Adeladius Makwega –Butiama MARA.
Mwanakwetu yu katika gari aina Toyota Land Cruzer mpya kabisa huku akiwa na watu wengine kama saba wakitoka Musoma Mjini Kwenda Vijiji vya Halmashauri ya Wilaya Butiama. Ndani ya gari hii mijadala ilikuwa ni ya siasa za Tanzania, juu ya kukamatwa kwa Dkt. Wibroaa Slaa ambaye yupo kolokoloni kwa muda sasa. Awali Dkt Slaa alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweeden baadaye ya kustaafu na waungwana wakampoka heshima hiyo ya Ubalozi na kupikwa mkasi.
“Unaona Dkt. Wilbroad Slaa kakamatwa na hajapata hata mtu wa kumtolea dhamana, unajua mtu ukiwa na shida unakosa hata mtu wa kukusaidia, siunaona yule Mkuu wa Mkoa wa Geita wa zamani alipotumbuliwa akakosa hata watu wa kumpigia simu.”
Dereva wa gari hii anapiga gia zake vizuri, dereva akaingilia mazungumzo haya akasema, jamani hizo hoja siyo kweli Dkt. Slaa amenyimwa dhamana kama dhamana ingekuwa wazi asingalikosa wa kumdhamini. Jamaa mwingine akasema Dkt Slaa kazidi , ameongea mambo mengi ya akina Mbowe kwa nini? Jamaa wanaongea, mjadala wa moto garini. Mwanakwetu hapa hapa akajisemea moyoni Watanzania ni hodari mno wa kuyasema mambo hata kama hawayaelewi, Mwanakwetu akaendelea kujisemea moyoni.
“Shauri hili lilipelekwa mbele ya hakimu wa mahakama ya Kisutu mhe. Beda Nyaki Januari 10, 2025 maana Dkt Willbroad Slaa alifunguliwa kesi namba 993 ya mwaka 2025 kwa kosa analodaiwa kutenda la kusambaza taarifa zinazo daiwa ni uwongo katika mtandao wa X, zamani twiter.”
Mwanakwetu kumbuka yupo na watu karibu saba wanaelekea Butiama, wakitokea Musoma Mjini. Kweli gari hilo lilifika eneo lenye makazi ya zamani mno, jamaa mmoja akasema hapa pana popo wengi! Wakashuka na kukaribishwa na nyumba kadhaa zenye chokaa nyeupe iliyofubaa na kuchujuka sana, madirisha ya mbao ya zaamani, huku kila nyumba ikiwa na banda la mifugo na hasa hasa mbuzi na kondoo walionekana wakila kando majani. Mwanakwetu alipotaza mabanda haya yalikuwa na mbuzi na kondoo wasiozidi watatu kila banda.
Hapo hapo Mwanakwetu aliwaacha kundi alilofika nalo na wakiwa wanaongea na yeye kwenda kukaa kando ya makazi haya ambayo kulikuwa na sehemu ya kukaa kama benchi lakini lililojengwa kwa sakafu. Akiwa hapa aliona nyumba mkono wa shoto mlango unafunguliwa huku anatoka Ajuza mmoja mtu mzima, alifungua mlango kama mtoto kisha mama mmoja kuja kumsaidia kutoka katika kizingiti cha makazi haya , huku akitambaa kuelekea katika ukumbi wa taasisi hii. Mama huyu akiwa na mama anayemuongoza alitumia dakika 10 kutembea kwa kutambaa katika umbali usiozidi mita 100, huku mama huyu nguo zake ziliburuza vumbi na mwili wake amevalia nguo nyingi ili kuepusha miguu yake kuumizwa na sakafu, miba wadudu katika ardhi ya eneo hili la Nyabange hapa Butiama mkoani Mara. Haya mazingira yalimsumbua mno Mwanakwetu ambayo ni hali ya kwanza ya mazingira ya huzuni aliyokutana nayo kwa mara ya kwanza akiwa mkoani Mara. Mandhari hii ya kusikitisha ilimbeba Mwanakwetu mzegamzega hadi mwaka 2006 akiwa mkoani Iringa,
“CCM mkoa wa Iringa ilimpokea Marehemu Kingunge Gombale Mwiru , nadhani alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, akafika akapokelewa na viongozi wa CCM Mkoa huu wa nyanda za juu ya Tanzania. Mwenyekiti CCM mkoa wa Iringa akiwa ni Mzee Mmoja ambaye jina lake limesahuliwa leo hii na Mwanakwetu, wakati huo kabla ya Jah People na Philip Manhgula hawajagombea nafasi hiyo.
