Adeladius Makwega-Musoma MARA.
Jumuiya ya Waisilamu wa Mkoa wa Mara wakiongozwa na Shekhe wa Mkoa wa huu, Ustadh Kassimu Msabaha, wamesoma dua maalumu la kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa taifa hili, huku dua hili likiwa agizo ya Shekh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakari Bini Zuberi lililotolewa na Baraza la Waisilamu Tanzania (BAKWATA) Januari 27, 2025 kwa Mashekh wote wa Wilaya na Mikoa Tanzania, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi akishuhudia kisomo hicho na dua likisomwa.
Haya yamefanyika Januari 28, 2025 katika Msikiti Mkuu/ Msikiti wa Ijumaa hapa Mjini Musoma ambapo ndipo zilipo Ofisi za BAKWATA mkoa wa Mara, hatua chache na lilipo Ziwa Victoria.
Dua hili lilisomwa kwa dakika 4 na sekunde 50 huku dazeni tatu ya Mashekhe wakubwa wa Mkoa wa Mara wakishiriki. Akizungumza ndani ya Msikiti wa Ijumaa hapa Musoma Mjini, Mkuu wa Mkoa Mara Kanali Mtambi alizungumzia mambo makuu matatu,
“Dini ina umuhimu mkubwa kwani zote zimesisitiza katika matendo mema na upendo, serikali lazima ishirikiane na dini ili serikali yenyewe iwe madhubuti na mwisho naipongeza Jumuiya ya Waislamu Mkoa wa Mara maana mara zote imekuwa karibu nami na Serikali ya mkoa wa Mara kila shughuli tukiwajulisha mnashiriki huku mkiambatana na kutuombea dua.”
Awali kabla ya dua hii kusomwa, Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi alipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti huo mkubwa na wa kisasa na kutoa ahadi ya kuwashika Mkono Waisalamu wa Mkoa huu katika ujenzi huo.Baadaye Mkuu wa Mkoa wa Mara alitembelea Kituo cha Yatima cha Alijaziira ambacho kinalea na kuwapa elimu watoto yatima kadhaa kutoka maeneo ya Mkoa wa Mara na mikoa jirani.
Wakati Mkuu wa Mkoa wa Mara anahitimsha ziara yake hiyo katika Kituo cha Yatima cha Aljaziira, mvua kubwa ilianza kunyesha ambapo mvua hiyo ilinyesha kwa zaidi ya saa moja na dakika 20 katika eneo la katikati la Musoma Mjini na iliweza kumsindikiza Kanali Mtambi kutoka kituo hichi cha yatima hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mara huku ikimpigia salute ya heshima na taadhima.
0717649257
Post a Comment