Adeladius Makwega-Musoma MARA
“Mamaaa… mamaaa …mamaaa…namtaka mama, namtaka maama, namtaka mama, namtaka mama. Wewe nenda atazoea tu ndivyo walivyo, wenzake wote siku hizi za mwanzoni wote walisumbua.”
Hilo lilikuwa tukio lililotokea mbele ya geti la shule ya moja Kimataifa jijini Dar es Salaam mwaka 2004, Mwanakwetu akiingia kazini zikiwa siku za mwanzo mwanzo Mwanakwetu akiwa mwalimu shuleni hapo.
Jambo hilo lilikuwa geni mno kwa Mwanakwetu, japokuwa alikuwa mwalimu aliyehitimu na kufuzu mafunzo ya ualimu kwa ngazi ya Stashahada mwaka 2003 pale Chuo cha Ualimu Kasulu, lakini yeye alibobea kusomesha wanafunzi wa sekondari tu huku akifanya mazoezi ya ualimu kwa vitendo hapo Mwandiga na Bogwe Sekondari zote za mkoani Kigoma.
Mwanakwetu akiwa shuleni hapo alibaini kuwa baadhi ya mambo anaweza kujifunza kazini kama hilo la watoto wa chekechea, japokuwa yeye alikuwa hafundishi madarasa hayo.
“Wazazi waliweza kufika shuleni hapo na kuwasajili watoto wao kwa masomo ya chekechea, shule ya msingi na hata sekondari. Wanafunzi wageni wa madarasani ya juu walitambuliwa kwa sare zao kuwa mpya tu lakini wale wa chekechea utambulisho uliendelea kuwa vilio tu kwa mwezi mzima.”
Baada ya mwezi kuisha vilio vyao vilipotea kabisa huku walimu wa chekechea wakiwashika mikono wanafunzi hao na wakiingia getini na hata wakati wakirudi nyumbani wakiwapungia walimu wao.
“Bye teacher Rehema, Bye teacher Lina, Bye teacher Neema and Bye bye teacher Penina-Kwa heri mwalimu Rehema, Kwa heri mwalimu Lina, Kwa heri mwalimu Neema na kwa heri mwalimu Penina.”
Mwalimu Penina, Mwalimu Lina na Mwalimu Rehema wakisomesha chekechea wakati huo.Mwanakwetu ndani ya mwezi mmoja tu mtoto aliweza kubadilishwa tabia na kuipenda shule na mazingira yake, hilo likiwezekana kutokana na mbinu mbalimbali za kufundisha watoto. Mwanakwetu aliweza kubaini uwezo mkubwa wa walimu wa madarasa ya awali ushawishi mkubwa wa kuweza kuwafundisha watoto hawa kutoka kutofahamu hadi kufahamu mambo mbalimbali kwa kutumia michoro, picha, sanamu, nyimbo na pia kutumia mazingira halisi ya jamii.
Walimu hawa wa chekechea walielewana sana na wanafunzi wao na Mwanakwetu alibaini kuwa ujirani huo ulikuwa wa kama mama na mtoto wake, huku watoto hao wakiwasimulia walimu wao mambo yote yanayotendeka majumbani mwao.
“Baba na mama jana walipigana, mama hadi kaumizwa na leo mama hajaenda kazini, amevimba jicho jicho.”
Mwalimu alimuuliza mtoto huyu kuwa nani aliyemchokoza mwezake? Mtoto huyu wa kike alimueleza mwalimu wake kuwa mama yake ndiyo aliyemchokoza baba yake. Mwalimu alimuuliza je mama kupigwa na baba ilikuwa sahihi? Mtoto huyu alijibu kuwa jambo hilo lilikuwa sahihi lakini kosa la baba yake kumuumiza jicho mama yake tu. Mwalimu alimueleza mtoto huyu kuwa akienda nyumbani akampe pole mama yake na akamwambie baba yake asiwe anampiga mama yake. Mtoto alifika nyumbani na kumpa pole mama yake kwa kipigo hicho na kumueleza pia baba yake kuwa akimpiga mama yake asimuumize, ampige kidogo kidogo.
“Wazazi walitambua fika kuwa yale yanayofanyika majumbani yanafika shuleni kama yalivyo, japokuwa kuna wakati baadhi ya wazazi walikuwa wakigombana na walimu wakisema haya mambo ya nyumbani kwetu hayamuhusu kabisa mwalimu.Walimu waache umbea, wakati mwingine baadhi ya walimu wa kike wakiambiwa waache kuwasiliana na waume za watu, mambo ya familia zao na hata watoto wao wasiulizwe chochote.”