Kigunge akiwa mkoani Iringa aliwatembelea wazee wenzake kadhaa aliyokuwa nao zamani Umoja wa Vijana wa TANU na baadaye CCM waliyokuwa hai. Mzee mmoja alikuwa mkazi wa Kata jirani na Kihesa na Gagilonga. Kigunge akiwa anakwenda huku Adeladius Makwega Kiongozi CCM kutoka Tawi la CCM Tumaini Iringa akiambata na wajumbe wachache wa Kamati ya Siasa Kata ya Kihesa waliagizwa watangulie nyumbani kwa mzee huyo, katibu Kata ndugu Mwakiyoma, Mwenyekiti CCM Kata Wazazi Mzee Lukas Mgongolwa na mama mmoja Kiongozi wa UWT wa Kata ya Kihesa wakakutana Ofsi ya CCM kata kisha kuelekea kwa mzee husika kwa miguu, wakafika nyumba hii na kweli baada ya muda mchache Mzee Kingunge alifika na kumsalimu Mzee mwenzake huyu mgonjwa na kuwasalimia wote waliokuwapo alafy akaomba watoke nje, ndani ya makazi haya akabaki Mwenyekiti CCM Mkoa wa Iringa , Kingunge na huyu mzee mgonjwa, wakaongea na baada ya muda tukaambiwa turudi sebuleni.
Marehemu Kingunge akawa anasema,
‘Msimuone Huyu Hivi Alikuwa Machachari Sana Alipokuwa na Nguvu Zake.’
Jamaa wakawa wanacheka. Mzee huyu baada ya ugeni wa Kigunge alipata matibabu vizuri sana lakini mwishowe alifariki dunia.”
Mwanakwetu akiwa na mawazo haya ya tukio hilo la mwaka 2006, wakaja watu wanne; wazee wawili, mama wa makamo mmoja na dada mmoja, hapa kwenye sakafu hii kukawa watu wanne na Mwanakwetu watano. Binti mmoja ambaye nadhani ni Afisa Ustawi wa Jamii akiwa hapa wakapita mtu na mkewe kasha akasimulia kisa hiki,
“Mzee mmoja alikuwa na mkewe, hapo kijijini wakazaa naye mabinti wengi, baadaye huyu mzee akaondoka na kwenda Mwanza kuishi na mama mwingine, huko akaanzisha maisha mengine mapya na wamama wa Kisukuma. Nyumba ya awali akatupa jongoo na mti wake. Mwanamke wa Mara anaendelea na maisha yake mabintizake wadogo akawalea vizuri wakawa wakubwa, wakati wakuozesha ulipofika, mke akatuma mjumbe kumjulisha hilo mumewe huko Mwanza,
‘Mume wangu njoo, binti kapata mchumba, mume wangu njoo binti kapata mchumba.’
Maneno haya yakawa yanajirudi kila mara mithili ya CD iliyogoma cheza katika ukumbi wa muziki hapa Musoma Mjini.
Kweli akafika akapokea ng’ombe baada ya kuoza mabinti zake hao desturi aliswaga ng’ombe hizo na kwenda nazo mnadani kuziuza. Kazi hiyo ilifanywa kwa mabinti zake wote 1-10 na kutokomea Mwanza. Alikaa Mwanza wee umri umemzidi akaamua kurudi zake kwao kwa mkewe wa kwanza , kweli mkewe akampokea na kukaa naye, maisha yakawa yanaendelea.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu amekaa na watu hawa wanne na binti anaendelea kusimulia.
“Hapo Serikali inaendelea na mipango wake ya Kaya Masikini, katika mkutano wa mmoja wa kijiji nilioshiriki wananchi wakawa wanasomewa waliobahatika kupata fedha za Kaya Masikini akiwamo mzee huyu muuza ng’ombe na posa na kutokomea Mwanza. Katika mkutano huu wa kijiji wakapinga na kutamka hadharani hawamtaki mzee huyu kijijini, maana alikuwa akimpiga mkewe na kutokutunza ng’ombe za posa za wanawe..
Mkuu Wilaya mkutanoni yupo anatatua mgogoro huo, hali ilikuwa tete, kuokoa uhai wa huyu mzee ikaamuliwa atafutiwe makazi mengine akaishi kama makazi ya wazee.”
Binti huyu Afisa Ustawi alipomaliza kuzungumza hayo aliinuka na kwenda kuongea na watumishi wenzake kando. Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu alikuwa jirani na watu wengine watatu kumbuka pia jamaa wawili walikuwa wazee nao ni Bibi Amina Saire Magoti ambaye alijitambulisha kama Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Mara na Joseph Nyiraha ambaye alijitambulisha kama Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wazee Mkoa wa Mara.
“Shida latika maisha inaweza kuwa mtu mmoja kati ya mume au mke, pia shida ya pili inaweza kuwa kwa watoto na ndugu na tatu shida inaweza kuwa kwa jamii zungukwa. Katika kisa hiki shida naona ni jamii zunguka.”
Haya yanasemwa na na Mzee Nyiraha, mzee mtanashati akiwa na suti maridadi ambayo Mwanakwetu aliipenda Suti ya Mzee huyu.
“Hapa akija Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara nitamuomba afike hapo atazame hali ilivyo maana hakuna uwekezaji wowote mkubwa uliofanyika hadi sasa.”
Wazee hawa watu wazima yaani Mzee Nyiraha na BI Magoti ambao waliwatembelea wazee wenzao katika Makazi ya Wazee ya Nyabange hapa Butiama Mkoani Mara wanaongea juu ya mustakabali wa kituo chao wanapoishi ndugu zao wazee wenzao 14.
“Unajua hata Naibu Waziri Jumanne Sagini ambaye ndiye Mbunge wa Butiama na yeye tumwambie aweke nguvu zake katika kituo hiki kilichopo katika jimbo lake, vinginevyo tutaomba kituo hiki kihamie Manispaa ya Musoma. Hapa lazima aje Makamu Mwenyetikiti wa CCM Bara anaweza kutoa agizo pakaboreshwa.”
Mjadala huo ulivyokuwa unapamba moto mara aliyekuwa anagojwa alifika na kuendelea na shughuli katika makazi haya ya Wazee Nyabange Butiama mkoani Mara.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kikubwa ni kila anayesoma makala haya, akumbuke utu uzima una mambo mengi, hata kama unaweza kuwa unajiweza lakini afya ikaporomoka, hivyo suluhu ya kulinda uhai wako ukahamishiwa Hospitali, kumbuka hospitali nayo ni makazi kama haya ya wazee.Wengine wanakumbwa na umaskini wa watoto anakosa mtu wa kukaa naye ili kumfichia aibu zake, wengine umaskini wakipato nayo ni balaa na wengine jamii zunguka kuwakataa, haya ni machache kati ya mengi sababu, kwa hiyo kwa mwanadamu mwenye nguvu leo hii kumbuka lolote linaweza kukukuta, kwa hiyo maboresho ya Vituo vya Wazee kama cha Nyabange, na hata Hospitali zetu ni jambo la lazima.
“Chakufanya unaweza ukafanya ukarabati wa nyumba moja, mwingine akapiga rangi nyumba pili baada ya miaka miwili nyumba zote za makazi ya wazee zitakuwa bora.”
Msomaji wangu kumbuka maelezo yale ya Kingunge Gombale Mwiru pale Kihesa Gangilonga Iringa Mjini kwa yule kijana mwenzake wa zamani wa TANU na CCM akisema,
“Msimuone Huyu Hivi Alikuwa Machachari Sana Alipokuwa na Nguvu Zake.”
Hakuna anayeufahamu mwisho wake utakuwaje, kwa familia nyingi hivi sasa wazee wanazunguka majumbani mwa watoto wao waliowazaa ili kutunzwa maana vigumu watoto wao kurudi kuwatunza baba/mama zao katika makazi yao kutokana na kujitafutia kipato, hawa wazee wakifariki tu ndipo maiti zao zinarudishwa kwenye makazi yao ya awali ili kufanyika sala za mazishi, kikubwa tuombe tuwe na mwisho mwema .
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka,
“Msimuone Huyu Hivi Alikuwa Machachari.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
NB
Makala haya yametayarishwa na MwAnAkWeTu Januari 27/28, 2025 hapa Butiama Mkoani MARA kwa Heshima ya Marehemu Mzee wetu Kingunge Gombale Mwiru.

Post a Comment