CHAKULA MASOMONI AJENDA YA KUDUMU

Adeladius Makwega–Musoma,MARA

“Ukiwa kijijini unaweza ukawa na kuku wako wengi majogoo kwa temba (tetea), majogoo yako yanaweza yakawa yanapanda vizuri na tetea zako wanataga vizuri sana, kuyalalia na hata kutotoa vifaranga vizuri mno lakini ukautamani uzao wa jirani yako, ukachukua kuku kwake uende kuwafuga kwako ili kuongeza uzao wa kuku wako.

Kinachokufanya kuchukua kuku wa jirani ni tamaa ya kibinadamu, kwa hiyo unapoleta kuku mgeni katika banda lako kuna mambo makubwa mawili unaweza ukawa na manufaa lakini pia inawezekana ikawa vinginevyo.”

Anachokifanya mfugaji huyu wa kuku kinaweza kulingana na mchezaji wa karata,

“(Carta-Kireno, Karatasi-Kilatini, Cards-Kiingereza) Hasahasa mchezo wa Arubasitini. Katika mchezo huu mchezo wa sitini na nne, huwa kuna karata 36, unachezwa na watu wawili, wanne au sita ambapo ulaji wa karata hutegemea karata inayotawala mchezo (Alalae) na mshindi hupata alama zaidi ya 60 (Wahedisitini).

Katika mchezo huo unapopata karata inayotawala mchezo (Alalae) au kupata karata dume, jike la karata nyingine ukicheza vizuri zina faida , kusaidia kupatikana kwa mshindi. Huku yule anayeshindwa katika mchezo inawezekana akapuna magarasa ambazo ni karata zisizo na thamani yoyote ile, mtu huyu huambulia patupu.”

Msomaji wangu ebu nikurudishe nyuma kidogo, Mei18, 2017 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadiki alijiuzulu na Rais John Magufuli aliliridhia kujiuzulu huko na Juni 3, 2017 akamteuwa Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa huo. Kukiwa na hoja mbona mpinzani kateuliwa? Wengi wakiwa hawafahamu uwezo wa mama huyu.


 

Kwa maeneo mengi wakati huo suala la elimu bure lilikuwa linasumbua sana, maneno kama msitoe michango, sera ya serikali ni elimu bure yalisemwa. Maeneo mengi ya Tanzania kelele zilipigwa mno, lakini sikusikia Mkoa wa Kilimanjaro, Mwanakwetu ikambidi aanze kufuatilia hivi huku Kilimanjaro mbona kelele za elimu ya bure za kukataa kuchangia elimu sizisikii?

Jibu likapatikana kwa rafiki ya Mwanakwetu Mwalimu Rehema Bonifase (Cheusi Mangala) , mchaga wa Tandika Dar es Salaam. aliyesoma naye zamani akiwa Tambaza naye Cheusi Mangala akiwa Zanaki. Baadaye kufundisha naye pale Dar es Salaam International School mwaka wa 2003-2004, wote wakisoma Chuo Cha Ualimu Kasulu miaka hiyoo.

 “Mwanzoni jambo hilo lilikuwa gumu , lakini viongozi wa dini walishirikishwa vizuri, jambo hilo likaeleweka vizuri , ikiwa kila Jumapili Kanisani, kila Ijumaa Msikini matangazo ya kusisitiza michango ya elimu yalitolewa-hoja wazazi wote kulipa pesa ya chakula cha mchana shuleni.

Zikaundwa kamati za wazazi za shule ambazo zilikuwa zinasimamia suala hilo, wanakusanya fedha, wananunua chakula wanawapikia watoto wao na kuwagawia wenyewe.

Walifungua akaunti zao, wanayasimamia mambo yao wenyewe, wanafunzi wanapikiwa kande na siku zingine wanapikiwa mseto wa mchele na maharagwe badala ya wanafunzi kutoka shuleni saa nane walianza kutoka saa kumi jioni na hata muda wa kusoma uliongezeka.”

Walikwenda mbali mno,Cheusi Mangala alimwambia Mwanakwetu kuwa kila viongozi wa dini wa mkoa wa Kilimanjaro wakishirikiana wakisema, Waumini/washirika nendeni mkatoe pesa ya chakula cha mchana cha watoto wenu shuleni, usijidanganye kuja kutoa sadaka/zaka wakati mtoto wako haujamlipia pesa ya chakula cha mchana shuleni. Kwa hakika Mashekhe, Mapadri na Wachungaji walifanya kazi kubwa katika hilo.

“Hata kama elimu bure, hao wanaonadi elimu bure mnadhani wanaweza kumnunulia sare za shule mwanao? Hata kama elimu bure, hao wanaosema hivyo wanaweza kumnunulia mwanao chakula cha mchana? Hata kama elimu bure, hao wanaopaza sauti juu ya hilo wanaweza kumnunulia mwanao madaftari ya kuandikia shuleni?”

Viongozi wa dini waliingia hadi katika kamati za shule hizo mathalani kuna shule inaitwa J.K Nyerere Moshi Mjini, miongoni mwa wajumbe wa kamati ya shule ya chakula alikuwa Mchungaji Nkya ambapo wakati huo aliongoza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ushariki wa Majengo.



 

Cheusi Mangala mchaga wa Tandika Temeke Dar es Salaam akawmabia Mwanakwetu,

“Mama Anna Mghwira alikuwa na PHD ya theolojia kwa hakika alitumia elimu hiyo kujenga ushirikiano na viongozi wa dini na kweli chakula cha mchana mashuleni mkoa huo si tatizo tena na wazazi waliitikia.”

Japokuwa Mama Mghwira amefariki lakini Kilimanjaro itaendelea kunufaika na chakula cha mchana mashuleni, kwani nin hakika wanafunzi wa mkoa huo wataendelea kufanya vizuri zaidi na zaidi kitaaluma Kitaifa.

Natambua yapo maeneo yalijaribu kuhamasisha hilo lakini mwisho wa siku waliogopa pengine kutumbuliwa, wakakaa kimya, kimya kabisa, ziii kama maji ya mtungini na baadaye na hata shule zilizokuwa zinakula chakula cha mchana zikakacha huo mtindo na hawa jamaa hata kama walipona kutumbuliwa wakati wa John Pombe Magufuli lakini baadaye walitumbuliwa, huku watoto wetu sasa hawali chakula cha mchana shuleni.

Nakuuma sikio msomaji wangu kuwa mie shule za kwetu wanakula vizuri wali na maharage na muda mwingine wali na kunde/mbaazi.

Maswali ubaoni ni haya,

“Je wewe kama kiongozi wa kata, shule zako wanafunzi wa kutwa wanakula chakula cha mchana shuleni? Wewe mbunge wa jimbo, je jimboni kwako wanafunzi wa kutwa wa shule za umma zote umehamasisha wazazi wachangie watoto wao wale chakula cha mchana shuleni? Wewe mkuu wilaya ama wewe Mkuu wa mkoa katika mkoa wako ni shule ngapi za umma zinakula chakula cha mchana shuleni?”

Hapa ndipo anapozaliwa Katibu Mkuu wa wizara … na shule ile ndiyo kasoma. Ukienda hapo uliza je wanafunzi wanakula chakula cha mchana shuleni? Jibu lake hawali. Ukifuatiliwa ndugu hao katika fomu zao za likizo wanakwenda makwao, basi ninawauma sikio jamani muende kuhamasisha watoto wetu wale chakula cha mchana shuleni ili kuongeza virutubisho mwilini na kukuza uelewa wanafunzi wafanye vizuri kimasoma, tupate makatibu wakuu na maprofesa wengine kutoka maeneo yenu. 


 

Uhamasishaji wa Chakula cha Mchana Shuleni siyo suala la TAMISEMI tu hii ajenda mtambuka na siyo kuwaachia Mkurugenzi Watendaji , Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, hili ni jukumu la kila Mtanzania.

“Mama Mghwira amefariki huku akiacha shule zote za umma za kutwa Kilimanjaro wanakula chakula cha mchana, hilo ni jambo kubwa la ustawi wa maisha ya binadamu na kama mambo yameharibika huko Kilimanjaro basi ni sasa, narudia tena kama mambo yaharibike basi ni sasa.

Kumbe uteuzi wa Mama Anna Mghwira kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ilikuwa ni sawa na kupata karata ya mchezo (alalae) kwa Arubasiti na pia kama mfugaji wa kuku basi tetea wake alitaga, kuyalalia na kutotoa mayai yote na vifaranga vyote vi hai na vinakuwa salama bila kuchukuliwa na Mwewe.”

Natambua fika siyo kwamba ukichukua kuku wote wa jirani watafanya hivyo, watafanya vizuri kama Arubasitini maana Mwanakwetu unaweza ukalamba magarasa, kumbuka magarasa huwa mengi kuliko madume, jike, mzungu wa nne, mzungu wa tatu na mzungu wa pili.

Mwanakwetu anahitimisha kwa kusema kuwa kwa Anna Mghwira CCM ya Magufuli kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro haikulamba garasa bali ililamba Alalae.

 


Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa makala haya shabaha ni kuhamasisha jamii ya Watanzania kuweka mikakati ya kupatikana kwa chakula cha mchana shuleni kama walivyofanikisha mkoa wa Kilimanjaro ili watoto wetu wapate elimu ambayo ni msaada kwa jamii yote hapo mbeleni.

Makala haya yametayarishwa kwa sababu Disemba 18, 2024 Mwanakwetu alishuhudia Kikao cha Tathimini ya Elimu cha Mkoa wa Mara cha miezi miwili, huku kikiwa chini ya Uenyekiti wa Katibu Tawala Mkoa wa Mara ndugu Gerald Kusaya, akisisitiza hupandishaji wa Takwimu za Lishe Mashuleni , akisema wazi kuwa hufuatiliaji umeanza na akiwaambaiwa maafisa elimu wa Halmashauri zote wasije kuonana wabaya maana kipenga kimeshapigwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi hata katika RCC ya Disemba 2024 amesisitiza hilo na watakutana naye uwanjani Shule zitakapo funguliwa, huku Mkoa wa Mara takwimu zake zinaonesha kuwa hadi Disemba 2024  alama ni 54% tu.

Kwa tafsri ya Mwanakwetu kama kuna shule 100 basi ni shule 54 tu ndizo zinamudu katika hilo, 46 wakiwa kando. Msomaji wangu kumbuka Mkoa wa Mara ndipo anapozaliwa Mwalimu Julius Nyerere ambaye ambaye alikuwa kinara wa falsafa ya Elimu Kwa Wote.

“Kwa hiyo mzazi asiyechangia chakula cha mchana kwa mtoto wake, hapa anapingana na hoja ya Mwalimu Nyerere ya elimu kwa wote, kumbuka wewe mzazi wa mkoa Mara Julius Nyerere ni ndugu yako, ambaye kwa hakika akiwa kiongozi amefanikisha huyu hata huyu anayeandika makala haya akabahatika .”

Mwanakwetu kwa makala haya na kwa heshima ya Julius Nyerere maarufu kama Mchonga Meno anawaomba wadau wote wa elimu mkoa wa Mara haya wajitahidi watoto wetu wapate chakula cha mchana shuleni, huku anatambua makala haya yanaweza kutumika na hata kwa mikoa mingine ya Tanzania na Taifa lolote ambalo linahitaji kuhakikisha watoto na wanafunzi wake wanakula chakula cha mchana shuleni na waweze kuongeza ufaulu shuleni.

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Chakula Shuleni Ajenda ya Kudumu.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 


 


 


 

 

0/Post a Comment/Comments