Adeladius Makwega-Mbagala DAR ES SALAAM
“Kwa mara ya kwanza nilikutana Mohammed Khelefu mwaka 2006 katika Vikao vya Viongozi wa Wanachuo wa Vyuo Vikuu vya Tanzania, NDUGU HUYU akiwa ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanachuo wa Chuo Kikuu Cha Tumaini Dar es Salaam huku Mwanakwetu Akiwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanachuo ya Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa. Mohammed KheLefu alijitambulisha hadharani kuwA yeye ni Mtanzania mwenye asili ya Zanzibar huku MwAnakwetu akinadi kwake kuwa yeye ni Mtanzania Mzaliwa wa Mlali Mpawapwa Dodoma, pia akiwa na asili ya mikoa miwili ya Tanganyika Morogoro (baba) Singida (mama) huku akikulia Mbagala Dar es Salaam.
Baadaye Mwanakwetu hakuweza kuhudhuria vikao hivyo vya Umoja wa Viongozi wa Serikali ya Wanachuo Tanzania kutokana na majukumu mengi huku vikao kadhaa vya mbele kwa mwaka 2006/ 2007 na hata mwanzoni mwa 2008 akishiriki Rais wa Serikali ya wanachuo cha Tumaini Iringa Antipas Zeno Mngungusi (sasa ni Mbunge CCM wa Malinyi Morogoro.)”
Maisha yaliendelea huku tukisoma na kuhitimu elimu hizo kila mmoja na kurejea kazini naye Mohammed Khelefu kupata kazi DW KISWAHILI Bonn Ujerumani.
“Mapema mwaka 2012 Mwanankwetu anaingia chumba cha habari cha DW Kiswahili, anakutana na Mohammed Khelefu akiwa amiongoni mwa wahariri wa chumba hiki cha habari huku akianza kuaminiwa na wakubwa wa taasisi hii akiwamo Bi Andrea Schimdt (Mkuu Wa Idhaa wakati huo)
Nikampa salaam kwema akajibu kwema na kukaa naye vizuri na hata siku anahamia katika nyumba kubwa wakati familia yake inahamia Ujerumani nadhani ikitokea Zanzibar miongoni mwa waliomsadidia muungwana huyu kubeba na kupanga vyombo Mwanakwetu alikuwepo.”
Mwanakwetu ni mwanasiasa na nilikuwa natambua kuwa lazima Mohammed Khelefu atakuwa na mpenzi na siasa za Zanzibar, nikiwa DW KISWAHILI pale Bonn nilipododosa niliambiwa na jamaa zangu kuwa,
“Mohammed Khelefu aliwahi kuwa Blue Guard wa Chama cha Wananchi (CUF) akiwa ni mwanachama wa CUF.”
Hili nakumbuka hata nilipokuwa naongea naye mara kadhaa dhana na Muungano kama koti linalovaliwa nyakati za hata za joto kwa Zanzibar liliibuka,
“Kwa vijana wengi wa Kizanzibari wasio nafasi kwenye CCM na Serikalini wanajitambulisha kama wao ni Wazanzibari kisha ndipo wanakuja na huu Utanzania ambalo hilo halipo kwa vijana wenye asili ya Tanganyika.”
Makwega ebu sikiliza ,
“Hawa jamaa wanaleta stori za Ujerumani Magharibi na Ujerumani Masharikl. Hivi hapa Ujerumani wamekuja na passport ya Zanzibar? Hata kama wameukana uraia wa Tanzania passport iliyowapa Uraia wa Ujerumani ni passport Bibi na Bwana na bendera yake yenye rangi zilizolala mshazali.”
Unaweza kujiuliza msomaji wangu inakuwaje siku ya leo Mwanakwetu anamtaja ndugu yake Mohammed Khelefu mara kadhaa? Muungwana huyu kutoka Zanzibar kafanya nini tena?
