Adeladius Makwega Musoma MARA
Mwishoni mwa miaka 1980 mahusiano baina ya eneo la Mbagala na Mtoni yalikuwa karibu sana kwani yalikuwa ni vijiji vilivyomo katika jimbo moja la Uchaguzi la Temeke chini ya mbunge wao marehemu Masoud Ali Masoud a.k.a BEDUI jamaa mmoja mfupi, chotara, Muisilamu mwenye roho nzuri.
Jamii hizi mbili za Mtoni na Mbagala zilikuwa zinafahamiana kidugu na kiimani maana ilikuwa ni jambo la kawaida vikundi vya madrasa kwenda Mbagala kufanya Maulidi na vya Mbagala kwenda Mtoni kushiriki Maulidi hizo kwa dini ya Kiisilamu.
“Kwa upande wa Wakristo ambayo ndiyo jamii ya Mwanakwetu tangu awali Kanisa la Kwanza linakadiliwa kujengwa mwaka 1939 kwa kadili za simulizi za Wakristo wenyeji, hili ni Kanisa Katoliki la Mtakatifu Antony wa PADUA ambalo lipo hadi leo hii ndani ya Kituo cha Kiroho Mbagala na kipindi hicho hicho ndipo uliposimikwa Msalaba wa Mbagala Msalabani ndani ya Kiwanda cha Nguo cha Karibu.
Huku kwa kadili za simulizi za kale, Wakristo wa madhehebu mengine walichagua moja kati ya haya; kusali Kanisa Katoliki Mbagala Misheni au kufunga safari hadi Temeke Mwisho na Posta ambapo madhehebu hayo yalikuwa na makanisa.”
Nakumbuka hata kwa wale wapenzi wa mchezo wa soka wa Mbagala nyakati hizo walifunga safari hadi Mtoni Mtongani kwa Mzee Komba ambaye alikuwa anamiliki televisheni na mitambo mikubwa ya kunasa mawimbi ya runinga na kutazama mechi za kombe la dunia la mchezo wa soka mwaka 1986.
Mwanakwetu anatambua wasomaji wa makala haya wapo wengi ni wadogo kwa umri na wapo wengi wakubwa lakini hawakuwepo katika ulimwengu wa soka na hata ulimwengu wa habari nadhani itakuwa vizuri niwakumbushe kitu kidogo juu ya Kombe la Dunia la mwaka 1986.“Mashindano haya yalifanyika Maxico(MEKIKO) na Diego Maradona alikuwa mshindi wa Mpira wa Dhahabu akiwa mchezaji bora wa michuano hiyo, huku Gary Lineker wa Uingereza akishinda Kiatu cha Dhahabu akiwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia akiwa na mabao sita , Kwa sasa Gary Lineker ni mwanahabari.”
Ebu fikiria mwendo wa mguu kutoka Mbagala Kizuiani, Mbagala Rangi Tatu au Mbagala 77 hadi Mtoni Mtongani, hoja ni kutazama mpira tu, huu ulikuwa ulevi mkubwa wa mchezo wa soka.
Msomaji wangu tambua kuwa Mwanakwetu japokuwa hakuwa mlevi wa mchezo wa soka lakini yeye na rafiki yake Fredrick Mwambene, Rashid Mng’oi na Antony Masele waliitazama mechi ya fainali kati Argentina na Ujerumani nyumbani kwa Mzee Komba, hapo Mtoni Mtongani wakitokea Mbagala Sabasaba umbali kama wa KM 5 kw mguu huku njiani kukiwa na wakabaji wengi, lakini kwa bahati nzuri wakabaji hawakujaribu kuwakaba wapenzi wa kuangalia kombe la dunia la mwaka 1986 ambapo Argentina ilishinda kwa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Ujerumani Magharibi.
Msomaji wangu sitaki kuingai ndani katika mechi hii maana siyo mada ya makala haya, bali hoja ni juu mahusiano baina ya Mbagala na Mtoni wakati huo.
Parokia ya Mbagala wakati huo ilikuwa na Padri Muitaliano marehemu Padri Fidelis na Parokia ya Mbagala ilikuwa inamiliki Shule ya Sekondari ya AMET(Sant Antony Of Padua Sekondari School ya sasa), na eneo la jiografia la Parokia hiyo lilianzia Mtoni Mtongani hadi kuelekea maeneo ya Wilaya ya Mkuranga na Mafia. Huyu Padri alikuwa na eneo kubwa la kuhudumia huku akisaidiwa na mapadri kutoka parokia za Kurasini na Sant Joseph hasa wale Wamisionari wa Afrika (White Fathers)
Kutokana na eneo la huduma hiyo ya kiroho kuwa kubwa, kuna siku Padri huyu akiwa na vijana nne siku ya Ijumaa Kuu wakizunguka kufanya ibada ya siku hiyo muhimu vigangoni walivalia kanzu zao nyekundu wakizunguka katika vigango kusalisha Ijumaa Kuu.
