TUNATEMBEA MBELE KIFUA

 


Adeladius Makwega-Bunda MARA

 

Majira ya Jioni ya Disemba 5, 2024. Mwanakwetu akiwa na wenzake wawili; Musa Makali na Gidion Chilingani wanafika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mara (Mara Girls Secondary School). Eneo hili ambalo linaonekana ni tulivu sana na kwa mbali yakionekana majengo kadhaa, mabinti wakipita, sauti za kuku na ndege zikisindikiza mandhari haya tulivu. Huku kwa mbali masikio ya Mwanakwetu yanabebwa na mvumo wa mawimbi yakimkaribisha mgeni Mwanakwetu katika shule hii ya umma nchini Tanzania. Hapo hapo huku anamuuliza rubani wa safari hiyo ndugu Chilingani Mgogo wa Dodoma naye Muwaha(Mkubwa) Chlingani anajibu,

“Unajua Mkoa wa Mara kama vile umekumbatiwa na Ziwa Victoria , sawa na mtoto aliyepo katika tumbo za uzazi wa mama mjamzito, huu mkoa umeingia ndani ya Ziwa Victoria, kila unapozunguka unakutana nalo, ukiwa mgeni lazima uchanganyikiwe, hapa tulipo ni umbali mchache lilipo Ziwa Victoria.”

Mwanakwetu alipotazama Google Map ilimjulisha kuwa hapo alipo ni Wilaya ya Bunda. Hapo hapo alimtafuta Katibu Tawala wa Bunda lakini mtandao wa simu uligoma kumpa ushirikiano, hivyo alifika katika ofisi ya walimu na kukutana mwalimu Suzan Mwisawa, aliyewapokea vizuri na kutoa ushirikiano mkubwa .

Wakiwa wanafanya mazungumzo ya utambulisho gafla ikasikika kengele ngee ngee ngengeeeeee…kundi la wanafunzi wa kike karibu 300-walijongea mstarilini na ukaimbwa wimbo huu,

“… Mambo mema ya kwetu Afrika , Tanzania Tanzania Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote…”

Kumbuka msomaji wangu hapa sasa Mwanakwetu anajitambulisha kuwa anatokea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na wamefika hapo kufanya makala za miaka 63 ya Uhuru wa Iliyokuwa Tanganyika hasa yale mafanikio ya Sekta ya Elimu na shule hii ikiwa chaguo la Mwanakwetu, walimu hawa wakasema hakuna neno.


 

Nako huko nje ya ofisi aliyopo Mwanakwetu nyimbo zinaendelea kusikika na sasa ukaimbwa wimbo mwingine,

“Mungu Ibariki Tanzania, Dumisha Uhuru na Umoja, wake kwa waume na watoto, Mungu Ibariki Tanzania na watu wake, Ibariki Tanzania, Ibariki Tanzania , tubariki Watoto wa Tanzania.”

Mara baada ya wimbo huo ndimi za Mwanakwetu zinakutana na mwanafunzi wa Kidato cha tano mwenye jina la  Vitendo Mohamed Ndunda ambaye kwa asili ni mzaliwa wa Nachingwea huko Mkoani Lindi nyumbani kwa Kassimu Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu 2015 hadi 2025 na ndiye aliyeweka jiwe la msingi la shule hii. Mwanafunzi Vitendo Nyadunda akisoma masomo ya sayansi akasema,

“Nipo Mara kimasomoa tangu mwaka 2019, kwa upande wangu nina furaha kusoma hapa, hatuna sufuri, wala daraja la nne, huku tukiwa na daraja la tatu chache, tuna majengo mazuri, Mara Tunatembea Mbele Kifua.

Tunamshukuru sana mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga pesa za ujenzi wa shule hii. Sisi mabinti tunaotoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Hapa tupo wanafunzi kama 200, tunaomba maboresho katika majengo ambayo ujenzi wake unaendelea uendelee. Kwa hakika tuna walimu wa kutosha.”

Mwanakwetu baada ya kupokea kwa heshima na taadhima maelezo ya mwanafunzi huyu alikumbuka takwimu kutoka Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evansi Alfred Mtambi juu ya Idara ya Elimu zinanadi haya,

“Mkoa wa Mara unaendelea na ujezni wa shule za msingi mpya 17 zenye madarasa 224 na kukarabati madarasa 113 katika shule 52, madarasa ya mfano 18 na madarasa ya elimu maalumu 2, sambamba na ujenzi wa miundo mbinu kupitia mradi wa Boost wenye thamani ya shilingi Bilioni 12.7. Isitoshe ujenzi wa sekondari mpya 21 kupitia mradi wa SEQUIP shule zenye thamani ya shilingi bilioni 13.5.”

Hapo hapo Mwanakwetu akakumbuka kumbe hata hii Shule ya Wasichana Mara ni miongoni mwa shule mpya ambazo zinapokea kidato cha kwanza kwa mara ya kwanza Januari 2025. Mwanakwetu akiwa katika tafakari ya hayo gafla akasikia wimbo mwingine,

“Shule ya Sekondari ya wasichana Mara ni shule ya mfano ya kimkakati kutimiza nia ya Serikali kuinua taalumu kwa wasichana, pongezi serikali kutujali na sisi tunatoa ahadi kusoma kwa bidii na imani yetu kuyafikia malengo haya ya Serikali.”

Mwanakwetu sasa akakutana na mwanafunzi Sofia Bernad Ngumbi anayetokea Dar es Salaam na yeye anasema haya,

“Nipo hapa kusoma kidato cha tano na sita, haya ni mazingira tulivu unayoweza kusoma, namshukuru mama Samia kwa kutuwezesha kusoma vizuri na naishukuru Serikali kwani kila tunachoomba inatufikishia kwa wakati mathalani walimu wa masomo yote ya sanyansi wapo na tunafanya vizuri sana, Serikali itegemee kuvuna matunda mema kutoka kwetu.”

Mwanakwetu akiwa hapo alitamani kusikia nini kinasemwa na wanyeji wa eneo hili ambapo alikutana na Bi Elizaberth Paskali ambaye pia uwepo wa shule hii imemsaidia kupata ajira.

“Hapa mwanzoni eneo hili lilikuwa ni shamba ya kijiji tu na hata kulimwa hatukuliwa na sasa limekuwa shule huku tukipokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali, tunapata ajira na sasa maisha yanakwenda na shule hii itapokea wanafunzi kutoka hapa hapa kijijini.”

Naye Mkuu wa shule hii Mwalimu Mwisawa alimalizia kwa kusema kuwa Shule yao ipo vizuri na wanashukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada wanazofanya katika maboresho ya elimu ya watoto wa Kitanzania.

 

 

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yupo katika Shule ya sekondari ya Wasichana ya Mara Wilya Bunda mkoani Mara, huku sasa sauti za wanafunzi zikisikika, ndege wakilia na mawimbi ya Ziwa Victoria yakishika kasi, huku ardhi na majengo kando ya shule hii ya Kimkakati yakiwa imara mithili ya ngome cha Chifu Mkwawa Lilinga.

Mwanakwetu akiwa katika viunga vya shule hii alibaini kuwa lipo jambo dogo ambalo aliumwa sikio linalohitaji kufanyiwa kazi,

“Baba hupatikanaji wa sodo(ped) siyo wa bure, tunajinunulia wenyewe kama mahitaji ya mengine ya sabuni na mafuta ya kupakaa kutoka fedha tunazopewa na wazazi. Mwenzako akikwamu unamuazima pisi ya sodo ajisitiri. Tunaiomba serikali itusaidia tuwe tunagawiwa sodo hizo bure.Ila baba usinitaje kama nimesema haya.”

Majibu ya hoja hii yalikuwa ni haya,

“Sodo zinatolewa kwa dharula tu.”

Kwa taarifa alizonazo Mwanakwetu ni kuwa mkakati wa Serikali ya Tanganyika huru na hata baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka ule 1964, sodo zilitolewa bure kwa mabinti wote nyakati zote wakiwa katika siku zao katika shule za umma, hali hii iliendelea hadi mwanzoni mwa miaka 1990 utoaji wa sodo mashuleni ulisitishwa kutokana na hali mbaya ya uchumi.


 

Msomaji wangu tambua jina la Binti Sodo litabaki kuwa siri ya milele ya mtayarishaji wa makala kama mwanahbari na kama mzazi.

Hayo sasa yalikuwa majira ya jioni, huku jua likiwa limeshazama, nayo sauti iliyosalia ni mawimbi ya Ziwa Victoria Mwanakwetu hakufahamu kama maji yalikuwa yanakupwa au yanajaa, sasa Mwanakwetu na wenzake kuingia garilini na kuanza safari ya kurudi Musoma Mjini .

Msomaji wangu jambo la kutilia maanani ni kuwa Shule ya Wasichana Mara ni miongoni mwa shule mpya katika katika Mkoa wa Mara ambapo sasa inakamilika na imeanza kupokea wanafunzi kwa vidato kadhaa, huku ni miongoni mwa shule zinanufaika na karibu bilioni 26 katika sekta za elimu kutoka serikalini na wadau wa elimu katika mkoa wa Mara.

Kwa hakika hoja ya soda ni jambo dogo ambalo likiwekewa utaratibu linaweza kutatuliwa vizuri ambapo kwa mataifa jirani mathalani Kenya Sodo zinatolewa bure kwa mabinti wote waliopevuka Shule za Msingi na Shule za Sekondari(Shule za Upili) kwa hili Tanzania hatuwezi kushindwa isitoshe kwa sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanazania ni mwanamke.

Mwanakwetu Upo

Kumbuka

“Mara Tunatembea Mbele Kifua.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257 


 




 














0/Post a Comment/Comments