MWALIKO WA KUWA WASTAHAMILIVU

 


Adeladius Makwega Tarime MARA

Ni siku ya Jumamosi Aprili 12, mwaka wa 2025 nyumba jirani na alipo Mwanakwetu anasikia kelele ya jamaa anayekata matawi ya mti unaofanana na mnazi. Baadaye anaona kundi la vijana wakibeba matawi ya mti huo, walipoulizwa walijibu wakisema wanakwenda nayo kanisa maana Jumapili ya Aprili 13, 2025 ni Jumapili ya Matawi.

“Jumapili ya Matawi/Mitinde ni sikukuu ya Kikristo ambayo huangukia Jumapili moja kabla ya Pasaka. Sikukuu hii ni ukumbusho wa kuingia kwa ushindi  na kishindo kwa Kristo Jijini Yerusalemu, tukio hili linatajwa katika kila moja ya Injili nne katiba Bibilia. Jina lake linatokana na matawi ya mitende yaliyopeperushwa na umati wa watu kumsalimia, kumlaki na kumtukuza Yesu Kristo alipoingia Jijini Yerusalaam.”

Jumapili ya Mitende huadhimishwa kwa baraka na usambazaji wa matawi ya mitende (au matawi ya miti mingine ya asili), inayowakilisha matawi ya mitende ambayo umati uliyatawanya mbele ya Kristo na kumpungia Yesu Kristo alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu. 

Mitende hii wakati mwingine hufumwa kuwa na umbo la misalaba lakini ugumu wa kupata mitende katika hali mbaya ya hewa ulisababisha kubadilishwa kwa matawi ya miti ya asili, kama vile mizeituni, mierebi, minazi, michikiti ukindu nakadhalika na sasa inatumika  kuipamba Sikukuu hii ya Kanisa Ulimwenguni.


 

Mwanakwetu alibaini kuwa ndiyo maana jamaa hawa vijana hapa Mkoani Mara walikuwa wakikata matawi ya mti ule na hapo hapo na yeye Mwanakwetu akanyakua tawi moja kutoka nyumba hii jirani ili kesho yake akalitumie kama tawi lake kuipamba Sikukuu hii ya Jumapili ya Matawi na sasa tawi hili limebarikiwa na lipo sebuleni kwa Mwanakwetu likingoja jumatano ya majivu ijayo.

Historia ya Kanisa Ulimwenguni kwa madhehebu mengi ya  Kikristo, yakiwemo ya Kiorthodoksi, Kikatoliki, Kilutheri, Methodisti, Anglikana, Moravian inadokeza kuwa wakristo husambaza matawi ya miti hii kwa waamini wao Kanisani wakati wa liturujia za Jumapili ya Matawi,. Wakristo huchukua mitende hii, ambayo mara nyingi hubarikiwa na makasisi, hadi kwenye nyumba zao, ambako huyatundika pamoja na picha zingine za Kikristo majumbani kwao.

Kanisa katoliki ulimwenguni kuipamba sikukuu hii limepuliza mbiu ya mgambo yake kwa kusema haya,

 

“Tumtazame Yesu, neno aliyefanyika mwili, akijifunua kwetu katika masomo ya Jumapili hii, tunalianza Juma Takatifu kilele cha safari yetu ya Kwaresima, huu ni ukumbusho wa mateso yake, kifo chake na ufufuko wake wa Bwana wetu Yesu Kristo, wiki yetu inaanza kwa baraka za mitende inayokumbusha kuingia kwa ushindi kwa mfalme wetu Yerusalemu, tunamwimbia hosana, ambaye anakuja kwa jina la Mungu, siku hii pia tunatangaza shauku ya Bwana.

 

Mtakatifu Luka katika injili yake anatuambia kwamba wazee walimpeleka Yesu kwa Pilato kwa mashtaka ya uwongo ambayo watu waliomba asulubiwa, ingawa Pilato hakumwona Yesu na hatia ya mashtaka hayo, Bwana Mkubwa Pilato aliinama mbele ya umati na kusema bayana Bwana Yesu hana hatia lakini umati ulijawa na vituko, vituko hivyo vinapoteza matumaini kwa wanadamu wenzetu na kukatishwa tamaa kabisa.

 

Lakini kwake Kristo Yesu na baadhi ya watu waliokutana nao pale Kalvari kuna matumaini , huku binti za Yerusalemu waliokaa karibu naye. Hapa tumkumbuke yule mwizi aliyesulubiwa na Yesu ambaye alimtambua kuwa ni mfalme, tunakumbuka jinsi Yesu alivyomwomba Baba awasamehe wale waliomtesa kwani hawakujua walichokuwa wakifanya , ndugu zangu katika nyakati za ubinafsi na umimi, giza la jamii likitanda tutafute dalili za matumaini ambazo Yesu anatutuma, yeye anayeteseka na yeye ni uso wa matumaini.”

