Adeladius Makwega-Musoma MARA.
Februari 25, 2025 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ilipokea ugeni wa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara mhe. Exaud Kigahe(mb) ambapo awali kiongozi huyu alifanya mazungumzo kadhaa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi yakiwa mazungumzo ya faragha yakilenga sekta za Biashara na Viwanda shabaha ikiwa namna ya kuzistawisha sekta hizo katika mkoa huu alipozaliwa na kuzikwa Mwalimu Julius Nyerere.
Shughuli hii katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ilihudhuliwa na viongozi kadhaa akiwano Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ndugu Geofrey Kusaya.
Baada ya mazungumzo haya Naibu Waziri Kigahe alizunguka katika wilaya kadhaa za mkoa wa Mara, akijikita katika kukagua miradi iliyo yote bila kubagua hai na hata ile iliyodhohufu ya Viwanda na Biashara.
Mwanakwetu anashiriki ziara hii tangu mapema Februari 25, 2025 hadi jua linazama na akiwa katika ziara hii alikuwa anatafakari mengi na mojawpao ni hili;
Je ziara hii ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, wizara inayoongozwa Waziri makini Mh Dkt .Seleiman Jafo, je ziara hii ina maana gani kwa watu wa mkoa wa Mara?
“Katika kulitazama hli alikubaliana kuwa katika Mikoa inayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ipo mikoa ya aina mbili, ile shughuli zake za uchumi za misimu msimu na ile shughuli zake zimechangamka mwaka mzima.
Mwanakwetu anatambua hata kama shughuli za uchumi katika mikoa fulani mwaka mzima zinachangamka lakini zipo sekta ambazo zinadolola kipindi fulani lakini nafuu inatokana na baadhi ya sekta kuziba pengo la sekta fulani bini fulani, kwa hiyo unapotazama takwimu hasa za nakisi katika mapato kutoka mwezi mmoja kwenda mwingine haipo NAKISI, huku ile mikoa ya akina yakhe mdololo unapoibuka hakuna sekta inayoweza kuziba pengo la sekta nyingine.”
Mwanakwetu anatambua mikoa yenye sekta hizi mbili yaani Viwanda na Biashara inafanya vizuri, kwa kina ndiyo inayofanya biashara kama kutunza fedha zako kubaki katika mzunguko na kuwa mikoa yenye uchumi uliyochangamka mwaka mzima.
Mwanakwetu angeweza kuitaja mikoa hiyo lakini hapana kikubwa,
“Kama kuna shabaha ya kulenga kwa mkoa wowote ilikufikia uchumi uliyochangamka lazima, lazima ,lazima hawa ndugu wawili Viwanda (Jafo) na Biashara (Kigahe) wawe sehemu ya maisha ya wananchi wa mkoa huo , hilo ndilo jukumu alilokabidhiwa Dkt.Seleiman Jafo na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Katika hili la kukuza uchumi kwa mkoa wa Mara, ndugu yetu Kanali Evans Alfred Mtambi alizungumza katika wino uliyokoza ofisini kwake mbele ya Waziri Mdogo Kigahe.
“Tuna fursa nyingi zikiwamo Ziwa Victoria na madini yamelala katika ardhi yetu, mifugo bora ipo katika ardhi yetu, yapo mambo tunayoyafanya ikiwamo hata kubadilisha fikra kwa wanaopata utajiri kutokana na madini, ziwa, utaliii na mifugo, sasa kuanza kuwekeza mkoani Mara.
Wapo ndugu zetu wengi wanapata utajiri hapa wanawekeza mikoa mingine ya Tanzania, hilo siyo tatizo, hii yote ni Tanzania lakini ni vizuri kuwekeza pia pahala ulipopata ngekewa ya utajiri wako.”
Msomaji wangu hayo ni ya Mkoa wa Mara huku yapo ambayo lazima Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya kufanya kwa ngazi ta taifa.
Mwanakwetu amebaini kuwa ziara hii ni ya kwanza ya kiongozi wajuu kutoka wizara yenye sekta za Viwanda na Biashara kutembelea mkoa wa Mara tangu mara mwisho mkoa huu ulipotembelewa na mh Waziri Charles Mwijage miaka mitano nyuma. Kumbukumbu zinautendea haki mkoa wa Mara kwa kudokeza kuwa miaka mitatu nyuma waziri kutoka sekta hizo mbili wakati huo Dkt. Ashatu Kijaji alifika mkoani Mara ikiwa ni shughuli za chama na kisha kuondoka, huku bila kutafuna ziara ya Mhe Charles Mwijage ikibaki katika rekodi ya juu ya mkoa huu.
Hizo msomaji wangu ni rekodi mbazo ni vigumu kupingana nazo, ndiyo kusema uwepo wa Waziri wa Viwanda na Biashara mkoani Mara unaweza kusaidia mengi;
“Serikali huwa inapata taarifa ya hali zote na sekta kila siku lakini Waziri akiwepo anapata picha ya hali ya mkoa kwa macho yake na yeye kuwa na taswira halisi inayoweza kumuongoza kuelekea kumshauri rais na Baraza la Mawaziri vizuri.”
Naibu Waziri Kigahe alifanya mazungumzo na wafanyakazi wa Forodhani pale Sirari, ambacho kilikuwa kikao kilichokusanya wataalamu wengi kwa siku ya Februari 25, 2025 kutoka kada mbalimbali, ambapo Mwanakwetu aliingia katika kikoa hicho akiwa na matumaini makubwa watumishi hawa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wangefunguka mbele ya Waziri wetu mdogo mh Audax Kigahe.
Wafanyakazi hao kwa hakika wanafahamu vizuri juu changamoto za kibiashara katika mpaka huu Tanzania na Kenya na wanafahamu nini kifanyike lakini naona kwa bahati mbaya Mwanakwetu kwa macho na masikio yake baada ya Katibu Tawala wa Wilaya hii kuongea wafanyakazi hawakuweza kufunguka kwa Naibu Waziri Kigahe, hii ni tathmini ya Mwanakwetu.
“Kwa hakika wafanyakazi wale wanafahamu changamoto ni zipi, kipi kifanyike na kifanyike kwa namna gani ili kufikia malengo ya serikali kibiashara hapo mpakani.”
Mwanakwetu anatambua Wizara ya Viwanda na Biashara inazo taarifa na inao uwezo wa kupata taarifa na kuishauri serikali ili mkoa wa Mara uzidi kufunguka zaidi kibiashara na milango ya kibiashara ikifunguka na haya maisha ya biashara za msimu yataondoka.
Jambo hili liligusa mno tafakari ya Mwanakwetu na wakati Mwanakwetu anatayarisha makala haya ya uchambuzi ya Viwanda na Biashara alikumbuka mwaka 1993 mhe Charles Mwijage akiwa kijana sana jijini Dar es Salaam alikuwa mwenyekiti wa kamati ya Harusi Moja ambayo Mwanakwetu alishiriki.
“Siku hiyo harusi ilifungwa Temeke Bomani, kando ya Uwanja wa Taifa (sasa Benjamin Wiliiam Mkapa) Mwanakwetu kijana akishiriki kwa karibu maana Binti Makwega(Demetria (Ayub) Makwega)-Mpogolo wa Mbagala alikuwa anaolewa na Hamduni Millanga Mhaya kutoka Muleba. Mandhari Kando na Ofisi ya Mkuu Wa Wilaya ya Temeke zilisikika nyimbo za Pepe Kalle na Papi TAX kutoka Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam kulipokuwa na Bonanza fulani ambalo haikumbukwi lilikuwa na jambo gani. Ndoa ya Kiserikali ikafungwa kisha sherehe kufanyika katika ukumbi wa Bandari Tandika.
Wakazi wengi wa Mbagala akiwamo Mwanakwetu na familia nyingi za kijiji hicho cha ujamaa walizoea kufanya sherehe katika viwanja vya wazi, hakuna kadi wala kiingilio, wakaazi wengi walitoka Mbagala hadi Bomani Temeke na wengine kwa mguu hadi Tandika Bandari Club wakijua mambio ni yale yale lakini ukumbini waliruhusiwa watu 50 tu kutoka kikeni waliyopewa kadi na kundi kubwa la watu kutoka Mbagala kubaki nje akiwamo Mwanakwetu.
