MVUTO ENEO KUBWA BARA YA TANZANIA

 



Adeladius Makwega –TARIME MARA

Nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi yenye kuteua katuni nne katika kapu la katuni tele zilizochorwa na wachoraji mbalimbali kisha kuielezea katuni moja baada ya nyingine na kuambatanisha na uchambuzi wa katuni hizo.

Kuyaanza makala haya Mwanakwetu anaikamata katuni ya kwanza ambayo imechorwa na King Kinya ambapo kunaonekana jamaa mwenye haiba kama ya Tundu Lissu Makamu Mwenyekiti CHADEMA Bara yupo katikati ya vifaa viwili; mbele fagio na nyuma yake kizolea cha takataka, macho ya huyu jamaa yanatazama ufagio huku kichogo chake kinakaribiana na kizoleo cha takataka, huku juu ya kichwa cha huyu jamaa kumepachikwa alama ya mshangao.

Mtayarishaji wetu anapoitazama katuni hii inaonesha wazi kuwa je huyu Tundu Lissu na harakati zake za kugombea Uenyekiti wa CHADEMA atafagiliwa kisha kuzolewa mbali na kutupwa kusikojulikana?

Kwa hakika katuni hii ya King Kinya inaibua maswali ambapo jamii ya Watanzania wapenda Demokrasia akiwamo Mwanakwetu wana maswali mengi likiwamo hilo. Huku dhana kadhaa zikijengwa.

“Tundu Lissu kapewa ahadi ya cheo kikubwa kutoka utawalani, Tundu Lissu akishindwa Uenyekiti atakimbilia ACT WAZALENDO maana huko kahakikishiwa atagombea URAIS na huko CHADEMA kugombea tena urais 2025 linahisiwa mambo yatakuwa kama yalivyomkuta Dkt Wilbroad Slaa ambapo baadaye alikimbilia ughaibuni baada ya nafasi hiyo kupewa Edward Lowassa.

Tundu Lissu anagombea Uenyekiti CHADEMA ili ajihakikishie kugombea Urais  2025 ?”

Kwa hakika msomaji wangu hizo zote ni dhana tu na kuwa na dhana si dhambi hata wanadamu wanazo hisia nyingi sana juu ya uwepo wa pepo baada ya kufa, hata kama hakuna aliyekufa na kurudi kuja kutuambia huko peponi kuna nini, na nini na nini?

Kikubwa kwa hili la uchaguzi wa CHADEMA tusiandikie mate, tungoje maamuzi ya siku ya kupiga kura yataamuliwa na wanaCHADEMA.


 

 

Sasa Mwanakwetu anaikamata katuni ya pili ya Shirika la Utangazaji la Ujerumani DW Kiswahili ambapo mchoraji wake ni Said wa Michael. Karagosi hii inaonesha jamaa wawili wamekaa katika kitu kama mzani ambacho egemeo lake ni jiko la moto, hawa jamaa wajihi wao unaonesha ni Mbowe na Lissu kama wako ulingoni kwa ajili ya pambano la Kiti cha Mwenyekiti.

Hili jiko la kati limepewa jina wapambe, naye Lissu akisema huu uzito unamfahaa naye Mbowe akisema atatea mkanda wake Hapa Mbowe akiwa na bango la uenyekiti CHADEMA kwa miaka 20.

Kwa hakika katuni hii inajieleza vizuri juu ya ushindami wa nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA huku wachoraji wengi wa katuni wakilitia maanani suala hili.

Mwanakwetu anaikamata katuni ya tatu ambayo iliyochorwa na Said wa Michael wa DW Kiswahili tena na kupachikwa katika kurasa za DW Kiswahili, hapa ndugu huyu anaonesha mandhari mbili, moja ya ndani ulingoni ambapo kuna sura za jamaa wawili Mbowe na Lissu, Ndugu Mbowe anasema nafikiri ulingo huu unaniifaa zaidi naye Lissu huku akiingia ulingoni anasema sijuhi majirani watasema nini tena?

Katika mandhari ya nje ya ulingo kunaoneka runinga moja kubwa ikiwa na sura ya Lissu na bango lenye maandishi kuwa safari hii nazichapa kuwania nafasi hii ya Uenyekiti, jamaa kando wanasema natamani jamaa jina lake likatwe iwe mwiko kugombea nafasi hii.

Kwa hakika mchoraji wa katuni hii bado nayeye anatilia maanani joto la ushindani wa nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA ambapo Ushindani wa namna hii haujawahi kutokea kwa chama chochote cha siasa tangu mwaka 1992 urejeshwe tena mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa Tanzania.


 

Katuni hii ya tatu inanipa nafasi ya kuikamata katuni ya nne ambayo imechorwa na Alwatan Masoud Kipanya ambapo kunaonekana jamaa wawili, mmoja kavaa sare za CHADEMA na mwingine za CCM, jamaa hawa wanaongea. Jamaa wa CHADEMA anamwambia jamaa wa CCM naona kipindi hiki mna raha sana. Naye Jamaa wa CCM anasema tena raha yenyewe haielezeki.

Mtayarisha wa makala haya anapoitazama katuni hii anakuwa na dhana kuwa hali ya changamoto ya CHADEMA kwa sasa inaonekana kuwa sherehe kwa Chama cha Mapinduzi na hii ndiyo dhana inayojenga na Masoud Kipanya katika katuni yake hii iliyozingatiwa pia na makala ya katuni.

Kwa hakika Mwanakwetu katika makala haya alikuwa na kitita cha katuni nne; Ile ya Tundu Lissu katikati ya ufagio na kizolea taka, ya pili ni ile Lissu na Mbowe wakipimana uzito katikati ya jiko la moto, ya tatu ni ya yale mandhari mbili za mpambano huu wa Lissu na Mbowe na katuni ya nne ni hawa jamaa wenye sare za CHADEMA na CCM wakitupiana maneno, ambapo Mwanakwetu anajiuliza kwanini suala la Lissu na Mbowe limetiliwa maanani mno na jamii kubwa hapa Tanzania?


 

Jibu lake ni moja tu CHADEMA ni chama chenye mvuto mkubwa baada ya CCM eneo la Tanzania Bara ambalo ndilo lenye eneo kubwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo ni jambo la kutiliwa maani na siyo jambo la kuwekwa kisogoni.

Basi kwa maelezo hayo ndiyo na mimi natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo .

Kumbuka

“CHADEMA INAMVUTO ENEO KUMBWA BARA YA TANZANIA.”

Nakutakia heri ya Krisimasi na Mwaka Mpya.

makwadeladius@gmail.com

0717649257







 

 

0/Post a Comment/Comments