawasiliano yakapotea. Hilo lilipotokea tu wazazi wakatilia shaka, kulikoni huko Mpwapwa?

 

Mdala Eliza akaomba ruhusa kazini kwake kwa mkuu chuo akaingia katika galimoshi kutoka Mwanza hadi Gulwe akashuka, akapata usafiri hadi Mpwapwa wilayani, alipofika hapo akaambiwa mwalimu huyu yupo Shule ya Msingi Tambi na huku anaendelea na kazi vizuri. Mdala Eliza kichwani mwake swali la mbona mawasiliano na mwanetu yamekufa, liliendelea kumuumiza.

 

Alipofika Kijiji cha Ujamaa Tambi alimuona mwenyekiti wa kijiji wa TANU akajitambulisha, mwenyekiti alimjibu kuwa Mwalimu Dorith yupo anatufundishia wanetu vizuri, Mwenyekiti alimpeleka Mdala Eliza hadi kwa mkuu wa shule, akaitwa mwalimu Dorith ofisini. Mdala Eliza alijiuliza kwa nini hawa walimu wasinipeleke nyumbani kwa binti yangu? Kwa nini wamuite hapa kwanza? Mdala Eliza hakupata majibu, lakini aliona kuwa hilo lilikuwa ni jambo la heshima siyo uugwana unakwenda nyumbani kwa mwanao unakutana na wakwe. Mwalimu Dorith alifika na kumchukua mama yake hadi katika nyumba yake ya shule aliyokuwa anaishi.

 


Kijiji cha Ujamaa Tambi walijitahidi kuwa na nyumba za walimu kwani mwalimu Dorith alipewa nyumba yenye vyumba vya kulala viwili na sebule. Mdala Eliza akakaa na binti yake kwa siku kadha na kumuuliza haya kulikoni mwaka 1973 umepita likizo haujakuja Mwanza?Huu ni mwaka 1074 au huku Dodoma umepata wazazi wengine? Akajibu hapana nyinyi ni wazazi wangu.

 

Lakini Mdala Eliza alipokuwa pale akagundua jambo maana shikamoo kutoka kwa mwalimu mmoja anayefahamika kama Francis zilikuwa nyingi sana. Mdala Eliza akajipa moyo wa uvumilivu wa muda ili aweze kufahamu kulikoni? Baada ya siku kadhaa alibaini kuwa kuwa tayari binti yake alikuwa mjamzito, akang’amua kuwa ndiyo maana likizo za Mwanza zilikwenda na maji.

 

Mdala Eliza akamwambia binti yake muite huyo mwalimu Francis mwambie nina mazungumzo naye. Kweli Mwalimu Francis aliitikia wito na kuungama kuwa ujauzito huo ni wake. Akamuuliza wewe kabila gani? Francis alijibu kuwa yeye ni Mpogolo anatokea Mbagala Dar es Salaam lakini kwao kwa asili ni Mahenge_MorogoroMdala Eliza akasema sawa, wewe Mpogolo mambo yameshaharibika inakuwaje? Mpogolo akajibu mimi nilishawaambia wazazi na likizo nakuja kulipa mahari na kufunga ndoa,

 

Mwanakwetu kweli ilikuwa hivyo hivyo, likizo ilifika, ndoa ilifungiwa Kanisa Katoliliki Parokia ya Murunguru-Nasio Ukerewe Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza wakati huo sasa ni Jimbo Katoliki la Bunda..

 


 

Kumbuka msomaji wangu hayo ninasimuliwa na Mdala Eliza sebuleni kwake, taarifa ya habari ilishaisha muda mrefu na sasa ni saa  4 ya usiku, bibi akasema sasa hivi ni usiku sana ukalale mjukuu wangu kesho muanze safari ya kurudi Lushoto mapema.

 

“Kabla yakwenda kulala tusali ili niombee na safari yako ya kesho.”

 

Bibi yangu huyu ni Muangilikani mzuri sana alisema , akasali pale akaiombea safari, alipomaliza tukaitiki amina akasema sasa kalale.

 

Nikamwambia mbona haujaimalizia hii stori, bibi akasema binti yangu alijifungua mtoto wa kiume ambaye ni wewe, huyu aliyesababisha mwanangu kutokuja likizo ni wewe, huyu aliyesababisha nikapanda gali moshi hadi Gulwe ni wewe, Huyo aliyesababisha binti yangu kutokujibu barua za maboksi ya samaki ni wewe, kumbe huyo aliyesababisha mwanangu akapoteza mawasiliano na sisi ni wewe.


 

 

Nikacheka sana tukaagana nikaenda kulala. Kweli kulipokucha mimi na dereva wangu John Kyando tulirudi Lushoto.mkoani Tanga

 

Mwanakwetu, Je na wewe unatambua ulivyozaliwa? Kumbuka kutambua zaidi ya majina ya wazazi, tarehe na pahala ulipozaliwa.

Unajua msomaji wangu Mwanakwetu anazaliwa kutokana na mambo haya haya ya siasa za ujamaa nchini Tanzania na ndiyo Mwanakwetu anakuwa mkali pale anapoona mtu anapofanya siasa za kitapeli kwa Watanzania, huwa anatamani amcharaze bakora huyu tapeli na laghai maana bila ya siasa za Ujamaa na Kujitegemea pengine Mwanakwetu angezaliwa Mbagala na saa hizi angekuwa anakwea minazi na kunywa pombe ya mnazi au angezaliwa Mahenge sasa anang’atwa na ruba katika majaruba ya mpunga akilima mpunga na kuska samaki au angezaliwa  Manyoni sasa angekuwa anachunga ng’ombe zake. Wazazi wake wamekutana, na yeye kuzaliwa kwa sababu ya siasa hizi hizi ndiyo maana anasema siasa za kitapeli hazifai.

Kumbuka Natambua Namna Nilivyozaliwa.

Nakutakia siku njema

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257 















 

 

0/Post a Comment/Comments