 

Haya ni maelezo ya Kadinali Luiz Antonie  Tagle Mkuu wa Propanganda Fide ya Kanisa Katoliki Ulimwenguni inayojihusisha na Uinjilishaji wa watu akieleza kwa kina juu ya sikukuu ya matawi japokuwa inajawa na shangwe lakini ndani inajengwa  dhana huzuni ilijawa na usaliti na kukatishwa tamaa.

Kanisa Katoliki katika kuipamba zaidi siku hii pia linaongeza zaidi sauti  ya mbiu yake kwa kusema haya kwa kila Mkristo;

 




Tumefikia awamu ya mwisho ya tafakari yetu juu ya mtu anapokuwa katika hali ya hatari , huwa anachanganyikiwa, kama ungeweza kukumbuka nyakati ulizopitia wewe binafsi utabaini hili, ukiwa umechanganyikiwa uliwajibuje walio kando yako? 

Kuchanganyikiwa kulimsukuma Musa kutomtii Mungu, kwa hiyo kwa mtu yoyote hali hii inapotuvuruga inapendekeza kuomba na kusali sana ili tupate kiasi, ili tuweze kujibu kwa umakini kwa wale walio jirani  nasi na kwa kujizuia, kuchanganyikiwa zaidi  katika hali kama hii mtu anaweza pia kusababisha watu kununa kama tulivyoona katika jibu la Mariamu wa Bethania kwa kuchelewa kwa msaada wa Yesu, uzoefu tuliojifunza kwamba kuwa tunapochanganyikwa pia kunaweza kuwa ni hatua ya kuelekea kuwa na ujuzi wa kina wa juu zaidi juu ya Yesu na yeye ni nani leo hii kwetu sisi. 

Tukumbuke baadhi ya nyakati za kukatisha tamaa ambazo Yesu mwenyewe alikutana nazo, ikiwa tutazingatia kwa makini simulizi za injili tunaweza kuhitimisha kwamba wanafunzi wa Yesu hawakuwa wanafunzi bora kabisa ambao mara nyingi walisahau mafundisho ya Yesu, pia walishindwa kuelewa maneno na matendo yake baada ya hata ya kulisha watu 4000. kwa ajili ya safari yao na hata Yesu mwenyewe alishangazwa.”

Kanisa Katoliki ulimwenguni pia linaongeza kuwa; Lazima hali hii ilikuwa inamkatisha tamaa Yesu, kwani kusikia kwa wanafunzi wake wakijadiliana kuhusu kuwa na mkate mmoja tu, wakati walikuwa wamewalisha watu wapatao 4,000 kimiujiza awali, hivyo swali lake hawakuona kwamba walilisha maelfu kwa mikate michache waliyokuwa nayo? 

Hawaelewi kwa nini walikuwa na vikapu saba vya mikate vilivyobaki? Kikubwa nyakati kama hizo zinatokea lakini Yesu akiendelea kuwafundisha na kuwafundisha wanafunzi wake bila ya kuchoka bila ya kukatishwa tamaa na hata wakati wa mateso yake bustanini hili linaonekana, kwa mfano wanafunzi wake hawakuweza kukesha naye, Yesu aliwauliza mara tatu Je, hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?

 Hapa alistaabishwa , huku hatari iliyokuwa ikija kwa maisha yake, ndugu zangu, Yesu aliwaomba tu wawe pamoja naye lakini walilala, katika nyakati hizo zote za kukatisha tamaa majibu ya Yesu kwa wanafunzi wake siku zote alikuwa na subira, angalia jinsi alivyowafundisha tena na tena baada ya kufufuka, baada ya kifo chake na kaburi lake kuonekana tupu, wanafunzi wake waliogopa na kukatisha tamaa na baadhi yao waliamua kurudi katika maisha yao ya zamani, wengine waliondoka kabisa Yerusalemu, Bwana Yesu mfufuka zaidi ya yote alitumia siku 40 kabla ya kupaa kwake kuwakusanya na kuwafundisha tena na tena, Yesu aliwafinyanga vizuri wanafunzi wake bila ya kuchoka, kwa hakika labda moja ya somo hapa kwetu sisi ni kuanza kutazama nyakati za kukatisha tamaa tunakuwaje, kama mwaliko wa kuwa wavumilivu na kuombea subira ambayo ni zawadi ya Roho Mtakatifu na jinsi gani tunaweza kuwa wavumilivu, huu ni ushauri wa Baba Mtakatifu Francisko kwetu. 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika Sikukuu ya matawi kwa nje inaonekana ni siku ya furaha kubwa, ya  shangwe, vifijo na ndelemo lakini mbele ya safari wanaoshangilia wanageuka kuwa wasaliti wa Bwana Yesu na haya ndiyo maisha mwanadamu yalivyo wanaokushangilia ndiyo wasaliti na ndiyo maana Mkuu wa Propaganda ya Kanisa Katoliki ametilia mkazo wa juu na maanani kubwa juu ya kuwa wastahamilivu katika hali ya mashaka.

Mwanakwetu upo?
Kumbuka 
“Mwaliko wa Kuwa Wastahamilivu.”
 
Nakutakia siku Njema
makwadeladius @gmail.com
0717649257


 





 
 

 

0/Post a Comment/Comments