Kigango cha mwisho kwa siku hiyo muhimu kwa Wakristo kikawa Mtoni Mtongani. Walipomaliza ibada hiyo ya Misa ambayo huwa ndefu sana alikuja muumini mmoja ambaye alisema kuwa nyumbani kwake kulikuwa na mgonjwa ambaye alihitaji huduma za kiroho kwani alikuwa katika hatari ya kufa.
Muumini yule mwenye mgonjwa alichukua baiskeli yake na kutangulia nyumbani kwake mbele, huku vijana wale wanne na Padri Fidelis wakija nyuma wakiingia na kanzu zao ndani ya Gari ndogo kuelekea kule Mtoni Relini kutoa huduma hiyo ya kiroho.
Walifika na gari na iliachwa mlimani kwa juu kwa kuwa waumini hao wenye mgonjwa walikuwa wakiishi bondeni njia ilikuwa haipitiki kwa gari. Baba Padri akielekea kutekeleza jukumu lake na sasa kusindikizwa na baadhi ya ndugu wa mgonjwa na huku akiongozana na vijana wake wale wanne wakiwa wamevalia kanzu zao nyekundu baada ya Ibada ya misa.
Msomaji wangu miongoni mwa vijana hao alikuwamo Mwanakwetu. Tukafika Padri Fidelis akamsalia mgonjwa na mwisho kumpa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu, tukamaliza na kuanza sasa kurudi kwa mguu kule juu mlimani maana huku walipo hii familia mabondeni na gari haikuweza kuingia kabisa.
Tulipokuwa tunarudi kwenye gari liliibuka kundi la vijana na watu wazima wakishangazwa na watu waliovalia kanzu nyekundu.
“Eee bwana nyie vipi ? Mbona mmevaa kanzu nyukundu ? Wanyonya damu? Ahh hawa wanyonya damu hawa. “
Tukawa tunawaambia hawa jamaa hawa jamaa, siye siyo wanyonya damu tunatoka kumuona mgonjwa, hapo bondeni, ndugu yake huyu hapa, Padri katoka kumsalia mgonjwa. Jamaa hawakuelewa somo. Watu wakawa wametuzunguka huku wakiimba nyimbo.
“Wanyonya damu hooo, haoo haoo ,
Wanyonya damu haooo haoo haoo
Wanyonya damu haoo, haooo haooo
Wanyonya damu haoa haooo haoo.”
Yule jamaa aliyemwomba Padri kuwa alikuwa na mgonjwa alikuwa siyo Mkristo mwenyeji na eneo la Mtoni Relini, ambapo wenyeji Wakristo walikuwa Wamakonde na Wafipa wachache, huku eneo hili lilikuwa msitu wenye mikorosho na minazi mingi, hawa watu walikuwa wagumu kumuelewa huyu Mkristo ambaye tulikuwa naye ana anatusindikiza. Eneo hili Wakristo hawakuwa wengi na hata Ijumaa Kuu ilikuwa haifahamiki vizuri.
Basi ilibidi watu walipojaa ikaamuliwa atumwe kijana mmoja nyumbani kwa mzee mmoja ambaye alikuwa ni udugu na mtangazaji wa Redio Tanzania (RTD) anaitwa Kisunga Steven alikuwa akijulikana kama Mzee Kisunga. Mzee huyu alikuwa Mkatoliki Mfipa maarufu na nyumba yake ndiyo ilikuwa jirani, mzee huyu akaja kuja kuokoa jahazi la vijana wanne na Padri Fidelis.
Eneo hili lilikuwa na familia zingine za Wakristo Wakatoliki mathalani baba mzazi wa mwanamuziki Vitalis Maembe lakini nyumba yao ilikuwa mbali kidogo na tukio hili siku hiyo.
Mzee Kisunga alipofika akawaambia,
“Jamani huyu ni Padri wetu na hawa vijana wenye kanzu nyekundu ni wahudumu wa kanisani, kwetu hapa Mtoni Bado tunahangaika kujenga Kanisa, japokuwa tunacho kiwanja, hawa wahudumu wa kanisa wanatokea Mbagala ndiyo maana hamuwafahamu, wamekuja kutoa Mpako Mtakatifu kwa Mgonjwa wa huyu ndugu yetu, hawa siyo wanyonya damu.”
Kidogo maelezo ya Mzee Kisunga yakawaingia jamaa hawa wakawa kimya,wakaacha kuimba wimbo Wanyonya damu hao hao haoo tukaongozwa na Mzee Kisunga hadi pahala ilipoachwa gari aina ya Golf na kurudi Mbagala Misheni, salama salimini.
Tukio hili la mwaka 1986 lipo akilini mwa Mwanakwetu ambaye alikuwa kijana mdogo wakati huo. Mwanakwetu hana hakika kama Padri Fideli alilifanyia documentation tukio hili wakati ule. Mwanakwetu anakumbuka sana maana hbari ya Wanyonya damu(Muumiani) lilikuwa jambo la hatari. Inakuwaje sisi na Padri sisi na Padri Fidelis tuitwe wauumiani?