Tukio kubwa linalokumbukwa na Mwanakwetu kwa mwaka huo ambalo kwa hakika linaonesha nguvu ya mwalimu ni hili,
“Siku moja mama mmoja, binti yake aliporudi shuleni alipokuwa anamuogesha alibaini kuwa mtoto wake alikuwa na maumivu chini ya kitovu, mama huyu alimchunguza mtoto wake na kila alipojaribu kumuuliza mtoto kilichotokea hakupata majibu. Mama huyu siku iliyofuata aliamua kufunga safari hadi shuleni kuhoji kulikoni?
Alipofika shuleni alikutana na mkuu wa shule na yeye kumsimulia kilichotokea, baada ya maelezo ya mzazi kwa mkuu wa shule wakaitwa mwalimu kadhaa wa darasa akiwamo Mwanakwetu na mwalimu wa darasa la chekechea kusadia kuitatua kesi na kukaa na binti mdogo kuzungumza naye.
Mbele ya kikosi cha walimu wa madarasa mwanafunzi wa chekechea hakusema kilichotokea. Mwalimu wa Chekechea aliyefahamika kama madam Lina akasema maneno haya, ‘Jamani naombeni mniruhusu nikazungumze naye darasani tukiwa wawili.’ Mwalimu wa chekechea alimuomba mkuu wa shule. Mwalimu huyu alitoka na kwenda huko alizungumza na mtoto kwa kina .”
Baada ya dakika 45 alirudi ofisini kwa mkuu wa shule ili kumueleza kipi kilitokea? Hapo hapo Mkuu wa Shule akatuita walimu wote wa darasa ofisini kwake naye Madaam Lina akashika usukani akaanza kusimulia kilichotokea,
“Wakati wa mapumziko siku iliyotangulia wanafunzi wa chekechea walikuwa wanacheza na huku wakiomba ruhusa ya kwenda chooni kwa zamu, watoto wa kike kwa wakiume kila mmoja chooni kwake. Wakati harakati hizo zinafanyika binti mmoja alipokuwa chooni mtoto wa kiume aliingia choo cha kike na kufanya kitendo kisicho cha kiungwana na kinyume na maadili cha kuingiza kidole chake katika sehemu ya siri za binti huyu mdogo na kumsababishia maumivu.”
Mwalimu huyu wa chekechea aliamuita mtoto huyo wa kiume na kweli alipoulizwa alikiri kufanya hilo tukio huku huko darasani mbele ya binti huyu wote wakisoma chekechea.
Mkuu wa shule aliamua kuwa wazazi wa mtoto wa kiume aliyetuhumiwa kuitwa pia shuleni hapo na kuelezwa kilichotokea. Siku iliyofuata walifika na kuelezwa namna wazazi wanavyopaswa kuwa makini katika malezi ya mtoto wao.Shida ilibainika kuwa wazazi wa mtoto wakiume walikuwa wanalala naye chumba kimoja na hilo ndilo lililosababisha hata mtoto huyu wa kiume kufanya kitendo hicho, wazazi wa mtoto huyu walikuwa wamepanga chumba kimoja hapo Sinza Kumekucha. Mkuu wa shule aliwaeleza walimu wake kuwa makini pia na kuwafuatilia watoto wakiwapo shuleni na hata maisha yao ya nyumbani.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Tukio hilo sasa linakaribia miaka 20 na Mwanakwetu anasemea hata wanafunzi hao walishiriki tukio hilo sasa ni watu wazima na pengine tukio hilo liliwafanya kuwa watu wema sana duniani.
Mwanakwetu hiyo ni nguvu kubwa aliyonayo mwalimu. Ifahamike wazi kuwa malezi ya watoto yanahitaji mno ushirikiano baina ya wazazi/ walezi, walimu na jamii nzima ili kuwa na raia wema huku serikali na waajiri wengine mkumbuke kuboresha mazingira ya walimu wetu. Mwalimu anao uwezo wa kumtengeneza Mwanafunzi wake baada ya 20 aweje na hata awe na mtazamo gani, kwa hiyo unaposikia mwalimu tulia maanani sana vinginevyo baada ya miaka 20 hao wanafunzi wa mwalimu huyu watakuwa katika namna ambayo mwalimu anataka pata picha kwa mwalimu anayelalamika unadhani upo usalama? Usalama haupo.
Mwanakwetu upo?
Mwanakwetu nakwambia popote pale ulipo, iwe juu au chini kumbuka, kumbuka sana sana kumpa heshima yake mwalimu wako.
Kumbuka ,
“Itambue na Kuiheshimu Nguvu ya Mwalimu.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment