WAKRISTO MAHUJAJI WA MATUMAINI

 


Adeladius Makwega -Musoma MARA.

Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki Ulimweguni anayejihusisha na Uinjilishaji wa Watu, Kadinali Luiz Antonie Tagle amesema kuwa wakristo wanaposafiri katika wakati wa mwaka wa liturujia wanapaswa kutambua tena jinsi wokovu wa Mungu unavyodhihirishwa kupitia matendo ya marafiki wa Yesu, maana wao ni mahujaji wa matumaini, wapate tumaini kwa Yesu na neno lake wawapelekee wengine ili sote tusafiri katika tumaini la pamoja.

Haya yamehubiriwa na Kadinali Tagle kupitia Word Expose Januari 26, 2025 ikiwa ni Jumapili ya Tatu ya Mwaka C wa Liturujia ya Kanisa.

“Ebu Tumtazame Yesu neno aliyefanyika mwili, akijifunua kwetu katika masomo ya jumapili ya tatu mwaka C wa Kanisa, injili ya leo inasimulia Yesu akiwa amesimama katika sinagogi na akisoma katika kitabu cha Nabii Isaya,

 

‘Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta, kuwahubiri maskini habari njema, amenituma kuwatangazia wafungwa uhuru wao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru walioonewa, kuwatangazia mwaka wa Bwana uliokubalika.’

 

Bwana Yesu asema haya yanatimia katika kusikia kwao jubilii iliyotabiriwa na Isaya, hatimaye umefika wokovu wa Mungu na ufalme wake umekaribia, tunaposafiri katika wakati wa majira ya mwaka wa Kanisa tutagundua tena jinsi wokovu wa Mungu unavyodhihirishwa kupitia matendo ya marafiki wa Yesu. Sisi ni mahujaji wa matumaini, tupate tumaini kwa Yesu, nafsi yake na neno lake tuwapelekee wengine ili sote tusafiri katika tumaini la pamoja.”

 

Wakati Kadinali Tagle akihubiri haya, hapa katika Kanisa la Mtakatifu Augustine Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma nchini Tanzania, Padri Julius Ogolla alilisisitiza,

 

“Jumapili hii tunasikia Ezra anasoma maandiko ya Mungu ambapo Kikanisa ni siku wasomaji wetu wanabarikiwa ili wasomaji wetu wasome vizuri, huku ikisisitizwa pia wajibu wa kulisikiliza neno hili la Mungu.”

 

Akihitimisha mahubiri yake Kadinali Tagle alilipiga chapuo suala la mwaka huu wa 2025 utusaidie kuadhimisha mwaka mtakatifu wa kuponya uhusiano wetu na jumuiya zetu na Mungu, kanisa linatualika kushiriki katika shughuli mbalimbali ambazo zinatuwezesha kuomba na kufanya upya tumaini kwa Mungu na kwa kila mmoja wetu kwa mwingine, sio wakati wa kutembelea vituo vya biashara na anasa watu wale raha hapana badala yake ni wakati wa kupata nafasi kufanya matendo ya ukarimu kwa watu wengine kama Yesu yeye mwenyewe alivyofanya, tujifunze uzoefu na mahujaji wenzetu, sisi kujifunza kuhusu hali nyingine za maisha na mitazamo hata hivyo inatufundisha kitu kuhusu maisha ya imani na kusafiri kiimani maishani, 

 

Kadinali Tagle alikumbusha na hili,“Wakati wa Misa ya mkesha wa Krismasi mwaka wa 2024 Baba Mtakatifu Fransisko alifungua mlango mtakatifu katika Kanisa Kuu la St Peter's Basilica akifungua rasmi mwaka wa Jubilii ya Matumaini ambao unaadhimishwa hadi Jumapili ya Epifania mwaka ujao 2026, maadhimisho ya mwaka wa jubilii hii ina mizizi ya kibiblia. Kwa maana katika kitabu cha Mambo ya Walawi tunasoma kwamba kila baada ya miaka wa 50 Waisraeli walijitahidi kurudisha mahusiano yao pamoja na Mungu kwa mazoezi mbalimbali yalihusisha upatanisho kwa ajili ya dhambi zao, kusamehana madeni na kurudishiana ardhi iliyonyang'anywa.Ukiangalia kipindi hiki kwa sasa utaona hilo katika siku ya leo maana Injili ya Yesu pia inazindua jubilii katika mazingira ya unabii wa Isaya, yeye alitangaza habari njema kwa maskini, uhuru kwa wafungwa na urejesho kwa wagonjwa na uhuru kwa waliodhulumiwa, alitangaza mwaka wa kukubalika na Bwana, katika muktadha wote huu ndugu zangu kiini cha jubilii ya mwaka huu ni uongofu na ukombozi. Baba Mtakatifu Fransisko anaitazama Jubilii ya mwaka wa 2025 kuwa mwaka mtakatifu wenye matumaini, hilo linaleta matumaini mno ambalo ni tumaini letu kwa Mungu.”

 

 

Kwa hakika katika Kanisa la Mtakatifu Augustine, Parokia ya Mwisenge Jimbo Katoliki la Musoma, mara baada ya mahubiri ya Padri Ogolla dazeni mbili ya wasomaji masomo walisomwa majina yao na walisimama jirani na altare na kupata baraka za kusoma masomo katika parokia hii, huku dazani mbili hizo za walei; wanaume, wanawake na vijana wachache walikuwa miongoni mwao.

Misa hii iliambatana na nia na maombi matano, huku ombi la nne la ibada hii ya misa lilikuwa hili,

“Utusaidia kutambua ya kwamba maisha yetu bila wewe huleta hasara lakini maisha na wewe huleta matumaini–Eee Bwana Twakuomba Utusikie.”

Wakati haya yakiwa ndani ya kuta za makanisa jumapili ya Januari 26, 2025 nje ya ibada hii ya dominika hali ya hewa katika Mji wa Musoma mkoani Mara nchini Tanzania kwa siku tano jua lilikuwa linawaka kwa kadili, lakini jumamosi Januari 25 na jumapili Januari 26, 2025 hali ya hewa ikabadili gia angani na kuwa na baridi, wingu angani, ardhi ikiwa kavu huku ikinung’unika bila kutoa machozi, kimyakimya, ikiubeba ububu lakini ikitamani kuloanishwa na mvua kutoka angani, pengine kama ardhi ya Mji wa Musoma ingekuwa na mikono basi ingeweza kufunga safari na kuinyoosha mikono yake na kuiloweka katika maji kutoka Ziwa Victoria jirani na kuimwagilia ili kusaidia mimea iliyopo katika tumbo lake kumea vizuri, cha kusikitisha ardhi ya Mji wa Musoma haijapewa haki hiyo na Mwenyeenzi Mungu.

makwadeladius@gmail.com

0717649257







 

0/Post a Comment/Comments