“Wakati huo muumiani alifahamika kama mtu ambaye alikuwa akiwavizia watu kwa siri na kuwanyonya damu na yule aliyenyonywa damu alikufa, alikishanyonywa damu anagongwa muhuli kasha serikali haifuatilii jambo hilo na enzi za mwalimu Nyerere Iliaminika kuwa damu hiyo ilikuwa inauzwa kwa fedha nyingi sana. Watuhumiwa nambari moja wa matukio haya walikuwa ni wale waliokuwa matajiri wa maeneo kadhaa. Ikiaminika kuwa utajiri wao ulipatikana kwa kunyonya watu damu.
Hata magari ya msalaba mwekundu na wahudumu wa afya walipata changamoto hiyo kwani katika maeneo waliyotembelea wananchi waliweza kupiga kelele kuwa jamani wanyonya damu wamekuja hasa maeneo ya shule, vyuo na taasisi zingine zenye mikusanyiko na hilo lilikuwa tatizo kubwa. Hata zoezi la uchangiaji wadamu lilikuwa likikumbwa na changamoto hiyo. Kwa hiyo taharuki ya muumiani kwa hakika iligharimu sana taifa letu huku ikileta chuki miongoni mwa watu.”
Mwanakwetu kama mwanasiasa anakumbuka,
“Mwaka 2010 katika uchaguzi wa kura za maoni za CCM mgombea mmoja ambaye alikuwa akiomba kura kuchaguliwa kuwa diwani katika kata mojawapo jimbo la Kigamboni wakati huo ikujumuisha na Mbagala alituhumiwa kuwa baba yake alikuwa muumiani(nyonya damu)
Wafitini wakisema kuwa hawamtaki kwa kuwa baba yake aliwatesa wazazi wao na kama anataka uongozi awe kiongozi wa familia tu na siyo kuwa diwani wa kata yao. Tuhuma hizo zilivuma sana kama zilikuwa za kweli au laa lakini zilitumika kumuangusha mgombea huyo.”
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?
Kwa sasa jamii yetu ya Tanzania kumeibuka suala la watu wasiojulikana, hali hii Mwanakwetu anaifananisha na ile ya muumiani, nina hakika unaweza mtu kutuhumiwa na jambo ikawa siyo kweli au ikawa kweli.
Mwanakwetu kwa moyo mweupe ana hakika na imani kuwa yapo majina ya watu wa leo hii miaka ijayo vizazi vyao vitatuhumiwa kuwa wao ndiyo walikuwa ni watu wasiojulikana na watoto watoto wao watasontwa vidole , wapigwa masingi, watanangwa hadharani na watanyimwa baadhi ya vitu, kazi na nafasi kutokana na tuhuma hizo bila kujalia kama wanaotuhumiwa walifanya kweli au la.
Ni vizuri jambo hili la watu wasiojulikana lifanyiwe kazi kwa ngazi zote ilikuondoa kutokuaminiana baina ya sisi kwa sisi, Watanzania kwa Watanzania, wenyewe kwa wenyewe. Hapo hakuna mgeni wa kulaumiwa na kama kulaumiana ni kwa Watanzania wenyewe, tusipokomesha habari za watu wasiojulikana damu hizi haziendi bure kutaendelea kuumizana vizazi kwa vizazi , chuki na chuki ,Fulani na Fulani, baba yake alifanya hivi, mama yake alifanya hivi .
“Fikiri tu unaweza kusema mathalani leo Mwanakwetu labda kiongozi nina ulinzi saa 24 siku saba mwezi mzima, mwaka mzima milele lakini baada ya miaka kumi nimezikwa mjukuu wangu hana ulinzi, ulinzi wa mjukuu na kitukuu changu ni wema niliyowafanyia watu wengine. Baba yake huyu jamaa alitujengea shule.Baba yake huyu jamaa alikuwa anatutibu kwa wema na siyo mama yake huyu jamaa alikuwa anawalinda watu wasiojulikana.”
Fikiria yule mgombea wa udiwani wa kura za maoni CCM, fitina zilitolewa na kumchafua mno hakuna anayetambua ukweli wa tukio hilo lakini tayari alishachafuliwa lakini swali la kujiuliuza je kwanini hawakuwatuhumu wagombea wengine? Watu wengine katika tukio hilo?Maana yake pahala fulani palikuwepo na shida.
Kumbuka tu kisa cha Padri Fidelis na wale vijana wanne waliponea tundu la sindano kudhuliwa kwa tuhuma za wanyonya damu wakati wao siyo wanyonya damu. Ifahamike kuwa kwa wale wenye watoto, hata kama wewe hautokuwepo duniani basi majina yetu yanabaki kupitia watoto wetu, vizazi vyetu wao wataishi kwa namna vile jamii ilivyokuwa inatupima mimi na wewe na si vinginevyo.
Hapo hautokuwepo Mzee Kisunga wa kuja kuokoa jahazi wa kutetea kuwa hawa siyo wanyonya damu, hawa siyo watu wasiojulikana bali wamekuja kutoa Mpako Mtakatifu.
Mwanakwetu upo ?
Kumbuka
“Ijumaa Kuu Ninayoikumbuka.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment