FUNGUKA MAPEMA

 



Adeladius Makwega -Musoma MARA.

“Kijana mmoja ambaye alikuwa katika msafara wa Waziri Bashungwa akiwa mpiga picha za video awali alihamishiwa GCU kutoka Habari Maelezo kuongeza nguvu. Maana alikuwa anapiga picha vizuri, awali nafasi hiyo alikuwepo kijana mwingine ambaye alirudi Maelezo kwa hiyo Idara Hbari Maelezo wakatoa kijana mwingine kwenda kuongeza nguvu. Kijana huyu kutoka Bukoba hakukaa muda mrefu hapo ndipo Waziri Bashungwa anakwenda Wizra ya TAMISEMI na Mchengerwa anaingia Utamaduni. Kijana huyu akawa analia, Kaka Makwega nafanyaje? Heri ningebaki Maelezo? Haya mambo mimi siyaelewi.Wenzangu wameshaondoka nafanyaje masikini wa Mungu?”

Kijana analia, shauri hilo mbele ya Mwanakwetu anafanyaje?Mwanakwetu akamwambia maneno haya,

“Bwana Mdogo Usilie, haya mambo ya kazi ni fursa tu, hapo ulipokuwepo alikuwepo kijana mwenzako wa Mbeya mbona aliondoka? Huku akiendelea na maisha yake vizuri? Kila fursa ina wakati wake na inapokuja tambua Mungu Kapenda, kuwa na amani, wewe ni mtumishi wa umma. Kwani Wewe Mganda ? Wewe ni Mtanzania kama alivyo mtu yoyote yule?

Mimi nitamwambia msaidizi wa Waziri na Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi anajua namna GCU inavyofanya kazi. Nikupe siri . Mimi Video Editting na hata kupiga picha nafahamu vizuri ila sipendi watu watambue hilo,nakataa kusumbuana na watu na umri umesonga, hapa kitengoni hakuna mwingine anayefahamu hilo, hii fursa ni yako wewe milele, tulia tuu ufanye kazi.”

Kweli aliambiwa Msaidizi wa Waziri Mchengerwa na kwa hakika Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi alikuwa anajua namna kazi zilivyokuwa zinafanywa na GCU na ofisi za viongozi. Baada ya majuma matatu manne upepo ulitulia na watu walirudi likizo na kuendelea na nafasi zao. Yule kijana nadhani bado hadi sasa yupo na Waziri Mchengerwa huko alipo akifanya nae kazi.


 

Miongoni mwa maamuzi yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mwaka 2022 ni uteuzi wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo ndugu Mohammed Mchengerwa alikalia kiti hicho baada ya kuundwa Wizara Mpya. Huku Idara ya Habari Maelezo kuunganisha na Tekinolojia ya Habari ambapo hivi majuzi Disemba 2024 mambo haya yalirejeshwa kama ilivyokuwa awali.

 

Nakuomba msomaji nikutoe hapo ulipo nikupeleke Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na baadaye Wizara ya Utamaduzi, Sanaa na Michezo muda mchache kabla ya maamuzi haya na muda mchache baada ya maamuzi haya ambapo Mwanakwetu alikuwepo katika Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.Wakati huo ndugu Innocent Bashungwa na Pauline Gekul wakiwa Waziri na Naibu Waziri na baadaye ndugu Mchengwrwa na Pauline Gekul.

 

Kutokana na Serikali kuelekea katika maamuzi haya, watu wenye nafasi walikuwa na hofu na nafasi zao na kwa hakika kulikuwa na taharuki tangu wakubwa hadi wadogo huku jamaa wengi waliomba likizo, mazungumzo nyuma ya pazia kulikuwa na utani kuwa kuna watu wanakwenda likizo kutazama kwa mafundi upepo ukoje? Ili wayaweke mambo sawa. Watumishi wasio na madaraka, wasio na hofu wakawa wanacheka koridoni.

“Jamaa kenda kwa Sangoma kaambiwa yaani usirudi hadi mama ayaweke mambo sawa, alafu ukiwa unatoka Ofisini muamchie Ofisi mtu ambaye hayawahi kukaimu hata siku moja, hiyo ndiyo salama yako.”