Jibu lake ni hili, mapema ya Januari 2025 Erick Kabendera ambaye ni mwanahabari aliyepata changamoto wakati wa Utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano iliyokuwa inaongozwa na Rais John Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan ambaye sasa ni Rais wa Serikali ya Awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ndugu Kabendera alipata misukosuko hadi kufungwa. Mwana habari Kabendera alihojiwa na mwanahabari Mohammed Khelefu katika Gumzo la Ghassani ambao ni mtandao binafsi wa mwanahabari huyu, kwa dakika 79.35. (saa 1.19.35) mwongozo ukiwa kitabu cha Kabendera
“In The Name Of The President.”
Kwa hakika Mwanakwetu anaona mahojiano haya baina ya Mohammed Khelefu na Erick Kabendera yametoa mwangaza wa kilichomo katika kitabu hiki kipya.
Mwanahabari Kabendera ambaye ni mwanahabari mahiri hasa kwa habari za kimombo ambapo kwa Tanzania wasomaji wa habari za kimombo ni wachache sana na hata umaarufu wa Erick Kabendera ni katika hadhira ya wasomi wengi na kimataifa ambapo hili ni jambo zuri sana maana kuiandikia hadhira ya kimataifa inahitaji ujuzi wa mambo mengi ambapo waandishi habari wengi wa Tanzania wanakosa sifa hiyo.Tangu kitabu cha In The Name Of The President na tangu mahojiano hayo baina ya Mohammed Khelefu katika Gumzo na Ghassani yafanyike siku zinasonga huku waliyo wengi wanakimbilia sana kuyasikiliza mahojiani haya ambayo yamekuwa njia mbadala kwa wale wasio fahamu kimombo akiwamo Mwanakwetu kupata mwangaza Erick Kabendera ameeleza nini kitabuni. Mpaka mapema Januari 14, 2025 watu 843 walipenda mahojiano haya huku watu 104,567 wakitazama mahojiano haya yalipachikwa Januari 3, 2025.
“Suala la Ben Saanane linasikitisha sana … ni jambo ambalo limetupa mjadala mkubwa sana kabla ya kulichapisha…Jambo hili nimelifuatilia tangu Ben Saanane akiwa hai, nazungumza naye, nafuatilia kisa chake choote na mazungumzo yetu yoote na nilikuwa nayaandika katika shajala yangu … na mpaka siku ya mwisho anapotea nilijua alikuwa wapi na nilifuatilia alikuwa na nani na walikwenda wapi na nikafuatilia hadi watu waliohusika kumkamata , wakati ule nikawajua nikawafuata na kuzungumza nao kila mtu akaelezea jambo lilivyokuwa zito na baada nikaja kusikia mtu mmoja akaniambia kuna mwili upo hospitali mojawapo na tunahisi ni huyo huyo bwana Ben Saanane, nikataka kujua huo mwili ni wa kweli mwili wake jamaa mmoja akasema ni kweli ni mwili wake kwa hiyo imekuwaje?
Mpaka mwili huo mwili ukafika hospitali? Mwili umetokea wapi? Mpaka kuchunguza kujua mwili huo ulitoka wapi ilinichukua mwaka mzima hadi mwaka 2018, lakini hili jambo nilizungumza na watu zaidi ya 30 na ni watu walikuwa labda wanafahamiana lakini hawafanyi kazi kwa karibu, walikuwa wanalijua jambo hili huku masimulizi yao yalikuwa yanafanana juu ya kitu gani kilichotokea siku hiyo.
Mtu mmoja alinisimulia akaniambia unajua Bwana Mkubwa jambo hili alilitenda kwa sababu alikuwa na hasira sana siku hiyo na alikuwa na hasira na ndiyo maana baada ya kulifanya hilo tukio alitetemeka sana, mpaka silaha ikaanguka chini (maana yake kwa mkono wake mwenyewe)…nilikutana na watu wengi niliyokuwa ninaaminiana nao na kuheshimiana nao sana maelezo yalikuwa yale yale ya kilichotokea…na wale mabwana walisema alipata masikitiko na alifadhahika na alijutia. Unapojutia jambo unaonesha kujua je familia yake inajua kuwa alijutia, kwanini mlikwenda kuutelekeza mwili wake kule kwa kuua ushahidi kwa nini mmefanya hivyo? Ili jambo likatupa shida sana kuliweka kitabuni…”
Haya ni maelezo ya mwanahabari Erick Kabendera ambayo yanatoa mwangaza mpya kwa jamii ya Watanzania.
