HAMISI ABDALLAH ALI MTAJI WA CCM MAJUKWAANI UCHAGUZI MKUU WA 2025

Adeladius Makwega-Butiama MARA

Ni majira ya asubuhi ya Aprili 24, 2025, safari ya wanahabari wa mkoani Mara, kutoka hapa Musoma kuelekea Wilayani Butiama, eneo alipozaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, shabaha ni kuripoti ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi. Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Wanahabari hao walikuwa wa kwanza kufika Butiama katika viunga vya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Kilimo na Tekinolojia kampasi ya Oswald Nang’ombe Marwa.

Kwa kuwa ilikuwa mapema sana wanahabari hao walimuomba Mkuu wa Msafara wanywe chai na kweli waliruhusiwa kupata hicho kifungua kinywa cha mkono mmoja.

“Wengi wao walikunywa chai na chapati isipokuwa Mwanakwetu na mwanahabari mmoja akiwa na Nembo ya ITV, walikunywa chai na vipande vya mihogo.”

Wakiwa hapa mkahawani mwanahabari wa Channel 10 alimtania Mwanakwetu kuwa wewe wa Mbagala kula tu mihogo. Huku mwanahabari wa ITV akisema hii mihogo mnayoidharau leo hii ukiwa Dar es Salaam inakulea vizuri sana.


 

Mara baada ya kifungua kinywa hicho wanahabari hao walingia ndani ya Kampasi ya Oswald Nang’ombe Marwa ili kumsubiria Bwana Mkubwa Katibu Mkuu CCM Taifa Dkt Nchumbi na viongozi wengine ili waripoti tukio hilo.

Mwanakwetu alikaribishwa na mandhari moja nzuri, majengo imara, huku wanachuo wakisoma na wafanyakazi wakitekeleza majukumu yao.

Mwanakwetu akiwa anashangaangaa alipita binti mmoja aliyevalia hijabu maridadi na gauni lake. Muungwana Mwanakwetu akampiga dada huyu na Asaalaam aleiukuum, binti huyu alijibu Aleukuum Salaam. 

Mwanakwetu akampiga maswali kadhaa na kisha kupewa majibu haya;

“Ninaitwa Swaumu Hashimu Idd, mimi ni Afisa Tawala wa chuo hiki, ninasimamia utawala mzima wa chuo hiki na kazi nimeanza mwaka jana wa 2024, kazi yoyote ina changamoto.

Binafsi sijaolewa bado, kwa mazingira haya siyo tofauti sana na kwetu Same-Kilimanjaro lakini nimeshayazoea, ninawaomba watoto na vijana wa Kitanzania mje kusoma Kilimo hapa chuoni petu maana mtaweza kujiajili wenyewe baada ya kuhitimu mafunzo yenu.”

Mwanakwetu alipokelewa vizuri na Swaumu Hashimu Binti Idd na kumuelekeza mazingira ya chuo hiki na kumkutanisha na watu kadhaa.


 

Kumbuka tu msomaji wangu Swaumu Hashimu Binti Idd hajaolewa na yupo hapa Chuo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Kilimo na Tekinolojia Kampasi ya Oswald Nang’ombe Marwa kama Afisa Tawala.

Mwanakwetu alikutana na wanafunzi darasani wakisoma na kiongozi wa darasa hili alikuwa huyu Martha Masome.

“Tunasoma masomo kadhaa ya Kilimo na tekinolojia, tunasoma ili kuweza kujiajili na kuwajili wengine. Kwa hakika nikimaliza hapa nitaweza kujiajli katika viwanda vidogovidogo, huku mtaji nitapata kupitia taasisi za kifedha kama vile benki kwa kukopa.”

Mwanakwetu anachanja mbuga za viunga vya Oswald Nang’ombe Marwa na kisha akakutanishwa na Siwema Rashid Binti Rajabu yeye ni Fundi Sanifu yaani mhudumu wa maabara ya taasisi hii.

“Nipo hapa tangu mwaka 2017 shughuli zangu ni kuandaa vifaa na sampuli  kwa ajili ya wanafunzi na wanapokuja kufundishwa na waadhiri. Mimi ninatayarisha vifaa vyote kabla ya majaribio kutoka vyanzo mbalimbali.

Mimi ni Mzaliwa wa Kibaha Mkoa wa Pwani.

Binafsi ninawaomba Vijana wa Kitanzania waje kusoma, wengi wanaosoma hapa kwa sasa ni wavulana waje na wasichana wenzetu, labda niseme ukweli watu wa Mara ni wazuri, mimi nimekaa hapa vizuri na tangu nije ni miaka saba, sijawahi kuguswa wala hata kupigwa na hawa jamaa tunakaa nao vizuri kabisa.”

Msomaji waagu kumbuka mtu anayeishi  mbuga yoyote akikupa simulizi ya uzoefu wake mbugani msikilize hapo amekwisha itembelea kwa hiyo watu ni Mara ni wema sana.


 

Msomaji wangu kumbuka tu Mwanakwetu yupo katika taasisi ambayo inatembelewa na Katibu Mkuu wa CCM Taifa katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Mwanakwetu hapa alikutana na Waziri wa Elimu wa Serikali ya Wanachuo Jesta Philbert nayeye kuyasema haya,

“Nategemea baada ya kuhitimu nijiajili mwenyewe, japokuwa hili ni jambo gumu lakini nitapambana kufa na kupona katika  na nitafanikisha tu.”

Kweli baada ya dakika 15, Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi alifika kampasi hii huku akipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Tekinolojia Profesa Carolyne Nombo na hapa hapa Kampasi hii kukaguliwa majengo yake mapya kadhaa kisha Katibu Mkuu CCM Taifa kuingia garini kuelekea Makao Makuu ya chuo hiki hapa hapa Butiama ambapo ujenzi mkubwa unafanyika.

 Walipofika hapa ugeni huu ulipokelewa na Injinia Sylivesta Francis nayeye kuelezea kwa kifupi kazi zinavyofanyika katika ujenzi mkubwa wa taasisi hii ya umma ambapo Mkuu wa Chuo hiki ni mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mtoto wa Mkulima) ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne.


 

Kwa hakika Mkuu wa Mkoa wa Mara alitoa nafasi wa Mbunge wa Butiama mh Jumanne Sagini na yeye kuyasema haya,

“Chuo Kikuu hiki kilikuwa kinapiganiwa na viongozi wezangu wengi walionitangulia mathalani mzee Nimrodi Mkono kwa sasa naishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha nyingi na sasa kazi inakwenda kwa kasi.”

Mkuu wa Mkoa wa Mara alitoa nafasi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa Nombo nayeye kukishukuru CCM kwa Chuo kutembelewa na mradi yao kukaguliwa na Katibu Mkuu wa CCM Taifa huku akisema bayana kuwa mradi huu utaendelea kusimamiwa kwa nguvu zote hadi utakapokamilika.


 

Baadaye Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi alisema kuwa uwekezaji wa serikali katika mradi huo ni mkubwa sana na una faida nyingi za uwepo wa mradi huu kwa sasa unazidi kufungua milango kwa kuwa kutakuwa kampasi ingine ya Chuo Kishiriki cha tiba wakishirikiana na Hospitali ya Mkoa wa Mara.

Baadaye Mkuu wa Mkoa Mara Kanali Mtambi alimualika Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi.Dkt. Emmanuel Nchimbi kuzungumza na wananchi wa Butiama, huku akisisitiza mshikamano na kutoa pongezi kwa viongozi wa Mkoa wa Mara na Wizara ya Elimu kwa kuusimamia mradi huo vizuri..


 

Kwa hakika katika ziara hii hapa Butiama ilikuwa nzuri, furaha tele ndelemo, nyimbo za  CCM zikisikika , kikubwa zaidi shughuli hii  ilipambwa na kwa mvuto wa Mzee Hamisi Abadallah Ali ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Songea Mjini kwa namna alivyokuwa akilimiki jukwaa na uteuzi wake wa maneno kwa hadhira yake.

Uwepo wa Mzee Ali kwa hakika ni mtaji mkubwa wa CCM katika katika majukwaa ya kisiasa kwa uchaguzi wa mwaka wa 2025 na Mwanakwetu anamlinganisha Hamisi Abdallah Ali na magwiji wa siasa za Tanzania wakati wa uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 kama vile Ustadh Mtopea na Shekh Ali Idd wa NCCR MAGEUZI na ndani ya CCM ni Ndugu Tambalizeni.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka,

“Hamisi Abdallah Ali Mtaji wa CCM 2025.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 




 


 














































 





0/Post a Comment/Comments