Mwanakwetu akakabidhiwa kitengo kwa muda, hiki kipindi cha mpito wakati kikipamba moto, siku moja kikaoni Msemaji wa Serikali kabla ya kikao hakijaanza, watu wapo ukumbini wanazungumzazungumza, ikaibuka simulizi moja ya Rais John Magufuli alivyokuwa hai, Msemaji wa Serikali akaongelea yale mapambano ya ugonjwa wa Korona, kumbuka wajumbe halali wa kikao akiwamo Mwanakwetu tunamgonja Waziri Bashungwa. Msemaji wa Serikali akasimulia kisa cha Korona alafu akasema

“Daaa, jamani, yaani, ngoja nistaafu, nitaandika vitabu viiiiingi.”

Mwanakwetu akasema kwa sauti ya chini chini akimwambia aliye kando yale akiwepo  Mkurugenzi mmoja wa Idara za wizara hii,

“Jamaa anagoja kustaafu?Aaandike sasa, unajua taarifa hata kama nzuri kiasi gani baada ya miaka 20 huyo unayezungumzia watu watakuwa hawamfahamu, kama unaandika makala au kitabu, andika sasa.”

Mkuu wa Idara akasema kwa kunong’ona,

“Hilo gumu sana, ngoja tungoje astaafu atuandikie vitabu vyake hivyo viiingi.”

Baada ya majuma kama mawili Rais Samia ndipo akaunda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Ndugu Mchengerwa akafika kuanza kazi akipokelewa vizuri na kikao cha kumpokea Mwanakwetu alikuwepo na ndiyo mara ya kwanza Mwanakwetu kuingia Ofisini kwa Waziri. 

Kwa wale wanaokumbuka Mchengerwa aliripoti pamoja na Balozi Said Yakub, Balozi wa Tanzania nchini Komoro kwa sasa ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Yakub yeye ni bingwa kwa kuandikia kwa kutumia mkono wa kushoto.



 

Ndugu Mchengerwa akaongea sana pale Ofisini huku Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi akawa anapokea maelekezo. Dkt Hassan Abbasi ni Kijana mchapa kazi, akawa anapokea maelekezo mengi tu ya Waziri Mgeni.

Katika haraka za kuondoka Idara ya Habari Maelezo Kitengo cha Mawasiliano Serikalini walibaki kama walivyo hapo Utamaduni kuipa nguvu wizara mpya akiwamo Mwanakwetu. Kumbuka watu waliokwenda likizo kwenda kuyaweka mambo sawa , hapa Mwanakwetu alikuwa yupo golini.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika msomaji wangu haya yote yanakumbukwa na Mwanakwetu baada ya maamuzi ya hivi karibuni ya Rais Samia Kuirejesha Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo ambayo ni maamuzi sahihi. Haya yanayoandikwa yanasaidia sana wale wanaofanya maamuzi wayafahamu na kisha wawe wazito kuhamisha hamisha idara hizi maana mwisho wa siku zinaleta kero kwa watumishi wa umma , vijana hadi wanatoa michozi na wanakuwa hawana amani na kazi hazifanyiki kwa ufanisi kipindi cha mpito.

Shabaha ya pili ni kwa wale wanaofahamu mambo, mkumbuke kuandikaandika sasa, mkisema mnangoja kustaafu, jamani ya kesho anayeijua ni Mwenyeezi Mungu peke yake, andika sasa ili jamii iweze kujifunza na kama kuna maboresho yafanyike.

Kwa sasa hivi kila kitu kinaweza kuwa kizuri lakini baadaye kwenye vitabu vyake mtu keshastaafu anafunguka mengi wakati umeshapita, Ustadhi Funguka Mapema.

Kwa ukweli wa Mungu kwa kuandika sasa, kama anavyofanya Mwanakwetu kuna changamoto tele, zinazoweza kusimuliwa na zingine ngumu kusimuliwa lakini ipo heshima na thawabu kubwa kwa Mungu yeye ndiye mlipaji wa haki..

Msomaji wangu najua una swali je huyu anayetakiwa kuandika sasa ni Balozi Mobhare Matinyi au Gerson Msigwa? 

Jibu lake ni hili, Balozi Matinyi kafanya kazi na Mama wakati Korona ishaondoka lakini Gerson Msigwa kafanya kazi wakati na mze Magufuli wakati mapambano ya Korona, yeye ndiye aandike sasa.


 


 

Msomaji wangu je makala haya uchambuzi yaitwaje?

”Hama Hama za Idara, Kama Unaandika Andika Sasa, Kwani wewe Mganda? Au Ustadhi Funguka Mapema. ”

Mwanakwetu anachagua Ustadhi Funguka Mapema.

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 




0/Post a Comment/Comments