Kwa hakika Mwanakwetu ameyasikiliza mahojiano haya vizuri na kwa hakika kama yaliyosemwa ni kweli mbele ya Mungu, yanaonesha kitu kimoja kibaya sana, kama tunampa mtu majukumu, je yupo anayeweza kumdhibiti baada ya kumkabidhi mtu madaraka haya kama kukiwa na kukengeuka?
“Je chama cha siasa kilichompa dhamana, Je nani? Au Mwanakwetu akiwa na madaraka anafanya atakavyo? “
Haya yanayotajwa ni madhaifu ya John Pombe Magufuli ambaye amelala kaburini, je wangapi wanayafahamu haya?Je wangapi wameshuhudia haya? Je hii ilikuwa tabia ya mtu mmoja tu? Kama madhaifu hayo ni ya kweli na udhaifu wa mtu mmoja tu, je kuna uhakika gani yaliyotokea yasijirudie tena juzi, jana, leo na hata kesho katika ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Je kuamini kuwa madhaifu yote ya Serikali ya Awamu ya Tano yamelala kule Chato Mkoani Geita ni dhana sahihi, Je yamezikwa kweli au tunazungukwa nayo mchana na usiku?
Erick Kabendera ameeleza yaliyomkuta Ben Saanane vipi Azory Gwanda lakini wapo Watanzania wangapi pengine wanajua mengi yaliyotendeka na wataendelea kuyasimulia mengi juu ya hali hizi za vifo vya Watanzania kadhaa kwa nyakati tofauti?
Katika hali hii ya tuhuma nzito kwa marehemu Magufuli wapo wanaoamini kuwa John Pombe Magufuli anabebeswa mzigo wa lawama kwa kuwa hayupo duniani na wapo wengine wanaoamini kuwa tuhuma hizo zina ukweli.
Swali la kujiuliza je kwa sasa Watanzania wana wajibu wa kuchagua moja katika ya haya mawili; Kuieleza Jamii ya Watanzania kilichotokea na Watanzania wafanye maamuzi au Tuendelee kukaa kimya?
Kikubwa hili la kukaa kimya Mwanakwetu anaona halina maana na tija kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni mali ya watu. Nakuomba msomaji wangu kulielewa jambo hili nakurejeshi nyuma kidogo katika kisa kimoja wakati wa utawala wa Jakaya Mrisho Kikwete akiwa madarakani.
“Mara baada ya kuingia madarakani Rais wa awamu ya nne ndugu Jakaya Kikwetu, wananchi walilalamika kuwa waliofanya mauwaji ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na kuhukumiwa na mahakama, walipewa msamaha kinyemela, jambo hilo lilianza kama uvumi kisha vyombo vya habari kuripoti. Jamaa hao waliokuwa askari nadhani Kituo ch Oysterbay wakati wa tukio hilo kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, Walishitakiwa kwa kosa la kuumimiminia Risasi Mtanzania mwenzetu Afande mwenzao kutoka JWTZ Imrani Kombe(Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa).
Serikali ya Dkt Jakaya Kikwete ilibebesha mzigo wa lawama hizo kwa kuwa jamii ya Watanzania ilibaini kuwa askari hao wa zamani wa Jeshi la Polisi Tanzania walionekana mitaani. Swali likaja haya mambo yakoje? Wakati Mahakama imewatia hatiani na iweje Rais Kikwete amewapa msamahaa?