Jamaa kutoka Mbagala wanahusudu pombe na msosi wa bure harusini wakati Wahaya wamejipanga ni watu 50 tu kutoka kikeni. Watu wa Mbagala wakafanya vurugu mlangoni askari wa bandari wakasema hakuna mtu kuingia ambaye hana kadi na kweli ikawa hivyo.
Watu wa Mbagala wakawa wanasema ,
‘Nyinyi Wahaya washenzi(ashakumu si matusi kabisa, acheni mambo yenu tumewapa binti yetu mzuri na mrembo, kuweni na adabu na nidhamu kwetu, mkiendelea tutavamia ndani tumchukue bibi harusi tuondoke naye na huyu binti ataweza kukaa na kijana wenu.’
Sherehe inaendelea, ikafika kipindi cha upande wa Bibi Harusi kutoa neno, hapo bibi Harusi na nduguze wengi wapo nje na zawadi zao, bibi harusi mchozi unamtoka nduguze hawaoni maana harusi ya watu 500 watu 50 wachache mno hawaonekani.
Hapo hapo Mwalimu Francis Makwega mwakilishi wa familia ya bibi harusi akasema maneno haya,
‘Jamani Wahaya eeeh , bibi harusi analia harusini kwenu huu ni uchuro ,kisa nduguze wapo nje. Kwetu Mbagala haya mambo ya kadi hayapo, sherehe tunafanya wazi uwanjani na kila mmoja anakuja, kabla sijasema neno la familia waruhusuni walio nje waingie, Kinyume chake mimi na tulio ndani tunatoka ili turudi nje tuungane na walio nje turudi nyumbani kwetu na nyie muendelee na harusi yenu.’
Hapo ndipo Wahaya walilainishwa na Wapogolo akina Mwanakwetu na jamaa kadhaa wa Mbagala wakaingia fungulia mbwa na nyimbo Sanguru ikichezwa.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika Mwanakwetu anaamini ujio huo Waziri Mdogo hapa Mkoani Mara una tija na unaweza kuongeza fursa zaidi kwa sekta hizi mbili za wizara hii. Mwanakwetu amekumbusha ujio wa mhe Dkt. Ashatu Kijaji miaka mitatu nyuma hapa mkoani Mara, pia anakumbusha ujio wa mhe Charles Mwijage miaka mitano nyuma na Mwanakwetu kwenda mbali zaidi kwa kumtazama mh Charles Mwijage wa mwaka 1993 pale Dar es Salaam kama mwenyekiti wa kamati ya harusi.
Kikubwa ziara hii ya Waziri Mdogo wa Viwanda na Biashara inatarajiwa kuwa na matunda zaidi kama ile ya Charles Mwijange ya miaka mitano iliyopita na itazama matunda mema kama ile ndoa ya ndugu Hamduni Milanga na Demetria (Ayub) Makwega mwaka 1993 amnapo sasa wanajukuu.
“Kikubwa kama ilivyokuwa harusi ile ya mwaka 1993 kila upande utoe nafasi kwa upande mwingine na kusikilizana , mtu akikaa kimya hatuwezi kufika mawazo yatolewe na yafanyiwe kazi kama hiki kisa cha Wahaya(Biashara) Waliolanishwa na Wapogolo(Wapogolo) lakini pia Wahaya wanaweza kuwa Viongozi huki Wapogolo kuwa Wafanyakazi wa forodha pale Sirari, pia Wahaya wanaweza kuwa viongozi wa Mkoa wa Mara na Wapogolo kuwa wananchi wa mkoa wa Mara.”
Wanaotekeleza majukumu ya sekta ya Biashara na Viwanda wasikilizwe mno maana bibi harusi wetu ni yale mafanikio ya sekta ya Biashara na Viwanda .
Mwanakwetu upo?
Je makala haya yaitwaje? Audax Kigahe Kama Charles Mwijage? Au Wahaya Waliolainishwa na Wapogolo? Mwanakwetu anachagua Wahaya waliolainishwa na Wapogolo.
Nakutakia siku Njema.
0717649257.
Huyu mama juu ndiye Demetria Ayoub Makwega.
Hamduni Millanga, kijana wao kati na Demetria Ayoub
Post a Comment