Jambo hilo likaleta maneno, vyombo vya habari vikahoji sana hadharani na wakati huo vyombo vya habari vya uchunguzi vilikuwa mahiri mno kuliko wakati wowote nchni Tanzania. Baadaye Msemaji wa Ikulu ya Tanzania wakati huo Salva Rweyimamu akatoka hadharani na kusema kuwa jambo hilo ni kweli lakini hawa jamaa wamepata msamaha na serikali iliyofanya hivyo siyo ya Awamu ya Nne bali maamuzi hayo yalifanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu wakati inakaribia kumaliza muda wake.”
Hali ya Serikali ya Awamu ya Tatu na ile ya Awamu ya Nne palikuwa na utafauti mkubwa hasa ukitazama na hali ilivyo ya sasa baina ya Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita. Tazama juu ya kura za kuiweka madarakani kura ni zile zile, Makamu Rais kawa Rais maana yake ridhaa ya wananchi bado ni ile ile, kwa hiyo tuhuma dhidi ya John Pombe Magufuli au sifa dhidi ya John Pombe Magufuli kati ya 5 na 6 tunaweza kuzitenganisha?
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mosi, vipi kuhusa umma wa Tanzania kuelezwa kipi kilitokea? Changamoto ilikuwa ni nini? Upi ni uhakika wa mambio haya kutojirudia? Maana kwa mujibu wa mila za Kiafrika tunapolia misiba lazima tuzike kisha tunanyoa vipara kila mmoja, kama wewe una wigi, kama umeweka zaazuuu, kama umeweka relax kama umechana Afro zote zinanyolewa kila mmoja na kipara.
“Kinyume chake familia zilizopoteza wapendwa wao moyoni wanamanung’uniko mengi na haya malalamiko hayawezi kuisha leo yatadumu milele dhidi ya ndugu wa wanaotuhumiwa kufanya ubaya huo au wale waliokuwa jirani na watuhumiwa hao.”
Kwa hakika suala hili tuna wajibu wa kuamua kunyoa nywele zetu na kubaki na vipara lakini kuamua kukaa kimya ni hatari zaidi. Ndugu zangu Wataznania tujifunze katika kile kisa cha Jakaya Kikwete na serikali yake ya awamu ya nne juu wa wale askari wa zamani wa Kituo cha Polisi Oysterbay waliotiwa hatiani kumiminia risasi ndugu yetu Afande Imrani Kombe akiwa ni Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa wakati huo na walipewa msamaha jambo hili lilimuibua Salva Rweyimamu alitoka Ikulu ya Magogoni na kusema na Watanzania na alieleza nani aliamua hivyo na malalamiko yalikwisha.
Pili, Mwanakwetu ameyasikiliza mahojiano haya vizuri, binafsi anampongeza Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam wakati huo Mohammed Khelefu kwa kufanya kipindi hiki makini hii inaoneka wazi wazee wetu akina Othmani Miraji walimpika na kupikika lakini hili pia inaonesha namna vyuo vya Tumaini vinavyomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT vilivyowapika wanahabari mahiri akiwamo yeye (Mohammed Khelefu.)
Tatu, uhai wa raia yoyote yule unapaswa kuwa na umuhimu na kupewa thamani kuliko cheo cha mtu mwingine yoyote katika ardhi ya huu ulimwengu.
Mwisho wale wanaofanya kazi katika vyombo vya Ulinzi na Usalama jamani tunawategemea sana msituangushe, nacho CCM kiwe makini na viongozi wetu na CCM ihakikishe usalama wa raia na mali zao unakuwepo na viongozi wetu wafanyiwe tathimini ya haki kama wanalinda uhai wa binadamu au la?Hili liwe jukumu namba moja kwa CCM kama chama cha siasa.
Mambo haya dunia ina kumbuka mauwaji ya Thomas More na Askofu John Fisher kule Uingereza mwaka 1535 enzi za utawala wa Mfalme Henry wa VIII.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Tunyoane Vipara.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment